Siku chache baada ya Polisi kuthibitisha kwamba Naomi Marijani ameuawa, uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba maandalizi ya mauaji yake yalifanyika wiki moja kabla, huku akiishi na mtuhumiwa wa mauaji katika nyumba moja.
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba kulikuwepo na misuguano baina ya Saidi (Meshack) Hamis Luwongo na mkewe, marehemu Naomi Marijani.
JAMHURI limethibitishiwa pasi na shaka kwamba misuguano baina ya wawili hao inatajwa kusababishwa na mmoja wao kuwa na kipato zaidi ya mwenzake. Naomi anatajwa kuwa na ukwasi kuliko mumewe, wakati mwanamke huyo akijizatiti kwenye biashara, mumewe alikuwa dalali wa mashamba, nyumba na viwanja.
Chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi kinasema kwamba kwa mujibu wa taarifa za awali, Saidi alianza kupoteza imani kwa mkewe kutokana na ukwasi aliokuwa nao, huku baadhi ya masuala muhimu ya ndoa yakidorora baina ya wawili hao.
“Unajua mtuhumiwa amekiri kwamba kumekuwepo na changamoto kadhaa baina yao… lakini anakiri kwamba alianza kupanga kumuua mkewe wiki moja kabla ya kutekeleza azima hiyo.
“Aliwaandaa vijana wa kuchimba shimo la kumzika mkewe huko Marogoro, Mkuranga shambani kwake. Halafu kazi hiyo ya kumuua, kumchoma na kumzika kimyakimya ikafanyika baadaye, huku watu wachache tu wakihusishwa kwa karibu.
“Tumepata rekodi ya mawasiliano ya simu zake zote mbili… tumekutana na mambo makubwa humo. Mengine sitayasema, maana watuhumiwa wataongezeka. Kazi ya kuchimba shimo la kumzika Naomi ilifanyika Mei 9, siku ya Alhamisi.
“Mtuhumiwa amekiri kwamba siku ya Jumatatu, Mei 13 kulikuwa na mzozo mkali baina ya wanandoa hao… hali ikawa mbaya zaidi siku ya Jumatano, Mei 15 ambapo mtuhumiwa alimpiga mke wake na haijathibitika bado kama alimchoma moto akiwa amekufa ama kuzirai.
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba, mtuhumiwa wa mauaji hayo amekuwa na washirika wake wa karibu, huku mmoja akitoa gari lake aina ya Toyota Pick – Up lenye namba za usajili T 206 CEJ kwa ajili ya kubeba mabaki ya mwili uliochomwa kisha ukabebwa kwa kuchanganywa na mbolea kuelekea shambani.
JAMHURI limebaini kwamba siku ya Jumatano, Mei 15, saa 05:41 usiku, siku ambayo Naomi aliuawa, mtuhumiwa ilipiga simu namba 071046..90. Mwanzo, mtu huyo hakupokea, akatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi usemao: “Huku tayari…” baada ya dakika kadhaa namba hiyo ikapiga katika simu Na. 0688318301 ya mtuhumiwa na wakazungumza kwa dakika 41:05.
JAMHURI halikufahamu mazungumzo hayo marefu baada ya ujumbe ‘Huku tayari’ yalihusu nini. Aliyetumiwa ujumbe huo namba yake inaonekana kutumika akiwa wilayani Bukoba usiku huo.
Taarifa za ndani ambazo JAMHURI limezipata zinasema suala la mauaji ya Naomi limewagusa watu wa aina mbalimbali, hivyo polisi wanalifuatilia kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Chanzo chetu kinasema kwamba katika uchunguzi unaoendelea wameshindwa kuthibitisha endapo Naomi alifariki dunia kwanza ndipo akachomwa moto au vinginevyo. Taarifa kutoka ndani ya Polisi zinasema kwamba hakuna taarifa ya daktari ambayo imethibitisha kifo.
“Unajua hatujaweza kuthibitisha kama alimuua kwanza ndipo akamchoma… maana inawezekana kabisa kwamba katika purukushani hizo Naomi alizimia na mumewe akadhani ameshakufa na kuamua kumchoma moto,” kinasema chanzo chetu.
Jirani: Tulisikia kama bomu limelipuka
Nyumba ya Meshack (Hamis) lilikofanyika tukio la mauaji, imejengwa kwa ukaribu mno na makazi ya jirani zake, kiasi kwamba ni rahisi majirani kusikia ugomvi au tukio lolote.
Mmoja wa majirani (jina linahifadhiwa) akizungumzia tukio hilo amesema: “Siku moja tuliona moshi unatokea humo ndani. Baadaye tukasikia kama kitu kinalipuka, puuu, tukadhani anachoma takataka labda chupa zimelipuka. Sasa baada ya kusikia hizi habari za kumchoma mkewe ndipo tumerejesha kumbukumbu nyuma.
“Inawezekana ule mlio wa puuu kama bomu limelipuka, inawezekana kumbe kichwa kilikuwa kinapasuka. Ilikuwa muda wa jioni. Kwa kweli yule dada (Naomi) alikuwa mstaarabu, kama kuna msiba mahali anakupakia kwenye gari lake, anakwambia mama twende na hata wakati wa kurudi anakwambia, turudi. Lakini majirani hatukuwa na mazoea ya kuingia nyumbani kwake.
“Alikuwa (Meshack) anakaa hapo (anaonyesha) … anacheza drafti, kila baada ya muda fulani anarudi nyumbani kwake. Wakati huo taarifa za kutoweka mkewe zilikuwa zimeshasambazwa… tukawa tunashangaa mbona hana wasiwasi? Mke wake kapotea yeye amekaa tu hana wasiwasi, kumbe inawezekana alikuwa anajua kilichotokea.
“Hata nyumbani alikuwa halali baada ya tukio, alikuwa akitoka huko, anaondoka saa tatu au saa nne kasoro usiku … anaondoka na gari lake. Tangu tukio hilo alikuwa halali, anakaa hadi muda wake wa kuondoka saa tatu au nne kasoro (usiku), hatujui alikuwa analala wapi.
“Anakaa hapo anaongea hadi wakifunga maduka naye anaondoka. Shughuli zake hata sijui. Anaondoka na gari lake muda huo ukifika, anakokwenda mimi sijui.”
Alipoulizwa walipoona moshi siku husika hawakusikia harufu ya aina yoyote, jirani huyo alijibu: “Harufu ‘hatukusikia’ lakini moshi tuliona. Siku hiyo tulikaa na mzee jioni, saa mbili kasoro, tukajiuliza mbona hapa kuna moshi? Lakini tukaona mwenyewe yuko pale (anacheza draft), tukasema kama kuna ‘shoti’ ya umeme atakwenda mwenyewe, lakini hakwenda.
“Ndipo tuliposikia mlio kama bomu. Ule moshi alitwambia kuwa anachoma mabaki ya minazi baada ya ‘kufua’ nazi. Hatukujua mengine ya ndani kwa kuwa hatukuwa na mazoea ya kuingia ndani kwake.”
Jirani mwingine anasema Meshack (Hamis) alikuwa anakwenda kwenye banda la kuku alikomchomea mkewe anageuza mwili sehemu ambazo zilikuwa hazijaungua, anarejea kwenye kijiwe anacheza ‘draft’.
“Alikuwa anaingia ndani mara kadhaa. Kijana aliyekuwapo anaweza kueleza vizuri. Inasemekana alikuwa anaugeuza mwili wa mkewe sehemu ambazo hazijaungua, kisha anaongeza mkaa na mafuta anachoma, anarudi kijiweni anacheza ‘draft’, anarejea ndani anageuza mabaki, kisha anayamwagia mafuta, anachoma tena, kwa siku tatu mfululizo hadi Mei 18, alipoamua kwenda kuzika mabaki shambani Mkuranga,” kimesema chanzo chetu.
Mwenyekiti azungumza
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kizani, Kata ya Somangila, wilayani Kigamboni – Dar es Saalam, Seif Nassoro, amelieleza JAMHURI namna alivyopata taarifa za tukio hilo la kuuawa kwa Naomi Marijani.
Anaanza kwa kueleza kuwa katika mtaa anaouongoza ndipo yalipo makazi ya Meshack, na Julai 16, mwaka huu alipata taarifa za kuitwa Kituo cha Polisi cha Mjimwema – Kigamboni na alipofika alimkuta Mkuu wa Kituo hicho akiwa na mtuhumiwa (Meshack).
“Nilikuta mkuu wa kituo pale, akaniuliza kama ninajua chochote kilichotokea katika mtaa wangu. Mimi nikamjibu hakuna tukio. Wakati nikiwa nimesimama pale Mkuu wa Kituo akamwambia mhusika mwenyewe anieleze kwa kifupi nini kimetokea.
“Kwa maelezo yake mtuhumiwa mwenyewe alinieleza kwamba amemuua mke wake na amemteketeza kwa moto, kwa kweli nilisisimka na kuogopa,” anaeleza Nassoro.
Anasema mtuhumiwa aliwaambia polisi kwamba alitumia magunia mawili ya mkaa na lita tano za mafuta kumteketeza kwa moto, na kwamba tukio hilo alilitekeleza ndani ya makazi yake.
Baada ya maelezo yake akiwa kituoni hapo, Nassoro anasema kuwa saa 10 jioni askari waliambatana na mtuhumiwa hadi nyumbani kwake kuona sehemu tukio lilipotendeka.
“Tulifika nyumbani kwake, akatuonyesha banda la kuku alikokuwa amechimba shimo na kumchomea mke wake, pale hatukupata chochote. Akawaeleza polisi majivu alikwenda kuyazika Mkuranga kwenye shamba lake,” anaeleza Nassoro, na kuongeza kuwa yeye pamoja na Polisi baada ya kujiridhisha na hali waliyoikuta kwa Meshack, saa 12 jioni waliambatana naye hadi Mkuranga alikoeleza kuzika majivu ya mwili wa mke wake.
“Ni umbali wa mwendo wa saa mbili na nusu kwa gari kutoka hapa Kigamboni hadi kwenye shamba lake, kule tulikwenda hadi kijiji kinaitwa Sangatini, tulipofika pale tukaanza safari ya kwenda kwenye shamba lake,” anaeleza Mwenyekiti Nassoro.
Anasema baada ya kufika Kijiji cha Marogoro lilipo shamba lake walikuta mashimo matatu, shimo moja likiwa limepandwa mgomba, na baada ya hapo walifukua shimo hilo, shughuli ambayo ilimalizika saa 4 usiku na walibaini mabaki ya nguo na mkanda.
“Polisi walichukua mchanga wa eneo hilo uliokuwa umechanganyika na mabaki ya mkaa na kuupakia kwenye mifuko miwili ya kaki kwa ajili ya uchunguzi.
Safari ya Polisi kurudi kituoni ilichukua saa tatu, na saa saba usiku tulifika Kigamboni na kuendelea kumshikilia mtuhumiwa kwa uchunguzi,” amesema na kuongeza kuwa baada ya siku mbili Polisi walirudi nyumbani kwa Meshack wakaanza kuchimba kwenye mabwawa ya samaki yaliyopo hapo, lakini hawakubaini chochote.
Mwenyekiti huyo anaeleza kuwa mpaka tukio hilo linafanyika Meshack hakuwa na ushirikiano wa kutosha kwa majirani zake.
Naye, Frank Wangara, mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kizani amelieleza JAMHURI kuwa Meshack na mkewe kabla ya kuwa wanandoa walidumu kwenye uchumba kwa kipindi kirefu na kulikuwa na ugomvi wa kifamilia baina ya wawili hao.
Wangara amedai wakati uchomaji wa mwili wa Naomi unatekelezwa, majirani hawakuweza kuhisi harufu kwa kuwa mtuhumiwa alibuni mbinu ya kuzuia harufu hiyo isitoke.
“Mtuhumiwa aliwaeleza polisi kwamba alikuwa anatumia nguo, mabaki ya vifuu vya nazi, chupa za maji pamoja na viatu kuvichoma pamoja na mwili huo ili harufu itakayosambaa iwe na utata katika kubainika,” anaeleza Wangara.
Baada ya mauaji kilichotokea Mkuranga
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI katika eneo la tukio wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, umebaini mambo mazito kutoka kwa majirani wa mtuhumiwa Meshack.
Mkazi wa Kitongoji cha Sangatini, Kijiji cha Marogoro lilipo shamba la Meshack, Bibi Shakiri Ramadhani, amezungumza na Gazeti la JAMHURI kuhusu tukio hilo na kueleza kuwa kabla ya Meshack kuletwa na polisi kitongojini hapo siku kama tano zilizopita akiwa amefungwa pingu, mara ya mwisho alimwona shambani hapo mwezi Mei, mwaka huu.
Japo hakumbuki ni siku gani kati ya Jumamosi na Jumapili ya Mei, mwaka huu, anasema Meshack alifika nyumbani kwake akamsalimia na kumuomba amtafutie wafanyakazi wa kufyeka nyasi na kusafisha shamba lake.
Anasema alifanya kazi ya kutafuta wafanyakazi mara moja na kupata vijana wawili ambao Meshack aliwaonyesha eneo wanalotakiwa kusafisha kwa siku hiyo.
“Wakati shughuli zikiendelea, Kitwana Mkwewa aliambiwa amtafutie mtu wa kuchimba mashimo kwa ajili ya kupanda minazi ya kisasa na choo ambacho kingetumiwa na wafanyakazi atakaowaleta kwa ajili ya kulinda mifugo yake,” anasema.
Kwa mujibu wa jirani huyo, kazi ya kuchimba mashimo hayo ilifanywa na Kitwana akisaidiana na mwenzake na kwamba kazi hiyo ilikwenda sambamba na ukataji wa miti kwa ajili ya kujenga uzio.
Makazi ya jirani huyo yapo umbali wa mita 80, kusini magharibi mwa shamba la Meshack. Anaeleza kuwa hata yeye siku hiyo alionyeshwa eneo la kufyeka ili kuandaa njia ambayo inaweza kupitisha gari kuelekea kwenye eneo la Meshack.
Anasema baada ya kumdadisi Meshack, alimwambia anafanya maandalizi ya kupanda minazi ya kisasa, kufuga ng’ombe, mbuzi pamoja na makazi ya wafanyakazi ambao angewaleta kwenye eneo hilo siku za baadaye.
“Mimi ndiye niliyefyeka na kulima ile njia unayoona inaelekea kwenye eneo la tukio, siku hiyo alinilipa Sh 5,000 na alikuwa akitueleza kuwa mwaka huu anataka kufuga mifugo kwenye shamba lake,” anasema Shakiri.
Ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba siku hiyo Meshack alikaa shambani kwake tangu asubuhi hadi jioni na kwamba ilipofika majira ya saa mbili usiku ndipo aliondoka na hakuwahi kurudi tena.
“Shughuli zote zilifanywa siku moja na Meshack alisema anataka apande minazi ya kisasa na migomba,” anasema.
Anakumbuka siku hiyo Meshack alikuja na viroba vitatu; viroba viwili vidogo na kimoja kikubwa ambacho alisaidiwa na vijana pamoja na mtu mmoja aliyekwenda naye kuvishusha shambani, huku akijihami kwamba viroba hivyo vilikuwa vimejaa mbolea ya samadi.
Anasema ilipofika jioni vijana waliofanya kazi ile walilipwa na kuondoka huku wakiwaacha Meshack na Kitwana Mkwewa, anayesemekana kuwa msaidizi wake wa shambani kwa muda mrefu.
“Kitwana alimsaidia kushusha kile kiroba kikubwa. Sisi hatujui alikipeleka wapi, kesho yake tuliona vimebaki viroba viwili tu, hatukujua kingine kilikwenda wapi. Viroba vilivyobaki nadhani unaona yamebaki marundo mawili ya samadi huku kile kikubwa kikiwa hakijulikani kama kiliwekwa kwenye mashimo au lah!” anasisitiza.
JAMHURI limeshuhudia eneo la tukio likiwa limezungushiwa utepe wa njano wa Polisi, ambapo eneo hilo kumechimbwa mashimo manne huku shimo moja likiwa na urefu kati ya futi 4 hadi 5.
JAMHURI limezungumza na Kitwana Mkwewa, ambaye amekiri wazi kuhusika kwenye uchimbaji wa mashimo hayo, huku akisema yeye alihusika kuchimba mashimo matatu tu.
Kitwana anayataja mashimo hayo kuwa ni shimo moja refu kwa ajili ya choo na mashimo mengine mawili mafupi kwa ajili ya kupanda minazi, yote yakiwa ndani ya uzio.
“Mimi alinipa kazi ya kuchimba mashimo akiniambia kwamba anataka kujenga kambi ya wafanyakazi wake watakaolinda mifugo yake, aliyokuwa anapanga kuanza kufuga.
“Tulikubaliana niyachimbe kwa siku tatu, lakini nilishindwa kumaliza ndani ya siku hizo, siku ya nne nilimaliza mashimo yote… alinipigia simu kama mara mbili kuulizia kama nimemaliza, siku ya nne nilimpigia akaniletea hela yangu,” anasema Kitwana.
Kitwana anasema tangu amemaliza kazi hiyo hajawasiliana na Meshack hadi alipoletwa hivi karibuni na polisi akiwa amefungwa pingu.
Anasema mmoja wa polisi aliyekuwa ameambatana na Meshack alimuuliza kama anamfahamu mtuhumiwa huyo, naye akajibu kwamba anamfahamu.
“Polisi wakamwambia Meshack aniambie amefanya nini? Akaniambia, aligombana na mkewe na alimpiga hadi akafa, akamchoma na kumzika katika shamba lake,” anasema Kitwana.
Anasema siku ya kwanza polisi walifukua moja kati ya mashimo waliyoonyeshwa na Meshack, humo wakakutana na mabaki ya fuvu lenye meno mawili. Baadaye polisi walirudi wakalifukua tena hilo shimo na kupata meno mawili mengine kwenye shimo hilo.
JAMHURI lazungumza na mshukiwa
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba siku ya tukio Meshack alizungumza muda mrefu na watu kadhaa. Mmoja wa watu aliozungumza nao kwa muda mrefu ni pamoja na Ramadhani Magwisa mwenye namba ya simu 0659 173380.
JAMHURI limezungumza na Magwisa, ambaye siku ya tukio alitumia zaidi ya dakika 78 kuzungumza na mtuhumiwa wa mauaji (Meshack) kwa nyakati tofauti. Mahojiano yalikuwa hivi:
JAMHURI: Wewe ni Ramadhani Magwisa?
Magwisa: Ndiyo, jina langu…wewe ni nani?
JAMHURI: Naitwa…Mhariri wa Gazeti la JAMHURI. Nimekupigia kutaka kufahamu uhusiano wako wa Hamis ‘Meshack’ Luwongo. Unafahamiana naye?
Magwisa: Hapana simfahamu kabisa!
JAMHURI: Una uhakika? Mbona mmewasiliana sana kati ya Mei 15 hadi 17?
Magwisa: Ninahisi ni baba mwenye nyumba wangu… maana mwenye nyumba wangu anaitwa Hamis (Meshack), ila sifahamu jina lake jingine. Amenipangisha kwenye moja ya nyumba zake huku Geza.
JAMHURI: Mlikuwa mnajadili masuala gani kwa muda wote huo?
Magwisa: Unajua ndugu yangu masuala ya kujadiliana kodi… halafu kulikuwa na masuala mengine ya wapangaji wasumbufu. Ndiyo maana unaona tumezungumza muda mrefu. Kesho yake nilimpelekea pesa zake na nikaendelea na mambo yangu.
JAMHURI: Mbona inaonekana mmewasiliana hadi Mei 17?
Magwisa: Unajua vitu vingine siwezi kukwambia… lakini jambo la msingi ni kwamba tulikuwa tunazungumza masuala ya kodi ya nyumba na usafi wa nyumba yake.
Yaliyojiri
Wiki moja baada ya Gazeti la JAMHURI kufichua namna Said Luwongo, maarufu kwa jina la Meshack, kuwa ndiye mtuhumiwa namba moja wa kutoweka kwa mkewe, Naomi Marijani, Jeshi la Polisi limemhoji Meshack na amekiri kumuua na kumchoma moto mkewe, kisha kuhamisha mabaki ya mwili kwenda kuyazika shambani kwake.
JAMHURI katika toleo lake la wiki iliyopita namba 407 lilikuwa na habari kuu yenye kichwa cha habari “Ameuawa?” ndani likionyesha namna uchunguzi wake unavyoelekeza mtuhumiwa namba moja katika kutoweka kwa Naomi ni mumewe, Meshack.
Katika habari yake hiyo, JAMHURI liliwahoji watu mbalimbali akiwamo Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumuy ya Dar es Salaam, Camilius Wambura, ambaye pamoja na mambo mengine, aliahidi kuongeza nguvu kwenye upelelezi.
Kamanda wa Polisi (RPC) wa Temeke, Amon Kakwale, alitoa taarifa kwa umma ikielezea namna Meshack alivyokiri kumuua mkewe huyo, iliyosema:
“… kosa mauaji. Mtoa taarifa ni SP. Thobias Walelo, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kigamboni. Anaeleza kuwa mnamo tarehe 15.07.2019 majira ya saa 0800hrs huko Gezaulole, Kata ya Somangila, Wilaya ya Kigamboni, Jiji la Dar es Salaam, nyumbani kwake Khamis Said Luwongo (38), Makonde, mfanyabiashara, mkazi wa Gezaulole anaeleza alimpiga na kumuua mke wake aitwaye Naomi Orest Marijani (36), Mpare, mfanyabiashara na mkazi wa Gezaulole.
“Mara baada ya mauaji hayo Khamis Said Luwongo anaeleza kwamba alichukua mwili wa mke wake na kuuweka kwenye shimo alilochimba kwenye banda lake la kufugia kuku, kisha aliweka mkaa gunia mbili na mafuta ya taa kisha akawasha moto uliowaka muda mrefu na mwili wote kuteketea kuwa majivu.
“Kisha alichukua majivu hayo akaweka kwenye mfuko na kubeba kwa kutumia gari lake lenye namba T 206 CEJ aina ya Subaru Forester, rangi nyeusi na kupeleka kwenye shamba lake lililoko Kijiji cha Marogoro, Kata ya Vikindu, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.
“Alichimba shimo kwenye shamba lake kisha kuweka hayo majivu na kufukia na akapanda mgomba juu yake. Kisha Khamis Said Luwongo alikaa nyumbani kwake akisema mke wake ametoroka nyumbani, tarehe 19.05.2019 alifungua taarifa ya mke wake kutoroka nyumbani na kupewa RB ya Kituo Kidogo cha Polisi, Mjimwema, MJ/RB/234/2019 yahusika. Kisha kuwajulisha ndugu, jamaa na marafiki zake kuwa mke wake ametoroka nyumbani.
“Tarehe 12.06.2019 alifungua jalada KGD/IR/3617/2019 kosa kutelekeza mtoto. Akimtuhumu mke wake kuwa ametelekeza mtoto aitwaye Gradous (sahihi Grecios) Khamis mwenye umri wa miaka sita. Tarehe 13.06.2019 ndugu wa Naomi Orest Marijani walitoa malalamiko yao ya kupotea kwa ndugu yao kukafunguliwa jalada la uchuguzi Temeke/CID/PE/69/2019 yahusika.
“Upelelezi uliendelea Khamis Said Luwongo akiwa anakwenda kuripoti Ofisi ya RCO Temeke hadi tarehe 15.07.2019 Khamis Said Luwongo alizuiliwa na mahojiano ya kina kufanyika ndipo akaamua kusema ukweli kuwa alimuua mke wake, tarehe 16.07.2019 aliongoza timu ya makachero kutoka Kanda Ofisi ya ZCO, Ofisi ya RCO Temeke, wataalamu kutoka PHD na daktari, iliyokuwa inaongozwa na ASP Msisiri OCS Kigamboni.
“Walifanikiwa kupata mabaki ya mwili yamechukuliwa kwenda Kanda kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Chanzo cha mauaji ni wivu wa kimapenzi, tukio limekaguliwa na SP Thobias Walelo, OC CID Kigamboni akishirikiana na makachero. Upelelezi unaendelea, nitaendelea kukujulisha maendeleo.”
Mkuu wa Wilaya atia neno
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, katika mazungumzo na JAMHURI mwishoni mwa wiki amesema vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wa kina wa tukio hilo na kwamba vyombo hivyo viendelee kupewa ushirikiano kutoka pande zote, wakiwamo wananchi.
“Uchunguzi unaendelea. Lakini uchunguzi wa awali unaonyesha wanandoa hao walikuwa na mgogoro wa miaka zaidi ya miwili, kwamba kila mmoja alikuwa akilala chumba chake. Mtuhumiwa amekiri kumuua mkewe, akamchoma na kuzika majivu.
“Hili ni funzo kubwa kwa jamii yetu, kwamba suala la usalama linaanzia ngazi ya familia. Kama mgogoro huu ungetafutiwa ufumbuzi bila shaka mambo yangekuwa tofauti, jamii ilichelewa kuchukua tahadhari kutokana na mgogoro huo.
“Lakini kuna mambo matatu muhimu hapa. Kwanza, sote tutambue suala la ulinzi na usalama linaanzia ngazi ya familia. Familia ni lazima ziwe na upendo, umoja na ushirikiano. Pale kwenye migogoro kama ya ndoa, wanafamilia watafute ufumbuzi na hata majirani wa hizo familia.
“Pili, kumekuwa na masuala ya kisiasa kwamba mtu akitoweka basi wanasema ametekwa na genge la watu ndani ya serikali. Hizi ni siasa, na katika tukio hili kuna jambo la kujifunza. Tatu, mara nyingi anapotoweka mwanamke, watu wanauliza ana umri gani, kama ni miaka 19 utasikia huyo ametoroka amekwenda kwa mwanaume.
“Hili ni tukio la kusikitisha sana, serikali inalipa uzito mkubwa na uchunguzi unaendelea, lakini nasisitiza, jamii isiwe na majibu mapesi katika masuala ya namna hii.
“Tunawashukuru sana wanandugu wa Naomi, wametoa ushirikiano mkubwa sana. Kwa kweli wamepambana mno, pale walipokwenda ngazi fulani ya vyombo vya dola wakaona kuna walakini, haraka sana waliweza kwenda ngazi nyingine.”
Polisi Kigamboni
Gazeti la JAMHURI katika uchunguzi wake lilibaini kuwa familia ya Naomi katika kuhangaika kumtafuta ndugu yao, ilikabiliana na changamoto kadhaa ikiwamo kupata shida hata kufungua jalada la uchunguzi wa tukio hilo Kituo cha Polisi Kigamboni, kwamba familia hiyo ilijaribu bila mafanikio kumuomba Mkuu wa Kituo cha Polisi-Kigamboni awasaidie kufungua jalada la uchunguzi bila mafanikio.
Baada ya familia hiyo kupata usumbufu katika Kituo cha Polisi Kigamboni kiasi cha kuwalazimu kuripoti usumbufu huo kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camilius Wambura Juni 12, 2019, siku 33 tangu Naomi atoweke, na Wambura akatoa maelekezo kwa RCO – Chang’ombe (Mkoa wa Temeke) kufungua jalada la uchunguzi. Siku iliyofuata, kazi ya kwenda kufanya upekuzi nyumbani kwa Meshack ilifanyika lakini Naomi hakupatikana.
Awali Polisi wa Wilaya ya Kigamboni walionekana kupuuza tukio hilo kwa kuwaambia ndugu kuwa, kupotea kwa mtu si kosa la jinai (halihitaji jalada la uchunguzi). JAMHURI limemtafuta Mkuu wa Kituo hicho, OC – CID, ASP Thobias Walelo, ambaye ameliambia gazeti hili kuwa kwa sasa suala hilo limefika ngazi za juu, kwa hiyo hawezi kulizungumzia kwa undani.
ASP Walelo ameulizwa kwa nini Polisi Kigamboni walipuuza tukio hilo kiasi cha kutoipa ushirikiano uliotarajiwa familia ya marehemu Naomi, na pili, kama kulikuwapo mawasiliano yoyote baada ya tukio hilo kati ya ASP Walelo na mume wa marehemu Naomi, Meshack, ambaye kwa sasa amekiri kumuua mkewe.
ASP Walelo alikiri kuwapo kwa taarifa za ndugu hao kufika kituoni hapo, lakini hakutaka kukiri iwapo awali alilipuuza tukio hilo. “Hili suala kwa sasa lipo ngazi za juu na uchunguzi unaendelea. Siwezi kulizungumzia kwa wakati huu,” amesema na kudai kuwa mengine yanayoambatanishwa na tukio hilo kuhusu Kituo cha Polisi Kigamboni ni ‘tetesi’ tu.
Polisi Temeke
JAMHURI limemtafuta Kamanda wa Polisi Temeke (RPC), Amon Kakwale, kuzungumzia kifo cha Naomi na taarifa ya ‘kupuuzwa’ kwa ndugu wa Naomi katika Kituo cha Polisi Kigamboni kwa madai kuwa “kupotea mtu si kosa la jinai”.
RPC Kakwale, amesema: “Kujibu swali lako la kwanza, jalada la uchunguzi linaweza kufunguliwa kituo chochote cha polisi. Lakini pia kwa mujibu wa taratibu za kipolisi, jalada la uchunguzi lililofunguliwa kituo fulani vilevile linaweza kuhamishiwa kituo kingine kikubwa zaidi pale inapotokea mahitaji ya kufanya hivyo.
“Kuhusu hili suala la pili la uchunguzi umefikia wapi, kwa sasa tunasubiri matokeo ya uchunguzi huo wa sampuli kutoka taasisi nyingine nje ya polisi,” amesema RPC Kakwale.
Alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa taarifa za ucheleweshaji wa uchukuaji wa sampuli kutoka kwa ndugu wa Naomi kwenda kuzilinganisha na mabaki ya mwili yaliyopatikana, amehoji: “Wewe unawajua ndugu wote wa Naomi? Ninachojua sampuli zimekwisha kuchuliwa miongoni mwa ndugu zake.”
JAMHURI lafika kwa ‘muuaji’
Julai 19, 2019 JAMHURI limefika nyumbani kwa Meshack na Naomi Gezaulole – Kigamboni. Cha kushangaza, pamoja na nyumba yalikofanyika mauaji kuwa imezungushiwa utepe wa polisi kuashiria kuwa ushahidi ama mazingira yaliyopo hayapaswi ‘kuchezewa’ kwani bado uchunguzi unaendelea, timu ya JAMHURI imekuta mafundi watatu wanafanya ukarabati wa mabwawa mawili ya samaki.
Mabwawa hayo awali yalifukuliwa kuchunguza kutafuta mwili wa Naomi. “Ni kwa nini mnaendelea na ukarabati wa mabwawa wakati nyumba hii iko chini ya uangalizi wa Polisi na uchunguzi wa tukio lililofanyika kwenye nyumba hii unaendelea?” JAMHURI liliwaulizwa mafundi hao.
Mafundi hao walijibu kuwa Polisi walipokuja kukagua mara ya mwisho waliwaruhusu kuendelea na ukarabati huo kuwarejesha samaki (waliohifadhiwa kwa muda kwenye pipa dogo la plastiki –drum) warejeshwe kwenye mabwawa hayo ili wasife.
JAMHURI limemuuliza RPC Kakwele kuhusu jambo hilo. “Kuhusu hilo… tuchukulie kuwa wewe ndiye umenipa taarifa, tutalifuatilia,” amejibu kwa ufupi RPC Kakwale.
Mtoto yuko wapi?
Kumekuwa na maswali mengi kuhusu hatima ya mtoto wa wawili hao, wengine wakitaka kujua anaishi wapi? Masuala ya shule yatakuwaje baada ya tatizo lililomkuta baba yake huku mama yake akiwa ameuawa?
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba mtoto wa Naomi na Meshack amekabidhiwa kwa upande wa ndugu wa Naomi baada ya awali kuwapo chini ya uangalizi wa shangazi wa Meshack.
“Kwa sasa Gracious yuko upande wa ndugu wa Naomi, tunaendelea kufanya mipango ya kumtafutia shule nyingine ili aweze kuendelea na masomo.
“Kabla ya kushikiliwa kwa Meshack na kukiri kwake kuwa amemuua Naomi, Gracious alikuwa kwa ndugu wa Meshack, lakini baada ya haya ya sasa familia ya Naomi imemchukua mtoto.
“Tunaendelea na taratibu za kumtafutia shule mtoto, hawezi tena kuendelea kusoma katika shule aliyokuwa anasoma awali,” anasema mmoja wa wanafamilia ya Naomi.
Anasema Gracious yuko salama zaidi upande wa familia ya Naomi kutokana na ukweli kwamba hakuna ugomvi wa pande mbili za kifamilia isipokuwa ni makosa yaliyofanywa na Meshack.
JAMHURI lilivyoripoti
Katika toleo lake namba 407, JAMHURI liliandika habari kuhusu Naomi, ikiwa na kichwa cha habari kilichohoji: Ameuawa? Katika habari hiyo, JAMHURI lilieleza kuwa, Jumamosi ya Mei 18, 2019 mume wa Naomi kwa jina la Khamis Said Luwongo, au Meshack, alikwenda nyumbani kwa mzee Robert Mchome anayeishi Mabibo (Dar es Salaam) kutoa taarifa kuwa, Jumatano ya Mei 15, 2019 saa 1:30 jioni akidai alipokea ‘meseji’ kutoka kwa mkewe kupitia namba 0655 527 203 (namba aliyokuwa akiitumia mke wake) ikisema: “naondoka na mtoto namwacha nyumbani peke yake na kesho nasafiri nje ya Tanzania.” Dakika kumi baadaye, saa 1:41 akadai kupokea ‘meseji’ ya pili ikisema “Na hutonipata kwa namba hii tena hudumia mtoto vizuri” kwenda kwenye namba zake za 0685043374 na 0714812530.
Akaongeza tena kuwa, alirudi nyumbani usiku saa tatu na kukuta mtoto akiwa peke yake, akaenda kumnunulia chakula akala, siku iliyofuata akamuandaa mwenyewe mtoto na kwenda shuleni.
Hapo, JAMHURI liliainisha utata uliopo, kwamba mkewe kadai kamtaarifu ameondoka na kamwacha mtoto Mei 15, 2019 na akamkuta mtoto yuko peke yake. Kwa nini hakupiga simu kokote kuulizia kuhusu mkewe siku hiyo ya Jumatano, na siku mbili zilizofuata, Alhamisi na Ijumaa hadi Jumamosi asubuhi ndipo alipofunga safari kwenda Mabibo kutoa taarifa? Je, ni kitu gani kilikuwa kinaendelea ndani ya hizi siku tatu; Jumatano, Alhamisi na Ijumaa?
Katika habari hiyo, gazeti hili lilieleza kuhusu mwajiriwa wa Naomi, anayejulikana kwa jina la Anna aliyekuwa akiuza katika duka la dawa la Naomi, kwamba, familia baada ya taarifa za ndugu yao kutoweka (kama zilivyofikishwa kwa mzee Mchome) ilikwenda Kigamboni kutafuta ukweli, kati ya waliozungumza nao ni huyo Anna ambaye alipoulizwa ni lini mara ya mwisho alimuona Naomi alijibu kuwa; Jumanne ya Mei 14, 2019 kwamba walishinda wote dukani na aliondoka saa mbili usiku, ilipofika saa 3:30 usiku alifunga duka na kumpelekea mauzo ya siku hiyo, na alimkuta nyumbani, akamkabidhi.
Lakini Mei 15, 2019 saa 1:44 hadi 1:50 asubuhi, inaonekana Naomi ‘alichati’ na na dada wa Tigo Pesa (mfanyabiashara) kuwa amtumie Sh 75,000; familia ilipomhoji alidai kuwa muda walipokuwa ‘wakichati’ hakuwepo dukani, hivyo akamuahidi (Naomi) kumtumia kiasi hicho cha fedha baadaye kidogo, na saa 4:13 asubuhi alimtumia Sh 75,000.
Anna anadai kuwa saa mbili usiku alifuatwa na dada wa Tigo Pesa ambaye alimwambia asubuhi ‘alimrushia’ Naomi Sh 75,000 kwa makubaliano kuwa atarudishiwa hiyo pesa na Anna jioni ya siku hiyo (Mei 15, 2019), na ili kujiridhisha Anna alimpigia Naomi kwenye namba yake ya 0655527203 na simu iliita lakini haikupokelewa, akaitumia meseji – haikujibiwa, alipojaribu kuipiga tena kwa mara nyingine haikupatikana. Anna alipoulizwa kama aliilipa hiyo pesa ama la, alijibu kuwa, kwa kuwa si mara ya kwanza (Naomi) kuomba kurushiwa pesa na dada wa Tigo Pesa, alikubali na kuilipa pesa hiyo.
Uchunguzi wa JAMHURI kwa kushirikiana na familia, na wataalamu wa mitandao ulibaini kuwa, simu ya Naomi ya 0655527203 ilitumika kumpigia Meshack (mume wake) na kumtumia ‘meseji’ saa 7:37 mchana kwenye namba 0677009128 ambayo kwa mujibu wa Meshack, Naomi haijui hiyo namba. Hapa, swali linajengeka: “Aliijuaje mpaka akaipigia?”
Uchunguzi zaidi ukabaini kiasi hicho cha pesa (Sh 75,000) hakikuwa kimetolewa kwenye simu ya Naomi muda wote, hadi Julai 10, 2019. Swali likaibuka: “Kwa nini (pesa) haijatolewa kama mtumiaji wa hiyo simu muda wa mchana bado alikuwa ni Naomi?
Lakini Meshack alipoulizwa kuhusu ‘line’ yenye namba 0677009128 ni ya nani? Alijibu kuwa ni ya kwake isipokuwa hakuisajili na alikuwa akiitumia kuwapigia watu ambao hataki waijue namba yake halisi, na alipoulizwa hiyo ‘line’ iko wapi? Alijibu; ameiharibu. Swali jingine likaibuka: “Kwa nini anasema baada ya haya matatizo kutokea alihisi itamletea matatizo kutumia ‘line’ ambayo haijasajiliwa?”
Mei15, 2019 siku ambayo Naomi alitoweka, simu yake haikupokea simu yoyote bali simu yake ilipiga simu moja tu saa 7:26 mchana kwenda namba ya mume wake (Meshack) na iliongea sekunde 15 tu.
Lakini simu ya Naomi ilizimwa siku aliyotoweka, kwamba simcard ya Naomi ambayo kuanzia Januari 13, 2019 ilianza kusoma kwenye simu yenye IMEI Na. 357544080102102/357544080102094, ‘line’ hiyo imekuja kutolewa siku Naomi alipotoweka, Mei 15, 2019 saa 7:18 mchana na kuingizwa kwenye simu ndogo (kitochi) aina ya ITEL IT5600 yenye IMEI 354289073319500.
Mei 15, 2019 saa 1318 mchana, siku Naomi aliyotoweka, simcard yake yenye namba 0655527203 ilitolewa kwenye ‘handset’ yake aina ya ICE- C 3G FREETEL yenye IMEI Na. 357544080102090 na kuingizwa kwenye simu ndogo ya kitochi aina ya ITEL IT5600 yenye IMEI: 354289073319510, simu ambayo askari walipokwenda kumpekua Meshack, Julai 3, 2019 walimkuta nayo. Na muda huo huo simcard iliyokuwemo kwenye simu hiyo hiyo kwa takriban siku 86 nyuma yenye namba 0677009128 ilihamishiwa kwenye simu nyingine aina ya ITEL IT2130 yenye IMEI 355209084172530 ikakaa siku moja tu (tarehe 15/5/2019) kabla ya kurejeshwa kwenye ITEL IT5600 yenye IMEI: 354289073319510 Ijumaa ya Mei 17, 2019 ambako ilikaa kwa siku tatu hadi Mei 19, 2019 na kutolewa.
Askari walipokwenda kumpekua Meshack Julai 3, 2019 simu zote mbili za ITEL IT2130 yenye IMEI 355209084172530 na ITEL IT5600 yenye IMEI 354289073319510 walimkuta nazo Meshack.
Na kuhusu ‘line’ ya namba 0677009128 iliyokuwemo, JAMHURI liliandika katika habari yake hiyo kwamba,alipoulizwa Meshack iko wapi, alijibu: “Nimeiharibu.” Kwa nini? “…kwa kuwa nimegundua itaniletea matatizo kwa vile nimekuwa nikiitumia bila kuisajili.”
Lakini dakika mbili baada ya ‘line’ ya Naomi yenye namba 0655527203 kuhamishiwa kwenye ITEL IT5600, iliipigia simu ‘line’ ya Meshack yenye namba 0677009128.
Mei 16, 2019 saa 12:49 jioni, siku moja baada ya Naomi kutoweka, simcard yake yenye namba 0679463985 aliyoisajili tangu Novemba 3, 2017 iliingizwa kwenye ‘handset; inayomilikiwa na Meshack aina ya ITEL IT5600 yenye IMEI 3542890733195009. Mei 17, 2019 simcard hiyo ilituma ‘meseji’ kwenda namba za Meshack 0679463985 (saa 12:24 asubuhi) na 0679463985 (saa 12:26 asubuhi) mtawalia, huku mtumaji na mtumiwaji wote wakiwa sehemu moja (same location).
Gazeti hili, moja kwa moja lilibainisha kuwa mtuhumiwa wa kwanza kuhusu kutoweka kwa Naomi ni Meshack, kwa sababu kadhaa, ambazo ni pamoja na kwanza, mara tu baada ya simu aliyokuwa akiitumia Naomi kuzimwa siku ya Mei 15, 2019 saa 7:18 mchana, ‘line’ ya Naomi ilitolewa na kutumika kwenye simu ya Meshack ITEL IT5600 yenye IMEI 3542890733195009.
Pili, muda mfupi baadaye, saa 7:20 simu (handset) ya ITEL IT5600 iliyokuwa ina line ya Meshack yenye namba 0677009128 ilitolewa na badala yake ikaingizwa ‘line; ya Naomi yenye namba 0655527203; na ‘line’ yenye namba 0677009128 ikaingizwa kwenye simu nyingine ya ITEL IT2130 yenye IMEI Na. 355209084172530. Tatu, dakika sita baadaye (saa 7:26) ‘line’ ya Naomi yenye namba 0655527203 iliipigia simu ya Meshack kwenye namba yake ambayo hajaisajili ya 0677009128 (ambayo Naomi alikuwa haijui na kwa hiyo asingeweza kuipigia na hata kama angeijua Naomi angeipigia simu kutokea kwenye handset yake ya FREETEL yenye IMEI Na. 357544080102090, hapa, ilielezwa na gazeti hili kwenye habari yake ya wiki iliyopita kwamba, inawezekana alishindwa kuitumia kwa kuwa hakuwa na nywila (password) yake hivyo kumlazimu kuihamishia kwenye simu ya kitochi.
Nne, kwenye mahojiano (Meshack) alikwishakiri kuwa namba ya 0677009128 alikuwa akiitumia kwa siri hivyo Naomi alikuwa haijui, na kwwa hiyo, Naomi asingeweza kuipigia muda ule wa mchana siku alipotoweka kutokea kwenye ‘handset’ ya ITEL IT5600.
Tano, muda wa saa 7:37 mchana, ‘line’ ya Naomi yenye namba 0655527203 ilituma meseji kwenye ‘line’ ya mume wake (Meshack) kwenye namba yake ambayo hajaisajili ya 0677009128; aidha mtumaji na mtumiwaji wote walikuwa sehemu moja.
Sita, kati ya saa 1:29 na saa 1:42 usiku alijitumia jumla ya meseji nane kwenye namba zake za 0685043374 na 0714812530, pia mtumaji na mtumiwaji wote wakiwa sehemu moja.Saba, saa mbili usiku, Anna wa duka la dawa alimpigia simu Naomi kwenye namba yake 0655527203 iliita bila kupokelewa, yumkini haikupokelewa kwa vile ilikuwa mikononi mwa Meshack.
Nane, Meshack alipoulizwa ana simu ngapi anazomiliki alijibu ni zaidi ya tano zikiwemo simu aina ya ITEL IT2130 na ITEL IT5600 alizokutwa nazo siku Polisi walipokwenda kumpekua, simu ambazo ushahidi unaonesha zilitumika kuingizwa ‘line’ aliyokiri kuimiliki bila usajili yenye namba 0677009128 na kuitoa kwenye mojawapo ya simu hizo Mei 19, 2019 na kisha kuiharibu, ushahidi huu pekee, JAMHURI likabainisha kuwa unatosha kumtia matatani kama mtuhumiwa wa kwanza katika kutoweka kwa mkewe ili ajibu ‘line’ za Naomi za 0655527203 na 0679463985 zilizotumika kwenye simu hizo baada ya kutoweka kwa Naomi ziko wapi.
Tisa, JAMHURI liliandika katika toleo lake hilo lililopita, namba 407, kwamba Meshack anapaswa ajibu Naomi yuko wapi kwani simcard ya Naomi yenye namba 0679463985 ilipita kwenye handset zake wakati Naomi amekwishatoweka. Hapa, swali kuu, kwa nini mtumaji wa meseji na mtumiwaji walikuwa wote sehemu moja? Uchunguzi wa JAMHURI ulijiridhisha kuwapo kwa uwezekano wa Meshack ndiye aliyekuwa anajitumia hizo meseji.
Kumi, ilimchukua Meshack siku nne tangu tukio la kupotea Naomi hadi kwenda nyumbani kwa walezi wa Naomi kutoa taarifa, je, hizo siku tatu zilipitaje kwake pasipokumuuliza mtu yeyote alipo Naomi? Hakuwahi kumpigia mtu yeyote, si kaka, dada wala mlezi wa Naomi kuulizia.
Mambo mengine yaliyofichuliwa na JAMHURI wiki iliyopita ni pamoja na kuhusu kijana aliyekuwa anampeleka na kumrudisha shuleni mtoto wa Meshack na Naomi, Grecious, mwenye umri wa miaka sita, kutokuhojiwa hadi siku tunachapisha gazeti, toleo lililopita.
JAMHURI iliandika: “Huyu kijana ambaye humpeleka mtoto shuleni apatikane ili atoe maelezo asubuhi (Mei 15, 2019) akimpeleka mtoto shuleni alikuta hali gani? Ni Naomi au ni Meshack alimkabidhi mtoto? Je, huyo mtoto akirejea kutoka shuleni alimkabidhi kwa baba yake au mama yake? Kama siku ya Jumatano (alipotoweka Naomi), Alhamisi na Ijumaa mtoto aliandaliwa na baba yake, kwa nini Meshack hakumtafuta mke wake popote wala kumuulizia mtu yeyote alipo mke wake?
JAMHURI wiki hiyo lilimtafuta Meshack na kumuuliza kuhusu kadhia hiyo ya kupotea kwa mkewe katika mazingira yenye utata, naye alijibu kwamba, suala hilo linaendelea kuchunguzwa, hakutana kutoa majibu ya kina, akisema angefanya hivyo wakati muafaka.
Gazeti hili kwa ujumla, pamoja na mambo mengine, lilihoji kwa nini Meshack ambaye ni mtuhumiwa wa kwanza kwa mujibu wa uchunguzi wa JAMHURI, aachwe akibaki huru mitaani? Na hatimaye wiki hiyo iliyopita, Meashack alikamatwa na kuhojiwa, na akakiri kumuua mkewe kwa kumchoma moto, na kuzika majivu sambamba na mabaki mengine aliyoyatumia kuteketeza mwili wa mkewe huyo.