Juma lililopita nilizungumzia chimbuko na dhana potofu zinazoendelea miongoni mwa jamii yetu kuhusu watu wenye ualbino. Leo naangalia masuala ya utu, afya, haki, matatizo na usalama wao.
“Watu wenye ualbino” kama wanavyotaka wao wenyewe kuitwa, na wasiitwe albino au zeruzeru kwa sababu majina hayo yanadhalilisha utu wao. Binafsi sioni kama kuna udhalilishaji juu yao.
Maneno hayo mawili ya Kiswahili na Kiingereza yote yanatoa maana ile ile moja ya kukosa rangi kamili ya mwili. Ni vyema ndugu zangu wayakubali majina hayo. Nasema ninawaomba wayakubali majina hayo.
Lipo dai kutoka kwao kwamba neno zeruzeru linadhalilisha utu wao, lakini ualbino halidhalilishi utu wao. Ama hii ni ajabu ya kukataza mchezo wa kamari, lakini unaruhusu mchezo wa bahati nasibu, wakati vyote ni kamari.
Utu wa binadamu unatokana na hadhi ya binadamu mwenyewe katika mwenendo wake kwa maana ya tabia, kazi, usafi, upendo na kadhalika. Utu wao ulenge maeneo hayo, siyo jina. Jina pekee halina maana kama hakuna utu.
Kwa sababu wenzetu hawa wana kilema, ukweli wana udhaifu fulani mwilini, huo bado hauzuii wala hauondoi utu wao — kwao na kwetu. Ni haki na wajibu wetu kuwajali, kuwaenzi na kuwatukuza maishani.
Wahenga wanasema, “Afya ni bora kuliko mali.” Msemo huu una maana kwamba hali nzuri ya mwili wa mtu humwezesha kufanya kazi na kupata mali. Mali hiyo humwezesha kuweka mwili wake safi na kuendesha maisha yake vizuri.
Jamii yetu kwa makusudi ina wajibu mkubwa wa kutunza afya za watu wenye ualbino, ili nao waweze kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi na elimu. Uchumi na elimu ndiyo mnasuo wa udhalilishaji wa utu wao.
Juhudi zinazofanywa sasa na Serikali za kutunza afya zao katika baadhi ya vituo na shule haitoshi. Ipo haja kubwa kwa watu binafsi, vikundi, mashirika na kampuni mbalimbali nchini kushiriki kutoa huduma za tiba na afya kwa watu wenye uablino.
Madhali watu wenye ualbino ni binadamu kama wewe na mimi, ukweli wanayo sifa ya kupewa haki zao za msingi, na hasa haki ya kuthaminiwa utu wao. Ulemavu wao si hati ya kudhalilishwa utu wao.
Hivi ninavyozungumza, watu wapatao 200 katika nyakati tofauti wamekamatwa na polisi nchini kote, wakituhumiwa kunyofoa au kukata baadhi ya viungo vya mwili au kuua watu wenye ualbino.
Kutokana na tuhuma hizo, ni kesi 10 zilizofikishwa mahakamani kati ya mwaka 2008 na mwaka 2014, na kesi tano zimetolewa hukumu za wahalifu kunyongwa, lakini hawajanyongwa kutokana na maridhiano ya haki za binadamu.
Hicho nacho ni kitendawili kipya na kigumu. Nasita, lakini natamka huyu aliyeuawa haki za binadamu hazimhusu? Ila aliyeua ndiye haki zinamhusu? Ufafanuzi wa kisheria una mambo yaliyo kinyume cha utu.
Aidha, inadaiwa kuwa vyombo vya kusikiliza na kutoa hukumu juu ya kesi kama hizo havina fedha za kugharimia uendeshaji wa kesi kwa kuwaita mawakili na mashahidi ili haki zipatikane!
Mazingira kama hayo ya haki za binadamu na bajeti ndogo au haipo inatoa taswira gani kwa wapenda haki na amani; na kwa wapenda dhuluma na ukatili ndani ya jamii yetu?
Ni dhahiri shahiri kundi la haki na amani litasononeka na kundi la dhuluma na ukatili litafurahia. Katika hali kama hii imani ya ndugu zetu hawa kwetu ni ndogo sana kama haipo kabisa mbele yao.
Tumewasikia wakati wanaadhimisha miaka tisa tangu kuundwa kwa chama chao cha watu wenye ualbino wakisema kwamba bado wananyimwa au wanakosa haki zao za msingi katika jamii ya Tanzania.
Ukweli wanazo sababu za kusema hivyo kutokana na mazingira niliyoyaelezea. Sasa tufanye nini? Kuna mambo matatu ya kufanya kwao.
Kwanza, kuwakubali na kuwathamini kuwa wao ni binadamu. Pili, tuwalee, tuwatunze na kuwalinda kwa kuwajengea mazingira bora na salama kuanzia nyumbani hadi shuleni na kazini. Pia kuwajenga kiimani kwa vitendo katika mazingira ya matembezi yao.
Tatu, kesi zilizopo mahakamani zisikilizwe na zitolewe hukumu zisizo na makengeza. Kama tulilia na kuahidi kutokomeza ukatili dhidi yao, ni nini kinachotufanya tushindwe kutimiza kilio na ahadi?