Wimbi la matukio yanayohusishwa na ugaidi limeendelea kuitesa nchi ya Kenya kwa kuua na kujeruhi watu, kuharibu mali mbalimbali na kuisababishia hasara kubwa.
Wiki iliyopita watu zaidi ya 10 waliripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa wakati wa milipuko miwili iliyotokea katika soko kubwa la nguo la Gikomba mjini Nairobi.
Huo ni mfululizo wa matukio kadhaa yanayohusishwa moja kwa moja na ugaidi likiwamo lililoshambulia kituo cha maduka ya kifahari cha Westgate jijini Nairobi.
Ilielezwa kwamba kikundi cha Al-Shabaab kinachopambana na wanajeshi wa nchi ya Somalia, ndicho kilichohusika kutekeleza shambulio hilo kubwa la kigaidi kutokea nchini Kenya.
Kuna maelezo kwamba kundi la kigaidi kutoka Somalia limeapa kuendeleza mashambulizi katika nchi ya Kenya, ambayo imepeleka majeshi yake kusaidia kuzuia mapigano nchini Somalia.
Mashambulizi yanayotokea nchini Kenya kuna uwezekano yakavuka mipaka na kuingia hapa Tanzania, kutokana na ujirani na mwingiliano wa watu katika nchi hizi.
Inaelezwa kwamba shambulio lililotokea Westgate na mengineyo nchini Kenya, yanasadikika kusababishwa na upungufu wa ulinzi na usalama katika vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo.
Kwa mantiki hiyo, ni vema vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hapa Tanzania vikajifunza kutokana na vitendo vya ugaidi vinavyowaandama majirani zetu Wakenya, hivyo kuhakikisha kuwa vinaimarisha ulinzi katika maeneo yote ya nchi yetu isije kukutwa na yanayoikuta Kenya.
Ulinzi uimarishwe katika maeneo muhimu na yenye vitegauchumi hapa nchini, kwani uzoefu umeonesha kwamba ndiyo maeneo yanayoangazwa zaidi na magaidi.
Serikali ichukue hatua ya kuhakikisha mipaka ya nchi yetu na maeneo nyeti yanawekewa ulinzi wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na vifaa vyenye teknolojia ya kisasa inayotambua mapema viashirio vya matukio ya ugaidi ili tusije kujuta mwisho wa siku yatakapokuwa yametukuta.
Lakini pia, wananchi wanaokabidhiwa kusimamia vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini wachunguzwe na kuthibitishwa pasi na shaka yoyote kuwa ni wazalendo, waadilifu na waaminifu kabla ya kukabidhiwa jukumu hilo nyeti linalobeba maslahi ya Taifa letu.
Ninasema hivyo kwa sababu kuna habari kwamba baadhi ya watu wanaokabidhiwa majukumu katika maeneo nyeti zikiwamo taasisi za fedha, wamekuwa wakishiriki kwa siri kufanya uhalifu katika maeneo yao ya kazi.
Ni wazi kwamba vitendo vya ugaidi vina madhara makubwa katika maendeleo ya nchi. Sote tunasikia na kushuhudia vitendo vya ugaidi vinavyoitesa Kenya na nchi nyingine mbalimbali duniani. Ugaidi ni moto wa kuotea mbali!
Mashambulio ya kigaidi yanasababisha mauaji ya watu kikatili, huku wengine wakipata vilema vya kudumu, hali ambayo inadhoofisha nguvukazi ya taifa na kudidimiza maendeleo kutokana na uharibifu wa mali mbalimbali.
Tunajua kwamba majeshi yetu ya ulinzi na usalama yamejipanga vizuri kukabili uhalifu wa aina yoyote katika maeneo nyeti, lakini bado kuna haja ya kuongeza msukumo wa kuimarisha ulinzi kwenye maeneo mengine yakiwamo maduka ya kifahari na benki.
Wadadisi wa masuala ya usalama na amani wanasema Tanzania haipaswi kubweteka na ulinzi uliopo sasa, kwani bado kuna maeneo muhimu ya kiuchumi hapa nchini ambayo ulinzi wake hauridhishi.
Kama ambavyo machafuko ya kigaidi yalivyoanza kuivuruga Somalia kabla ya kuvuka mipaka na kuingia Kenya, ndivyo inavyoweza kuwa rahisi kwa vitendo vya ugaidi vinavyotokea Kenya kuvuka mipaka na kuingia hapa nchini, ingawa hatuombi janga hilo litukumbe.
Wahamiaji haramu hapa nchini wasakwe sambamba na Watanzania wachache wasio na chembe ya uzalendo wanaowahifadhi ili wote wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Tanzania inaweza kuzuia kila aina ya ugaidi. Kazi ni kwenu vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Mungu ibariki na kuilinda Tanzania dhidi ya ugaidi.