Kutokana na upungufu wa umeme unaoikabili nchi yetu ya Tanzania, tunategemea kuwa uwekezaji katika sekta ya nishati utaongezeka, hivyo kuibua changamoto nyingi za kimazingira, kiuchumi na kijamii.
Haya yamebainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira Wizara ya Nishati na Madini, Gedion Kasege, hivi karibuni wakati akifungua semina ya siku tano iliyowahusisha mameneja wa Tanesco nchini ili kujifunza masuala ya uhifadhi wa mazingira (Strategic Environmental Impact Assesment), utwaaji wa ardhi, Sheria ya Mazingira na masuala ya jinsia katika sekta na jinsi ya kukabiliana nayo kuweza kufikia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
Akielezea umuhimu wa semina hiyo kwa mameneja hao, amesema mafunzo hayo yatawapa upeo mkubwa wa kuelewa na kuzingatia masuala mtambuka kwenye miradi ya nishati, hasa katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati ya umeme.
Aidha, amezungumzia shughuli zinazoendelea nchini za utafutaji wa mafuta na gesi ambao kwa kiasi kikubwa utaongeza kiasi cha uzalishaji wa umeme na kuwaasa kuhakikisha kuwa uzalishaji huo unakwenda sambamba na uhifadhi na usimamizi wa mazingira ili kuhakikisha kuwa binadamu na viumbe wengine hawaathiriki na kasi hiyo ya maendeleo.
Kasege amewataka mameneja na wafanyakazi wote wa Tanesco kutambua kuwa kuna sheria, kanuni na taratibu zinazohusiana na utunzaji wa mazingira na utwaaji wa ardhi ili kuepusha migogoro na wananchi na taasisi nyingine kwani kutozingatia taratibu kunasababisha uchelewevu katika kuanza utekelezwaji wa miradi ya umeme.
“uwekezaji wowote lengo lake ni kuleta maendeleo. Kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya 2004, maendeleo yoyote lazima yaendane na uhifadhi wa mazingira kwani mazingira yakiharibika maendeleo hayapatikani,” alisisitiza Kasege.
Aidha, amewataka wasimamizi hao wa miradi kuhakikisha kuwa mpango wowote unapoandaliwa, sera na sheria zinapoandaliwa pamoja na mikakati yake iandamane na Tathmini Mkakati wa mazingira na kila mwekezaji kufanya tathmini ya athari za mazingira kabla ya kuanza shughuli za uzalishaji.
Alisema si rahisi kumaliza kabisa tatizo la uharibifu wa mazingira katika kipindi cha muda mfupi bali ni muhimu kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa mazingira wenye lengo la kuondoa au kupunguza uharibifu wa mazingira.