Nakusihi wewe ambaye umeumizwa na mzazi wako, ‘msamehe’. Umeumizwa na mtoto wako wa kuzaa, ‘msamehe’. Umeumizwa na mume wako, ‘msamehe’. Umeumizwa na mke wako, ‘msamehe’. Umeumizwa na kaka yako, au dada yako, ‘msamehe’. Umeumizwa na jirani yako, ‘msamehe’. Umeumizwa na rafiki yako, ‘msamehe’. Umeumizwa na mwajiri wako, ‘msamehe’. Kusamehe ni bure. Yawezekana kwa wakati huu mambo yako hayaendi sawa. Una mawazo. Hupati usingizi. Unawaza lakini hupati majibu ya mawazo yako. Unahisi umetengwa. Unahisi umekataliwa na familia au jamii. Unakuwa mtu wa kunung’unika kwa kila jambo.
Mwandishi Dresch Messenger anasema: “Maadui wako ni rasilimali yako ya thamani kama haulipi kisasi kwa sababu wanakufanya uwe macho na kuchapa kazi vinginevyo ungebweteka.” Na mwandishi mwingine aitwaye Sidney Sheldon anasema: “Kufanikiwa unahitaji marafiki na kufanikiwa sana unahitaji maadui”.
Mwandishi wa habari, David Brinkley, naye anafafanua kwamba: “Mtu aliyefanikiwa sana ni yule ambaye anaweza kuweka msingi imara kwa matofali yale ambayo wengine humrushia kumpiga nayo’’. Maisha yanaweza kukurushia matofali mengi. Yadake na yatengenezee msingi ambao utakuwezesha kusonga mbele. Maadui zako pia ni warushaji wa mawe. Daka mawe yao na jenga ngazi.
Usiruhusu mambo hasi yanayotokea katika maisha yako yakufanye na wewe uwe ‘hasi’. Yageuze kuwa kitu chanya na yatumie kama msingi wa hatua inayofuata. Yatumie maneno wanayokusema watu kama mawe ya kuvukia ng’ambo ya pili ya mafanikio yako.
Tusiwachukie wanaotuchukia, tuwapende ili waone wema na upendo wa Mungu kupitia kwetu. Adui ni wa kumuombea mazuri ili yale mazuri anayopata na kukutana nayo yambadilishe kuwa mtu mzuri. Hilo linawezekana. Ukimchukia anayekuchukia unakosea.
Athisthenes, mwanafalsafa wa Kigiriki alipata kusema: “Wasikilize maadui wako, kwa sababu ni wa kwanza kugundua makosa yako.” Yesu alikuwa sahihi kabisa aliposema: “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi.’’ [Mat. 5:44]. Ipo methali ya kabila la Wafipa inayosema: “Mvua ya Mungu huwanyeshea hata washirikina.” Martin Luther King, mwanaharakati mweusi alipata kusema: “Giza haliwezi kutokomezwa na giza, bali hutokomezwa na mwanga tu. Vivyo hivyo chuki haiwezi kutokomezwa na chuki, bali ni upendo tu unaoweza kufanya hivyo.”
Jifunze jambo kutoka kwenye maisha ya hawa majirani wawili. Huko Amerika ya Kusini kuna mama wa Kizungu na mama wa Kiafrika waliwahi kuishi eneo moja la makazi kama majirani. Mama wa Kizungu alikuwa na tabia ya kutupa kinyesi kwenye eneo la mama wa Kiafrika.
Yule mama wa Kiafrika hakulipigia kelele jambo hilo. Siku moja mama wa Kizungu aliugua sana. Mama wa Kiafrika alikwenda kumtembelea hospitalini. Alimpelekea maua mazuri kama zawadi. Mama wa Kizungu alipoyapokea yale maua kama zawadi nzuri kutoka kwa jirani yake akauliza: “Umeyanunua wapi maua mazuri haya?”. Mama wa Kiafrika akamjibu: “Niliyaotesha kwenye kinyesi ulichokuwa unanitupia.” Mama wa Kizungu akanyamaza kwa dakika chache. Baada ya dakika chache za ukimya akafumbua kinywa chake na kusema: “Nakuomba unisamehe.” Malipo ni hapa hapa duniani. Tenda wema uende zako. Wema ni akiba.
Namna bora ambayo Mwenyezi Mungu anapendelea tuishi na maadui wetu ni hii; adui yako anapokata tamaa – mtie moyo. Adui yako anapokuwa dhaifu – msaidie. Adui yako anapokuwa mjinga – mfundishe. Adui yako anapokuwa na majivuno – ishi maisha ya unyenyekevu ili ajifunze unyenyekevu kutoka kwako.
Adui yako anapokuonyesha dharau – mwonyeshe heshima. Adui yako anapovaa sura ya chuki – vaa sura ya upendo. Adui yako anapovaa sura ya huzuni – vaa sura ya matumaini. Padri Faustine Kamugisha katika kitabu chake cha ‘Mafanikio yoyote yana sababu’ anasema: “Maadui wanaweza kukusaidia bila kujua.” Kwa namna fulani adui yako anaweza akawa mtaji wa mafanikio yako. Goliati aligeuka kuwa mtaji kwa Mfalme Daudi. Bila adui Goliati, Daudi asingechukua kiti cha Kifalme. Mungu alimbariki Daudi kupitia kumshinda Goliati. Kwa namna fulani adui Goliati alisaidia kampeni za Daudi kukitwaa kiti cha kifalme.