Wiki iliyopita hadithi hii iliishia katika aya inayosema: “Tatizo jingine ni pale nilipotaka kutembea kidogo; ilipaswa kule nilikoelekea watu wataarifiwe kuwa nitapita eneo hilo kwa hiyo wachukue tahadhari nisije nikawakanyaga kwa bahati mbaya nikiwa katika mishemishe zangu. Hii ilikuwa kero sana kwa wenyeji wangu.” Je, unafahamu nini kinafuata. Endelea…

Hata hivyo watu hawa walikuwa weledi sana na walikuwa na teknolojia ya mawasiliano iliyoendelea sana. Walikuwa wamenivisha kidubwasha hivi kichwani na kutokana na utaalamu wao, kile chombo kilimfanya aliyevalishwa kusema ukweli tu na kuelewana nao, wenyewe waliita mashine hiyo “msema kweli”. Utaalamu wa mashine hii ni kuwa ukiwa umevalishwa ulikuwa huwezi kusema uongo na uliweza kuelewana na watu wa lugha tofauti tofauti bila shida. Mashine hii ilikuwa na uwezo wa kusoma midomo na mawazo ya mtu aliyevalishwa.

Rafiki zangu hawa walikuja kunifahamisha kuwa nchi yao ilikuwa na maadui wengi kwa sababu ya maendeleo yao ya kisayansi, kwa hiyo waliniomba niende kuwashikisha adabu maadui hao ili neema katika nchi hii iendelee.

Hata hivyo maadui waliposikia ujio wangu waliahirisha mipango yao ya kuvamia rafiki zangu kwa kuhofia nisije nikawaangamiza nchi nzima. Jambo ambalo kwa hakika sikupenda litokee, kwani aliyewaleta viumbe hawa ndiye aliyenileta mimi, kwa hiyo wao pia walistahili kuishi hadi aliyewaleta atakapowaita tena.

 Bulongo, nilikaa na watu hawa kwa muda, na tatizo likawa hilo la chakula na adha ya kutoa tahadhari kila nilipotaka kutembelea eneo fulani. Nikajiongeza! Niliomba ruhusa ya kuondoka na kwa kufuata uhalisia wa mambo niliruhusiwa niende bila mjadala.

Siku ya kuondoka, niliondoka polepole na kwa tahadhari ili nisije nikawakanyaga rafiki zangu hawa. Hapo awali mwendo ulikuwa mdogo mdogo, lakini kadiri nilivyotoka katika nchi hiyo mwendo wangu ulizidi kukolea kisha kwa kweli nikaanza kukimbia, sijui nilikuwa ninaelekea wapi, lakini mwendo uliendelea. Sijui nitokako na sijui niendako.

Baadaye nilimkuta bibi kizee mmoja alikuwa ananiangalia kwa mshangao na huzuni. Alinifanyia ishara ya kuwa nimwendee. Nilikwenda mpaka karibu yake nikamsalimia. Shikamoo bibi.  Akajibu: “Marahaba kijana”. Kisha akaendelea kuniuliza: “vipi babu! Na huku tena?” Akishangaa! Nikamjibu: “Bibi sijui nitokako na wala sijui niendako.  Ila kwa hakika ninataka niende nyumbani kwa wazazi wangu na watu wangu”.

 “Ndiyo ninaelewa sana”.  Akasema na kuendelea: “Heri ungepita ile njia ya kule yenyewe ni fupi na haina mishemishe nyingi kama hii. Hata hivyo utafika. Ila utachukua muda mrefu zaidi kwa kupitia njia hii na ulipofika ni sawa na methali isemayo maji ukiyavulia nguo sharti uyaoge,” Nilijikuta ninamshukuru yule bibi mara mbilimbili. Kisha akaendelea: “Ila kuna masharti ambayo itabidi uwe na moyo wa ujasiri!” Akaendelea.

“Pita hii njia na huko mbele kwanza utakuta kamba njiani. Ichukue na hiyo ndiyo hirizi yako na itakusaidia”. Akaniangalia na kumalizia: “Hiyo kamba ndiyo itakuwa polisi wako wa kukulinda juu, chini na pembeni. Usiiache mpaka utakapofi kwenu.” 

Siku nyingine katika safari yako kijana”, yule bibi aliendelea. “Utakutana na mambo mengi, kitu kikubwa usiogope hayo ni mapito tu na ndiyo safari yako itakavyokuwa. Usiogope,” alisisitiza yule bibi.

Vilevile kijana”, aliendelea: “Utakutana na mambo mengi kabiliana nayo, ukitetereka hautafika kwenu!” Akatabasamu kidogo na nikafanikiwa kuyaona meno yake ya ajabu. Kwa kweli lilikuwa ni jino moja tu la juu lililotanda ufizi wote wa juu na pale chini pia kulikuwa na meno mawili tu!

“Katika safari yako, pia utakutana na ng’ombe mpole akiwa na mtoto wake. Chukua hiyo kamba uliyopata hapo awali ukamfunge na kisha umkamue yale maziwa yake. Na maziwa haya yatakusaidia katika safari yako hii. Haya nikutakie safari njema kijana wangu”. Yule bibi akamaliza.

Jamani huyu mtu alinichanganya lile jino lake la juu. Lilikuwa ni moja kama la fisi, na yale ya chini kadiri nilivyoyaangalia yalikuwa mawili tu; moja upande huu na jingine upande ule! Ndiyo dunia jamani. Ni kweli mimi ni mdogo sana kiumri, lakini niliyowahi kuona ni mengi mara elfu ya mtu mzima aliyoona.

Basi rafiki yangu Bulongo Gwike, ndipo nikaanza hiyo safari ya kurudi nyumbani ambako nyie mlikuwa mmemaliza matanga na kwa uhakika mlikuwa mmeanza kunisahau. Safari hii ilinichukua miaka mitatu mpaka siku moja wewe rafiki yangu uliponigundua kule porini, mimi nilikufahamu mara moja, lakini wewe nina uhakika moyo wako ulipata shida sana kuamini kuwa mimi ni rafikiyo Bhugulugulu Duu. Moyo wako ulipata kigugumizi kunitambua!

Sijui mlinionaje, ni kweli nilikuwa sijanyoa nywele na ndevu zangu miaka yote mitatu; hata kucha zangu zilikuwa zimerefuka sana kwani nyenzo za kukatia kucha na nywele huko hazipo. Pia huko kulinifurahisha zaidi kwa vile nilikuwa nikipata mlo mmoja mzuri wenye virutubisho vya kutosha basi njaa ilikuja tena baada ya mwaka mzima. Ni hakika kabisa kuwa nikiwa huko niliwahi kula mara tatu tu kama sikosei, na mara ya mwisho kula ilikuwa miezi sita iliyopita ulivyokuja kuniona kule porini.

Nilikuwa na kama miezi sita sijala na afya yangu ilikuwa kawaida tu! Vilevile nikiwa huko siku ya kula ndiyo ya kunywa maji na kuoga. Na baada ya kula, kunywa na kuoga unaendelea na safari. Hakuna njaa!  Hakuna kiu wala kuchoka! Je, mliponiona nilikuwa nimechafuka sana?

Basi rafiki yangu Bulongo Gwike, safari yangu ndivyo ilivyoanza. Nilkuwa ninarudi nyumbani ila njia siijui, basi nikawa natembea tu. Upweke wa eneo hili ulinipa nguvu za kuendelea kutembea. Nilitembea kwa muda wa majuma kadhaa usiku na mchana.

Nilipita milima na mabonde nikapita mapori na vichaka.  Siku moja nikiwa katika safari yangu, kwa mbele nilimuona nyoka mrefu aina ya koboko. Mwili uliishiwa nguvu. Nikaanza kukimbia ili kujiokoa. Kuona hivyo yule nyoka pia akaanza kunifukuza.

Ilikuwa pata shika. Bahati nzuri alipokuwa anajitayarisha kunigonga, nikapata ujasiri nikamkamata shingoni kabla hajatimiza azima yake ya kunidhulu. Mara akageuka na kuwa kamba! Mungu wangu na hapo ndipo nikakumbuka yale maneno ya yule bibi kuwa nitakuta kamba njiani. Niichukue! Na niivae shingoni! Itanisaidia, alisisitiza, nikakumbuka.

Hali hii rafiki yangu ilikuwa ya kutisha sana. Mimi sijawahi kushika nyoka katika maisha yangu yote. Sasa nilipata wapi ujasiri na nguvu za kumkamata koboko huyu nyoka wa hatari mimi sina maelezo ya maswali haya. Na ukweli ni kuwa ile kamba ninayo shingoni hadi hivi sasa. Hapa niliamua nitulie kwanza na akili yangu ifanye kazi vizuri zaidi.

Nilitafuta kivuli cha mti nikaamua nikae na kutulia, kisha niendelee na safari yangu ya kujikomboa. Kivulini pale, usingizi ulinichota na tena ukawa wa mang’amung’amu mara niote ninacheza na simba! Mara niote ndege wote duniani wanakuja kunitetea eti niachiwe! Kunguru walikuwa wananililia “Gwa! Gwa! Gwa!” Walikuwewpo pia wale ndege weusi wamekaa kwenye jopo lao wakitafuta namna ya kunisaidia ili nirudi nyumbani.

Kina mwewe pia walikuwepo wananyakua matambara kwa fujo kisha wanalia Zwi! Zululu! Ndege wengine wadogo walikuwa wanaruka juu juu na baadhi yao walikuwa wanaruka chini chini. Bata mzinga nao pia walikuwa wanahimiza wakisema mrudisheni mtoto wetu jamani, mrudisheni kwani amepotea na tunamtafuta.

Je, unafahamu nini kiliendelea baada ya hapo? Usikose sehemu ya tano yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa simu namba 0755629650.