Mbunge wa Kenya, Charles Njagua Kanyi, maarufu pia kama mwanamuziki ‘Jaguar’, ametukumbusha ugumu wa kujenga utangamano wa Wana Afrika Mashariki.

Jaguar ameamsha zogo hivi karibuni baada ya kutishia kuwavamia wafanyabiashara wa nchi kadhaa ikiwamo Tanzania na Uganda wanaofanya kazi Nairobi na ndani ya Jimbo lake la Starehe na kuwatimua warudi makwao.

Tatizo ni kuonekana kwa wafanyabiashara hao kudhibiti baadhi ya biashara na kuathiri uwepo wa wafanyabiashara wa Kenya ambao wameshindwa kuhimili ushindani wa soko.

Aliipa Serikali ya Kenya siku moja kuchukua hatua kuwaondoa nchini Kenya raia hao ama sivyo yeye angeongoza uvamizi wa maduka yao, kuwapiga na kuwatimua nchini.

Serikali yake ilichukua hatua mara moja, siyo dhidi ya raia hao, ila dhidi yake. Imemfikisha mahakamani kujibu mashitaka ya kueneza chuki dhidi ya raia wa nchi nyingine kinyume cha sheria za Kenya na katiba yake.

Zaidi ya kukabiliwa na kuvunja sheria na katiba, matamshi yake, ambayo yameonekana kuungwa mkono na baadhi ya wapiga kura wake yanatishia kubomoa nguzo muhimu kabisa ya ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo Kenya ni mwanachama muhimu.

Tafsiri ya utekelezwaji kamili wa vipengele vya soko la pamoja la nchi wanachama za jumuiya ni kuondoa mipaka au vikwazo vya biashara kwa bidhaa, nguvu kazi na mitaji. Aidha, raia wa nchi wanachama watakuwa na uhuru wa kuishi sehemu yoyote ndani ya jumuiya.

Yapo matatizo ambayo hayajaruhusu hali hiyo kutekelezwa kikamilifu na ndiyo maana yapo makubaliano kuwa kila nchi itaamua wakati muafaka wa kutekeleza vipengele vyote vya matakwa ya soko la pamoja.

Kenya ni moja ya nchi wanachama ambazo zimepunguza kwa kiasi kikubwa vikwazo kwa raia wa nchi wa nchi nyingine kuhamia nchini humo, jambo ambalo Jaguar au hafahamu au ameamua kusahau.

Tanzania bado imeshikilia taratibu ngumu za kuruhusu wageni pamoja na wanaotoka nchi wanachama za jumuiya kufanya kazi au biashara nchini. Lakini hata pamoja na ugumu huu bado tunafahamu kuwa wapo wageni wengi – pamoja na raia wa Kenya ambao wapo nchini kwa ajira na biashara.

Taarifa za biashara na uchumi zinaeleza kuwa kampuni 529 za Kenya zimewekeza nchini Tanzania mtaji wa thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.7. Tukizibadilisha hizo kwa shilingi za Tanzania tunaweza hata kukosa msamiati wa kuzitamka kwa jinsi zilivyo nyingi.

Hii thamani inazidi maradufu thamani ya biashara ndogo ambazo zinamsumbua Jaguar na ambazo zinamilikiwa na Watanzania na Waganda waliopo Nairobi. Labda angetafakari kidogo kabla ya kuongea angepunguza makali ya kauli yake.

Na ni vema kuwa kauli zake hazikuungwa mkono na sehemu kubwa ya wananchi wa Kenya na Tanzania kwa sababu athari zake zingeweza kuwa mbaya na hatarishi, si kwa raia tu, bali kwa uwepo wa ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Hata hivyo kufunguliwa mashtaka ya uchochezi dhidi ya Jaguar hakumalizi tatizo. Kunakumbusha tu changamoto zinazopaswa kumalizwa ili kusafisha njia kuelekea kujengwa kwa ushirikiano imara zaidi wa nchi wanachama na raia wa Afrika Mashariki.

Tuanze kwa kujiuliza: kama mbunge ambaye tunatarajia anao uelewa mpana juu ya mahusiano ya kimataifa ya nchi yake na nchi jirani ana msimamo huu, tunategemea nini kutoka kwa raia wa kawaida?

Lakini kama tukijitwalia uwezo wa kuwa wawazi tunaweza pia kukiri kuwa Jaguar amepaza sauti kufichua tatizo la kweli linalowakabili wapiga kura wake ambao wameshindwa kuhimili uwezo mkubwa wa kibiashara wa Watanzania, Waganda, na Wachina.

Suluhisho la matatizo ya aina hii kwenye mazingira ambapo hakuna nchi inaweza ikajifungia yenyewe na kukataa kushirikiana na nchi nyingine bila kuathiri maendeleo yake ya muda mrefu halipatikani kwa kuwafukuza wageni. Linapatikana kwa kuyakabili matatizo yenyewe na kuhakikisha kuwa hata ndani ya ushirikiano wa nchi na nchi au ndani ya jumuiya, raia wa nchi moja hawafikii uamuzi kuwa ushirikiano ni adhabu au mzigo kwao.

Ushirikiano unapaswa kuzaa matunda si tu kwa zile kampuni zinazovuka mipaka na kuwekeza upande wa pili bali unapaswa kuleta manufaa pia kwa raia wa kawaida ambaye ni rahisi sana kushawishika kuwa adui yake ni jirani yake kutoka Kenya, Tanzania au Uganda.

Jaguar anatukumbusha kuwa uamuzi unaofikiwa kwenye vikao vya marais na viongozi wengine waandamizi ni hatua ndogo sana ya safari ya kufanikisha uimarishwaji wa ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kazi nyingine muhimu ni kuwepo hatua madhubuti za kuelimisha raia juu ya umuhimu wa ushirikiano huo kwa nchi na kwa raia wenyewe ili kuleta maendeleo ya uhakika kwa wote.

Lakini pengine muhimu kuliko hatua zote ni kuhakikisha kuwa safari ile ya utekelezaji wa maazimio inalinda masilahi ya raia wa nchi wanachama ili safari iwe ya kujenga uungwaji mkono badala ya kujenga kada ya raia ambao wanapinga ushirikiano wenyewe.

Haya yakifanikiwa kina Jaguar na viongozi wa aina yake wanapoibua hoja ya kuwafukuza wageni watazomewa na wapiga kura wao, hawataungwa mkono kama ilivyotokea Nairobi.