Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na kumiliki bandari nchini, pia inamiliki Chuo cha Bandari (Bandari College) kilichopo katika Wilaya ya Temeke. Chuo hiki ndicho chemchemi au hazina ya kutoa utaalamu au maarifa ya kuwa na uwezo au umahiri wa kuhudumia meli na mizigo, usimamizi wake na utoaji wa huduma zinazohusiana na shughuli za bandari.
Historia ya chuo hiki inaanzia tangu wakati wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ilivunjika mwaka 1977. Jumuiya hiyo iliyoundwa na nchi za Tanzania, Uganda na Kenya ilianzisha chuo ambacho awali kiliitwa Chuo cha Mafunzo (Training School).
Shule hiyo ya mafunzo ilikuwa katika Barabara ya Sokoine. Shule hiyo ilihusika katika kutoa mafunzo ya Ukarani na Uendeshaji wa vyombo au mitambo kwa ajili ya shughuli za bandari.
Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzisha shirika la umma lililoitwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (Tanzania Harbours Authority – THA) mwaka 1977. THA ilikuwa na kazi ya kusimamia na kuendesha bandari za mwambao wa bahari ambazo ni Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Bagamoyo, Mafia, Pangani, Lindi na Kilwa.
Ili uendeshaji wa bandari usikwame au kusimama, THA iliamua kuijengea uwezo shule hiyo ya mafunzo ambapo mwaka 1980 shule hiyo ilihamishiwa eneo la Tandika katika Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam na kubadilishwa jina kuwa Chuo cha Bandari (Bandari College).
Chuo hiki cha Bandari kilianzishwa kikiwa ni chuo mahususi kinachofundisha masomo ya uendeshaji wa bandari, shughuli za huduma za meli na mizigo pamoja na usimamizi wake.
Kwa sasa chuo hiki kinatoa mafunzo katika ngazi za Astashahada (Certificate) na Stashahada (Diploma). Chuo kimesajiliwa na kupata ithibati kamili na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (National Council for Technical Education – NACTE).
Chuo kina miundombinu muhimu na ya kisasa kwa ajili ya kufundishia, ikiwa ni pamoja na madarasa ya kutosha, maktaba, karakana kwa ajili ya kufundishia kwa vitendo, miundombinu ya kipekee kwa shughuli za bandari na walimu wa kutosha wenye viwango vinavyotakiwa na kutambuliwa na NACTE.
Aidha, chuo kimepata mafanikio makubwa ambayo ni pamoja na kuongeza idadi ya udahili kwa kufuata viwango na vigezo vya NACTE kutoka wanafunzi 200 mpaka 800 kwa mwaka.
Wafanyakazi wengi wanaofanya kazi ndani ya bandari ni sehemu ya wahitimu wa Chuo cha Bandari na wengine wanafanya kazi kwenye taasisi zinazohusika na shughuli za bandari kama vile kampuni za Uwakala wa Forodha na Meli.
Chuo kimeweza kuimarisha mifumo ya taaluma na taratibu mbalimbali ili kuhakikisha kinatoa elimu bora kulingana na viwango vya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Pamoja na mafanikio ambayo chuo kimeyapata, bado kina changamoto ya kukabiliana na kukua kwa haraka kwa mahitaji ya sekta ya bandari hasa katika teknolojia ya meli na kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, chuo kinafanya utafiti wa mara kwa mara kuhusiana na mahitaji ya sekta ya bandari, hivyo kupitia upya mitaala ili iweze kujibu mahitaji ya wadau wa bandari.
Chuo kimeamua kujikita hasa katika mtindo unaozingatia umahiri zaidi ili mwanafunzi anayehitimu aweze kupata uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na si kukariri masomo kwa ajili ya kufaulu mitihani tu.
Aidha, chuo kinaendelea katika kuboresha miundombinu ya kufundishia kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika sekta ya bandari. Hivi karibuni chuo kimefanikiwa kununua mtambo mkubwa wa kufundishia (Simulator) uendeshaji wa vifaa na mitambo ya kuhudumia mizigo bandarini kwa lengo la kuhakikisha bandari inatoa huduma bora kama lango la biashara kitaifa na kimataifa ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini.
Pia chuo kimeweka utaratibu wa kuwatafutia wanafunzi wake sehemu za kufanyia mazoezi ya vitendo kwa lengo la kuwasaidia kupata uzoefu kulingana na kozi wanazosoma ili wanapokwenda kufanya kazi wawe tayari na umahiri wa kufanya kazi hizo kwa ufanisi.
Ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa tayari kwa ujenzi wa taifa, chuo kimeweka somo la ujasiriamali kwa kila kozi ambayo mwanafunzi anasoma. Hii inamjengea uwezo mwanafunzi wa kujiari badala ya kusubiri kuajiriwa.
Chuo kitaendelea kuboresha mitaala yake ili kutoa elimu bora kwa lengo la kutoa wahitimu walio mahiri katika sekta ya bandari. Kwa yeyote anayetaka kujiunga na Chuo cha Bandari awasiliane na; Mkuu wa Chuo, Chuo cha Bandari, S.L.P 9184, Dar es Salaam au apige simu 0222850970; anuani ya barua pepe: [email protected]; au tembelea tovuti ya chuo; www.bandaricollegedsm.ac.tz