Wiki iliyopita katika sehemu ya 6 hadithi hii iliishia katika aya inayosema: “Sina kitu nitakachopoteza lile dubwasha likinishinda mama yangu. Sana sana nitapoteza roho yangu tu. Sasa roho yangu ikipotea kutakuwa na hasara gani? Je, ni nani ajuaye kwa dhati roho huenda wapi baada ya kifo? “Aliyeiweka roho ndani yangu atajua pa kuipeleka.” Kijana wangu huyu alikuwa anasema kila mara. Endelea…
“Babu Bugulugulu”, yule bibi aliendelea: “Mawazo haya ya Masalakulangwa yalinifikirisha sana. Baadaye nikaanza kuona ukweli wa maneno yake kuwa ukidhulumiwa ni heri kupambana ili kurudisha hadhi ya utu wako. Maskini huwa hana cha kupoteza. Ni roho tu ndiyo hupotea.
“Kwenye masimulizi ya watu wa kale Samson alidhulumiwa na yule Delila na uwezo wake wa nguvu ukaisha. Jamaa walimshika njemba huyu, wakamtoboa macho baada ya kukata nywele zake. Lakini baadaye nywele zilipoota, nguvu zake zikamrudia.
“Samson tunaambiwa alikuwa amefungiwa kwenye nguzo za uwanja wa michezo kwa vile nguvu zake zilikuwa zimemrudia. Alizisukuma zile nguzo za uwanja na jengo lote likaporomoka na kuwateketeza watazamaji wote pamoja na Samson mwenyewe. Baada ya kuona kuwa wamemfanya kuwa kipofu na hawezi kuwa na raha kama Mungu alivyomkusudia.”
Ujasiri huu wa kujiua na kuwaua wengine wote wanaotetea wahalifu alizoea kuuita “Samsonism”. Au siku zingine alitumia neno jingine eti kujitoa mhanga. Unakufa lakini unakwenda na wengine kuliko kubaki na maisha ya kunyanyaswa na kudhulumiwa.
“Nilimweleza hatari ya kupambana na yule mnyama lakini wapi Bwana; maonyo yangu hayakufua dafu. Baadaye, kwa shingo upande ilibidi nimkubalie matakwa yake. Kwani nilifikiria kwa uhakika ni nani anayejua baada ya kifo hufuata nini? ‘Wakuda hudai eti kuna moto wa Jehanamu. Je, Waeskimo wa Greenland wanasemaje?’
“Wengine hivi na wengine vile. Nikampa ruhusa mwanangu. Nikamtayarishia zana za kupigania. Nikamzindika ili mwanangu huyu wa pekee asije akadhurika. Nilitumia siku arobaini kuomba na kukamilisha pambano na lile dubwasha. Muda ulipofika nikamuaga Masalakulangwa wangu ili aende kupambana na nguvu za giza. Akaenda.
“Alikaa porini muda wa siku arobaini bila ya kuona kitu chochote cha kutisha. Dhamira na hasira za kijana huyu dhidi ya uonevu nje ya nguvu za binadamu ulizidi kumsukuma aendelee na nia yake ya kupambana na nguvu hizo za giza. Kijana alilisaka lile dude huku na huko.
“Hata hivyo, fursa ya kuliona haikutokea. Baadaye Masalakulangwa aliendelea kutafuta. Siku moja likamjia wazo la kupanda mti mrefu na kisha apige kelele na aone kutatokea nini. Basi alitafuta mti mrefu kupita yote na akakwea hadi juu kabisa. Akaanza kuita kwa nguvu ajabu: ‘Ewe mla watu. Kama kweli u jasiri jitokeze hadharani upambane nami.’” Aliita hivyo mara tatu kisha akanyamaza asikilizie matokeo ya kuita kwake.
“Muda mfupi ikasikika sauti kwa mbali ikisema: ‘Ewe kijana ukitaka kupambana nami tengeneza chanja saba za kupigania. Mimi pia nitatengeneza idadi hiyo hiyo. Wakati wa kupigana ni lazima kupanda juu ya uchanja. Ukiharibika, unahamia mwingine. Ooooow!’ Sauti ya dude hili ilikuwa kali na ya kuogofya sana. Miti yote pale porini ikawa inatetemeka ungedhania imekumbwa na tufani au tetemeko la ardhi.
“Masalakulangwa alirudi nyumbani siku hiyo na aliponieleza, basi tukawa katika harakati za maandalizi ya vita. Siku hazifiki, zikafika. Muda ulipofika, akaenda kwenye uchanja wa kwanza. Nduli alilenga shabaha yake akaachia, ‘chwaaaa’ Masalakulangwa akaona uchanja wake unawaka moto na sawia ukaanza kuporomoka, akarukia uchanja wa pili. Zamu hii ikawa yake kulilenga lile limnyama.
“Akalenga shabaha na akaachia. Silaha ilipotua, uchanja wa adui nao pia ukawaka moto. Lile dude likarukia uchanja mwingine. Pambano liliendelea hivyo mpaka wakaenda kwenye chanja za mwisho na wakawa wamebakiza silaha yeye moja na lenyewe moja. Silaha yake ya mwisho lile dude ilikuja vibaya, nusura imdungue Masalakulangwa ila bahati ikawa upande wake.
“Silaha hiyo iliishia kuunguza uchanja na ndipo akarukia kwenye uchanja wa mwisho. Akalenga silaha yake ya mwisho. Akawakumbuka na wahenga wake. Akawataja kwa majina. Akasali. Kisha akaachia. Silaha ile ilibarikiwa na mababu. Ikampiga yule nduli kwenye jicho la kulia. Akaanza kulala kwa maumivu! Akaanguka! Akagaagaa! Akalia! Baadaye akamwomba Masalakulangwa aende karibu yake ili amweleze cha kufanya.
“Bugulugulu sijui Masalakulangwa alipata wapi ujasiri wa kulisogelea lile dude. Alilisogelea mpaka karibu kabisa likamwambia achukue kisu chake kisha alitumbue tumbo lake na kuwa chochote kitakachotokea basi hiyo ndiyo halali yake. Alichomoa kisu kutoka alani pake na kukitumbukiza kwenye tumbo la lile limnyama.
“Maelezo yangu yanaonekana kama hadithi za Abunwasi, lakini haya ni mambo ya ukweli kabisa. Mimi ni mtu mzima siwezi kukudanganya wewe kijana mdogo. Ninayokueleza ni ukweli mtupu, wala usisite kuyaamini.
“Kilichotoka tumboni mwa lile limnyama ni watu wote! Watu wote ambao lile dubwasha liliwameza. Walitoka! Wanyama wa aina mbalimbali pia nao walitoka tumboni humo! Ni ajabu! Watu mbalimbali walipotoka tumboni mwa yule mnyama walikimbia na hawakutaka kukaa karibu kwa tahadhari ya kuwa asije akatokea tena mnyama au kioja kingine na kuleta kiama.”
Bugulugulu rafiki yangu mpendwa. Ninajaribu kuandika mambo yote ya muhimu aliyonihadithia yule Mama Masalakulangwa. Huwa nakumbuka jambo jingine la muhimu sana miongoni mwa watu wa leo ambalo ni lugha na rangi tofauti za watu.
Mama huyu alidai eti hapo awali watu wote walikuwa wanatumia lugha moja iliyokuwa imetawaliwa na ishara mbalimbali. Kwa hiyo watu waliwasiliana kwa ishara na maneno machache sana yaliyokuwepo. Akatabasamu kidogo.
Mama Masalakulangwa alinichekesha pale aliponiuliza: “Kwa mfano huko kwenu mtu akitaka kukataa kwa ishara hufanya nini?” akanikazia macho na kungojea jibu la swali lake. Nilitoa ishara kwa kutingisha kichwa huku na huko. Kisha tena nikanyanyua mabega na kuyashusha sawia.
“Ishara hizi” Mama Masalakulangwa aliendelea: “Zinatumika miongoni mwa jamii zote duniani. Walijifunza kabla ya kumezwa na lile dubwasha.” Mama huyu akanikazia macho aone kama ninamfuatilia. Akacheka kidogo kisha akaendelea: “Je, wanapotaka kukubali huwa wanatoa ishara gani?” Akaniuliza tena huku ameniangalia kwa makini.
Nikainua kichwa juu na kisha nikakishusha haraka haraka. Yule mama alitabasamu na kuonyesha kuwa anakubaliana nami. “Je, kama mtu anaomba kitu huonyesha kitu gani?” Akauliza tena ungedhani tumo darasani.
Nikanyoosha kiganja changu kama vile ninaomba kitu kwa kutandaza na kunyoosha vidole vya mkono wangu. Vilevile nikajitahidi kwa kutumia nyusi na uso kuonyesha kuomba huruma au kupewa hisani. Baada ya ishara hizo nilitabasamu kidogo na “otomatikale” nikajikuta ninacheka.
“Basi babu Bugulugulu”, aliendelea kufafanua kwa kujiamini sana: “Hapo awali watu wote waliishi sehemu moja na lugha yao ilitawaliwa zaidi na ishara. Ilikuwa lugha duni sana ukiilinganisha na maendeleo yaliyotokea hapo baadaye kwa kila jamii ya watu. Au unadhani kuna jamii moja ya watu ambayo imezifundisha jamii zingine kwa kutingisha kichwa au kukataa kwa kunyanyua mabega na kushusha?
“Je, kutabasamu walijifunza wapi? Au unadhani kuna jamii fulani ilitoka huko ilikotoka na kuwafundisha ishara hizi? Jamii zote walijifunza ishara hizo kabla ya lile gharika la zimwi na walipokimbia wakatoka na ishara hizo ambazo zinaendelea hadi leo miongoni mwa jamii zote duniani. Akaniangalia tena kisha akaendelea:
Je, unafahamu nini kiliendelea baada ya kumwangalia? Usikose sehemu ya nane yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa Na. 0755629650.