Wakati nchi ikijiandaa kwenda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadaye Uchaguzi Mkuu 2020, Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) inazidi kuwapatia wananchi wa Dar es Salaam na Pwani maji.

Ni wakati mwafaka kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi, viongozi wa serikali za mitaa pamoja na kamati za maji kuhusu namna bora ya usimamizi wa shughuli za maji katika maeneo yao, zikiwemo taratibu za umiliki wa visima.

Dawasa imefanikiwa kutoa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira kwa Mkoa wa Dar es Salaam sambamba na kukamilika kwa mradi mkubwa wa Ruvu Chini ambao umeongeza upatikanaji wa maji kutoka lita milioni 182 kwa siku hadi kufikia lita milioni 270 kwa siku.

Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja, anasema Dawasa inajivunia kuzalisha maji yenye lita za ujazo zaidi ya milioni 502 kwa siku. Kiasi hicho cha maji kimepanda tofauti na ilivyokuwa  miaka ya nyuma, ambapo Dawasa ilikuwa ikizalisha lita za ujazo 300,000 kwa siku.

Maji hayo huzalishwa kutoka katika vyanzo vikuu vinne vilivyopo nchini, ambavyo ni Mtambo wa Ruvu Juu wenye uwezo wa kuzalisha lita za ujazo milioni 196, na Ruvu Chini unaozalisha lita za ujazo milioni 270, Mtambo wa Mtoni unaozalisha lita za ujazo milioni 9,000 pamoja na visima virefu ambavyo vinazalisha lita za ujazo milioni 27, kwa siku.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Jiji la Dar es Salaam ndilo jiji kubwa kuliko yote Tanzania lenye watu 4,570,000, hivyo wananchi wanahitaji kupata majisafi na salama kwa ajili ya matumizi ya majumbani pamoja na viwandani.

Luhemeja anasema ustawi wa taifa unategemea sana mafanikio ya shughuli za kimaendeleo jijini Dar es Salaam, na kwa msingi huo, huduma ya uzalishaji wa maji safi na uondoaji wa majitaka ni njia mojawapo ya kurahisisha ukuaji na ustawi.

“Ukweli ni kwamba maendeleo ya viwanda yanaonekana sana maeneo ambayo maji yanapatikana, na kwa upande wa pili ukuaji wa sekta ya viwanda unasababisha ongezeko kubwa la mahitaji ya maji, hivyo Dawasa tunajitahidi kuzalisha maji ya kutosha,” anasema Mhandisi Luhemeja.

Anasema baada ya uhuru kasi ya ongezeko la watu ilikuwa kubwa ambapo idadi hiyo haikuendana na uwezo wa vyanzo vya maji vilivyokuwepo, hivyo kilihitajika chanzo cha ziada kitakachosaidia upatikanaji wa maji.

Mhandisi Luhemeja anasema mwaka 1963 kazi ya ujenzi wa mtambo wa Ruvu Juu ilianza na baada ya kukamilika mtambo huo ulikidhi mahitaji ya wananchi wa jiji hilo, lakini baadaye kasi ya ukuaji wa mji iliongeza idadi ya watu na kusababisha maji kutokidhi mahitaji ya wakazi hao.

 Mwaka 1990 serikali ilianza kuboresha miundombinu ya mfumo wa usambazaji majisafi ikiwemo utafiti wa Kampuni ya Howard Humphreys ambao ulibaini maeneo matano ya kushughulikiwa kwa haraka zaidi.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu ya kuzalisha na kusukuma maji, ukarabati na upanuzi wa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, utafiti wa vyanzo vipya vya maji pamoja na uimarishaji wa mfumo wa kitaasisi.

DAWASA ina wajibu wa kukarabati miundombinu ya maji na kutoa huduma baada ya kubadilishwa kwa sheria na kuundwa kwa Dawasa mpya, hivyo ni lazima ieleweke kuwa jukumu la kulinda na kutunza vyanzo vya maji ni la wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo mamlaka yenyewe.

Huduma ya uondoshaji wa majitaka kwa sasa inapatikana kwa asilimia 10 tu katika Jiji la Dar es Salaam. Hii inatokana na kuwepo kwa miundombinu michache na chakavu ya kutolea huduma hiyo, suala linalosababisha uharibifu wa mazingira kutokana na mabomba kupasuka au kuziba.

Mhandisi Luhemeja anasema Dawasa kwa sasa imewekeza kwenye mtandao wa maji kwa kutumia fedha za ndani na kila mwezi wamekuwa wanatumia Sh bilioni 3 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Gezaulole, Chalinze Mboga, Kisarawe, Kibamba, Kiwalani Phase 3 na miradi mingine.

Luhemeja ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa wa Dar es Salaam upatikanaji wake wa maji ni asilimia 85 ambapo kwa siku yanazalishwa maji lita milioni 502 kutoka kwenye mtambo wa Ruvu Juu, Ruvu Chini, Mto Kizinga na visima vilivyojengwa na jamii au watu binafsi.