Watanzania tuna kitu kinachotusumbua. Tunataka kujenga jamii iliyo bora. Tunataka kujenga jamii yenye mshikamano na uzalendo. Tunataka kujenga jamii yenye maadili mema na kuwarithisha watoto wetu maadili hayo. Tunataka kujenga jamii ambayo itarithisha vizazi vijavyo Tanzania yenye neema. Tutaijenga vipi jamii hii? Tuanze kutafakari na kufikiri. Tunahitaji wanafalsafa wa Kitanzania ambao watakaa chini na kukuna bongo zao kama walivyofanya wanafalsafa wa mwanzo.
Sote tunalilia Katiba mpya. Ni jambo zuri na wala sina matatizo na hili. Lakini katiba bila kuwa na chombo cha kutuunganisha ni kazi bure. Tumeshuhudia nchi nyingi zenye katiba nzuri na iliyotengenezwa kwa kuwashirikisha wananchi lakini nchi hizo zinaingia kwenye machafuko na vurugu kubwa.
Tulishuhudia kule Mtwara wakati wa mabishano ya gesi, hasira za watu hadi wanachoma gari na nyumba. Hasira kama hizo ni ishara ya kutokuwa na fikra pevu. Ni ishara kwamba watu hawana mwongozo mzuri wa kufikiri na kutenda. Watu hawana kitu cha kuwaunganisha! Na hii ni hatari kabisa. Ni lazima tuanze kutengeneza mfumo wa kuzama kwenye fikra. Hili litatusaidia kufikia hatua ya kujenga chombo cha kutuunganisha kama taifa.
Ninapendekeza hekalu. Tukilijenga Hekalu la Tanzania halitakuwa na chama, halitakuwa na dini, halitakuwa na kabila. Hekalu “nyumba ya Mungu”, nafasi ya watu kukutana na kuungana, litawapokea wote, wanawake, wanaume, watoto, wazee, wasiojiweza, yatima, walemavu nk.
Katika hekalu hili tunaweza kuwafundisha vijana wetu maadili. Sasa hivi hakuna sehemu yoyote ya kuwafundisha vijana maadili. Ni wapi? Shuleni hakuna nafasi ya kufundisha maadili, vyuo vyetu havina nafasi ya kufundisha maadili, viongozi wa dini nao hawana tena nafasi ya kufundisha maadili.
Mwingine anaweza kupendekeza kitu kingine ambacho ni tofauti na vyama vya siasa na dini. Vyama vya siasa vimeonyesha kuligawa taifa badala ya kuliunganisha, vimepandikiza chuki na kuwatenga wateule wachache wa kula matunda ya taifa letu.
Dini nazo zinawagawa watu badala ya kuwaunganisha. Hii mifumo inayowagawa watu ni hatari sana na hasa kwa vijana, maana vijana wanayumbishwa haraka. Hivyo wanahitaji mfumo ulio imara ambao utawaunganisha na kuwajengea umoja na mshikamano.
Ninashindwa kupata neno zuri zaidi ya hekalu. Labda wengine wanachanganya neno hekalu na nyumba za ibada tulizozizoea. Sina maana ya kanisa wala msikiti. Nina maana ya “kitu” cha kuwaunganisha Watanzania wote. Nafasi isiyokuwa na tabaka, nafasi isiyowatenga matajiri na maskini, waheshimiwa na walalahoi. Nafasi isiyowatenga wanaume na wanawake, kabila na kabila na dini na dini. Ni mtu gani ana neno zuri zaidi ya hekalu? Basi ajitokeze.
Ninaamini kwamba Watanzania tunahitaji kitu cha kutuunganisha. Tunahitaji kitu cha kujenga uzalendo. Kitu cha kujenga maadili yetu. Tunahitaji kitu cha kutufanya kuipenda si Tanzania ya leo tu, bali na Tanzania ya vizazi vijavyo. Nilishaeleza kule nyuma kwamba mifumo yote tuliyonayo sasa hivi haitusaidii. Vyama vya siasa havitusaidii, dini hazitusaidii. Tufanye nini?
Vitabu vya Dk. Adolf Mihanjo na Padri Stephen Kaombe juu ya falsafa kwa Kiswahili ni msaada mkubwa kwa kila mtu anayethamini kufikiri na kutafakari mambo mbalimbali katika jamii. Katika vitabu hivi mtu anagundua jinsi maendeleo ya mwanadamu yanavyokuja kwa watu kukaa chini kufikiri na kutafakari, na kwamba wanadamu wanasumbuliwa na mambo mbalimbali katika vipindi mbalimbali vya maisha.
Wakati huu sisi tunasumbuliwa na namna ya kujenga jamii iliyo bora, yenye mshikamano, maadili na uzalendo. Wanafalsafa wa mwanzo wa kule Uyunani walisumbuliwa na kutaka kujua chanzo cha kila kitu. Kwa vile wao walianzisha hoja hiyo na kuitafakari, iliendelea na kufikia kiasi kwamba si hoja tena. Falsafa yao ilisaidia sana maendeleo ya sayansi ya siku hizi.
Mfano sasa hivi tunapojadili kuhusu Katiba, tungezama kwenye fikra na kuhoji juu ya katiba. Ni lazima kuwa na katiba au tunaiga kutoka kwa watu wengine? Hatuwezi kuendesha nchi bila katiba? Faida ya katiba ni nini na hasara za kutokuwa na katiba ni nini?
Leo hii ni Watanzania wangapi wanafahamu maana ya katiba na umuhimu wa kuwa na katiba? Ni wangapi wanajua kwamba wanaweza kuwawajibisha viongozi wao wakikiuka katiba? Ni Watanzania wangapi wanafahamu wajibu wao ndani ya katiba, kwamba na wao wakienda kinyume cha katiba wanawajibishwa? Ni nani anayajadili haya? Tunabakia kuorodhesha kila kitu kwamba kiwe kwenye katiba bila kuwa na ufahamu wa kina katiba ni kitu gani?
Si lengo la makala hii kufundisha falsafa. Ni kutaka kuonyesha jinsi fikra zinavyosaidia kuleta maendeleo. Ni namna ya kutaka kuonyesha kwamba hatuwezi kuwategemea wanasiasa na viongozi wa serikali peke yao kutuletea maendeleo. Ni kutaka kuonyesha kwamba watu wanapokuwa na kitu kinachowasumbua au ambacho wangetaka kujua, wanakaa chini na kutafakari na kuleta hoja mbalimbali. Mfano hawa wanafalsafa wa mwanzo, kwa kutafuta chanzo cha kila kitu walijaribu kila kitu, huyu anasema ni maji, huyu anasema ni hewa, huyu anasema ni moto, huyu anasema ni hesabu na mwingine anasema ni atomi. Kila hoja inajengwa juu ya nyingine, hatimaye kinapatikana kitu cha manufaa kwa jamii husika na wakati mwingine kwa dunia nzima.
Bunge, lingeweza kufanya kazi ya kuliunganisha taifa. Lakini mfumo tuliourithi kwa wakoloni ni mbovu na hauwezi kusaidia kutuunganisha na kujenga uzalendo. Kama wabunge wetu bado wanaamini kuna mambo ya kujadili kwa siri bila waandishi wa habari kuyafahamu. Bunge limekuwa likiilinda serikali badala ya kuisimamia. Hakuna matumaini.
Azimio la Arusha ulikuwa msingi imara ya kulijenga na kulisimika hekalu letu. Ujamaa na kujitegemea zilikuwa nguzo imara za kulisimamisha hekalu letu. Mwalimu Nyerere, alitaka kutujengea Hekalu la Kitanzania, hekalu ambalo lingemkumbatia kila Mtanzania. Hekalu ambalo kila goti liwe la kiongozi, la tajiri, la maskini lingepigwa. Hekalu ambalo lingelinda uhuru, haki na heshima ya kila Mtanzania. Hekalu ambalo lingelinda utajiri wa taifa letu, utamaduni wa taifa letu na maadili ya taifa letu.
Tulisitisha ujenzi wa hekalu kwa makosa, sasa ni wakati wa kulijenga tena. Hii ndiyo changamoto kubwa waliyonayo vijana wa Tanzania. Vijana wasikimbilie kutaka uongozi, kabla ya kuujenga msingi! Bila msingi, kamwe hawatasimama na taifa zima litayumba. Tunahitaji fikra pevu. Ni lazima kupambana na ulemavu wa fikra kwa nguvu zetu zote.