Katika mfululizo wa makala za bandari, wiki hii tunakuletea makala ya uhudumiaji wa shehena za mafuta na gesi katika bandari za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), hususan katika Bandari ya Dar es Salaam.

Shehena za mafuata huagizwa na Petroleum Bulk Procurement Agency (PBPA), ambao ni wakala wa serikali. Wakala huu uliundwa kuepuka msongamano wa meli bandarini, hivyo kupunguza au kuondoa kabisa gharama za tozo zitokanazo na meli kukaa muda mrefu bandarini (demurrage charges).

Faida nyingine ya wakala huo ni kuhakikisha upatikanaji wa takwimu za shehena za mafuta unakuwa sahihi ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kuna mizania ya kiuchumi inayoleta malipo ya kiwango cha chini kumnufaisha mtumiaji.

Shehena ya mafuta au gesi huagizwa kwa pamoja na PBPA kwa ajili ya wateja mbalimbali. Baada ya meli ya mafuta au gesi kufunga bandarini, kila mteja hupelekewa shehena yake ya mafuta au gesi kulingana na kiasi alichoagiza kupitia miundombinu ya mabomba maalumu kutoka bandarini hadi kwa mteja husika.

Katika Bandari ya Dar es Salaam kuna gati maalumu kwa ajili ya kuhudumia meli za mafuta na gesi. Gati hiyo inajulikana kwa jina la Kurasini Oil Jetty (KOJ) ambayo ina sehemu mbili ambazo ni KOJ1 na KOJ2.

KOJ1 ina uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa kubeba mafuta hadi tani 45,000 na KOJ2 ina uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa kubeba mafuta hadi tani 5,000. KOJ inahudumiwa na meli za mafuta ya aina zote, yakiwemo mafuta ya kula, mafuta ya taa, mafuta mazito, dizeli, petroli, gesi na mafuta ya ndege.

Pamoja na KOJ, kuna gati nyingine ya kuhudumia mafuta ambayo ipo baharini upande wa Mji Mwema, Kigamboni. Gati hii inaitwa Single Point Mooring (SPM) au Single Buoy Mooring (SBM). Gati ya SPM ina uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa kubeba mafuta hadi tani 150,000.

Gati hii ya SPM inahudumia meli za mafuta ya dizeli tu na mafuta ghafi kwa ajili ya Zambia. Mafuta ghafi hayo husafirishwa kupitia mabomba maalumu ya TAZAMA kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Ndola, Zambia kwenye kiwanda cha kusafishia mafuta.

Meli ya mafuta au gesi baada ya kuwasili bandarini, wataalamu wa TPA uhakikisha meli husika imefunga katika eneo lenye mitambo maalumu inayounganishwa na mabomba kushusha shehena ya mzigo huo. Baada ya hatua hiyo kukamilika, Nahodha pamoja na Afisa Mkuu wa meli hukabidhi nyaraka za mzigo wa mafuta waliouleta kwa maafisa wa TPA. Nyaraka hizo zinahusu taratibu mbalimbali zinazotakiwa kufuatwa wakati wa kushusha mafuta husika.

Baada ya makabidhiano ya nyaraka za utaratibu wa kupakua mafuta, hatua inayofuata ni upimaji wa mafuta kwenye meli. Kazi hiyo hufanywa na wataalamu wa Upimaji wa Mafuta (Surveyors). Lengo la kupima mafuta kwenye meli ni kulinganisha mafuta yaliyomo kwenye meli na kiasi cha mafuta kilichoonyeshwa kwenye nyaraka zilizokabidhiwa kwa mamlaka husika.

Wataalamu hao wa upimaji wanatoka kwenye makampuni yaliyosajiriwa na yanayotambuliwa na serikali. Kikundi cha wataalamu hao ni kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), mwagizaji wa mafuta na mpokeaji wa mafuta.

Hatua ya upimaji wa mafuta ikishakamilika ndipo kazi ya upakuaji wa mafuta au gesi huanza kulingana na kila mteja alivyoagiza. Mafuta au gesi hupakuliwa baada ya mamlaka husika kutoa vibali vya kuruhusu upakuaji huo wa mafuta husika, baada ya kujiridhisha ubora na uhalali wake kiviwango na ulipaji wa kodi ya serikali na tozo mbalimbali.

Kazi ya kupakua mafuta au gesi hufanywa kwa kumpelekea mteja mmoja mmoja kulingana na aina ya mafuta aliyoagiza na kiasi cha mafuta alichoagiza. Mafuta husukumwa kwa kutumia pampu maalumu zilizomo kwenye meli. Mafuta hayo husukumwa na kupelekwa kwa mpokeaji kupitia mabomba yake kutoka bandarini hadi kwenye matanki yake ya kutunzia mafuta.

Katika kituo cha KOJ pamoja na kuhudumia mafuta ya bidhaa za petroli, pia kituo hicho kinahudumia meli za mafuta ya kula (vegetable oil), ambapo kila mwezi kuna walau meli moja inayoleta mafuta ya kula. Mafuta hayo ya kula hupakuliwa kwa kutumia mabomba tofauti na mabomba ya mafuta mengine.

Wakati wa kupakua mafuta bandarini, tahadhari katika upakuaji wa mafuta huchukuliwa kulingana na sheria na kanuni za usalama. Katika Bandari ya Dar es Salaam kuna mitambo maalumu ya kuzimia moto endapo ajali ya moto inaweza kutokea. Mitambo hiyo hutumia maji na dawa maalumu ya kuzimia moto.

Pia kuna ‘tugs’ ambazo zinaweza kutumika kuzima moto iwapo moto unaweza kutokea upande wa baharini. TPA ina Jeshi imara la Zimamoto na Uokoaji ambalo ni lenye uwezo wa kukabiliana na ajali za moto.

Kabla serikali haijaanzisha Wakala wa uagizaji mafuta kwa pamoja, kila kampuni ya mafuta ilikuwa inaagiza mafuta kivyake, hali iliyosababisha msongamano wa meli nyingi ndogondogo bandarini. Kwa sasa meli za mafuta zinazoleta mafuta bandarini ni kubwa, hatua iliyoondoa msongamano wa meli za mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.

Iwapo una tatizo au swali kuhusu huduma za bandari usisite kuwasiliana nasi kwa kupiga simu au kutuma meseji za bure kupitia namba 0800110032 au 0800110047.