*Wasema Njowoka amewasaliti, anazungumza lugha ya Kipande
*Wasema elimu ndogo inamfanya ajikombe, tamko lake lawakera
*Waomba wabunge wambane DG, Mwakyembe, Bodi ivunjwe
*Serikali yamzuia kuvunja Idara ya Masoko, Benki ya Dunia yasitisha mradi
Wafanyakazi wa Bandari wameanza mkakati wa chini kwa chini kuhakikisha wanamng’oa madarakani Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tanzania (DOWUTA), Edmund Njowoka, wanayedai anatafuna fedha za Bandari kama mchwa.
Wafanyakazi hao wameiambia JAMHURI kuwa Njowoka amesahau jukumu la msingi, na kutokana na utaratibu wa kujilipa posho mara tatu kwa kikao kimoja, kama alivyobainisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2012/2013 kuwa ndani ya miezi tisa wametumia Sh bilioni 3.277, umeongeza hasira za wafanyakazi.
Iwapo fedha hizi zingetumika kutengeneza madawati ya mbao kwa ajili ya shule za msingi na sekondari ambazo watoto wanakaa chini nchini, zingetosha kutengeneza madawati 54,617. Hata hivyo, zimeingia mifukoni mwa watu kwa kulipana posho hewa.
“Nilibaini kwamba malipo ya posho kwa ajili ya mikutano hiyo [ya vyama vya wafanyakazi ikiwamo DOWUTA] yalilipwa kwa wajumbe mara mbili au tatu kwa siku bila uthibitisho ulio wazi. Mikutano hiyo iligawanywa katika vipindi ambapo kwa siku kulikuwa na vipindi viwili mpaka vitatu, ambapo wajumbe walilipwa kulingana na idadi ya vipindi ambavyo walishiriki katika vikao. Malipo ya posho ya zaidi ya mara moja kwa siku hayakufuata sera na taratibu za ulipaji wa posho hizo za CJIC, JIC, WC na MWC,” ilisema sehemu ya taarifa ya CAG.
Pia ukiacha taarifa ya CAG, taarifa ya udanganyifu aliyoitoa Njowoka kwa Baraza la Wafanyakazi mjini Morogoro mwezi Februari, kuwa Msajili alimwagiza asogeze mbele uchaguzi kwa mwaka mmoja wakati si kweli, nalo limewakera wafanyakazi.
“Hiyo barua [ya Msajili kuagiza DOWUTA ifanye uchaguzi mwaka huu] tulipopata habari kuwa imeletwa, tumeamua kuanza mikakati ya chini kwa chini kuhakikisha tunamg’oa Njowoka.
“Mwanzo tulidhani mfanyakazi mwenzetu akiingia kwenye Bodi atatetea maslahi yetu, lakini kwa sasa tunajuta. Pengine inatokana na kiwango chake cha elimu [darasa la saba] kwani maandiko mengi kwenye Bodi yanatolewa kwa Kiingereza wakati kwake Kiingereza ni sawa na kukutana na mama mkwe. Hatuna mwakilishi pale,” alisema mmoja wa wafanyakazi.
Mfanyakazi mwingine aliongeza: “Hatua ya Njowoka kuishi kwa posho hapa Dar es Salaam wakati kituo chake cha kazi ni Mtwara haikubaliki. Hakuna kazi yoyote anayofanya zaidi ya kushinda anapiga majungu kwa Kipande. Taarifa aliyoitoa kwenye vyombo vya habari akipinga habari zilizochapishwa na mkombozi wetu JAMHURI, ilitosha ajiuzulu baada ya taarifa ya CAG.
“Sisi tunamwamini Dk. [Harrison] Mwakyembe, lakini katika hili ametushangaza. Tunajiuliza kwa nini wafanyakazi wanaonewa, hata yeye ameyashuhudia haya lakini hakuna anachofanya? Tunaomba wabunge watusaidie sasa, maana hali ni mbaya kuliko maelezo,” alisema mfanyakazi mwingine.
Njowoka kwa upande wake alipowasiliana na JAMHURI hivi karibuni, alisema hawezi kuzungumza kwenye simu na akataka mwandishi aende ofisini kwake.
Mfanyakazi mwingine, naye mbali na kueleza kuwa wameanza mkakati wa chini kwa chini kuhakikisha Njowoka anaachia madaraka na kuondokana na watu wasio na elimu ya kutosha kuongoza DOWUTA, aliomba Bodi ya Wakurugenzi ivunjwe kwani imeshindwa kulisimamia shirika.
“Haya yote yanafanyika Bodi ya Wakurugenzi ikiwa inapata posho tu. Hata aibu hawana. Wajumbe wa Bodi wanakaa kwenye vikao, wanapokea posho na kumpigia makofi [Mzee Madeni] Kipande (58), basi. Sisi tunasisitiza, hatuna nia ya kuona Kipande anaondoka Bandari, bali aongoze Mamlaka kwa kuheshimu utawala wa sheria,” alisema mfanyakazi mwingine.
Habari za kutoka ndani ya Bodi zilizoifikia JAMHURI zinasema Kipande aliwasilisha pendekezo la kufukuza wafanyakazi aliowasimamisha, hali iliyowafanya wajumbe wa Bodi washtuke na kuona anakwenda mbali zaidi.
Wizara na Serikali pia imeanza kufanyia kazi habari zinazochapishwa na JAMHURI.
“Kipande alitaka kuvunja Kitengo cha Masoko, lakini Serikali imeiagiza Bodi imzuie. Tumemwambia hata kama ana ugomvi na mtu, hawezi kuvunja idara kwa sababu ya huyo mtu mmoja. Kuna mambo mengi yanayoendelea ndani kwa ndani na nakuhakikishia Serikali inayafanyia kazi kwa kina zaidi,” kilisema chanzo chetu kutoka serikalini.
Kipande kwa upande wake alipohojiwa na JAMHURI hivi karibuni, badala ya kujibu tuhuma hizi zilizothibitishwa na CAG ikageuka kuwa aibu kutokana na matangazo rundo waliyotoa kwenye magazeti mbalimbali nchini kukanusha habari hizi, alisema maswali anayoulizwa kuhusu masuala ya Bandari ni ya kitoto.
Dk. Mwakyembe yeye ameligeuza suala hili la kisiasa na alipoulizwa aliishia kusema gazeti hili la JAMHURI limemhukumu bila kumsikiliza, hivyo liendelee, lakini hakusema lolote kuhusiana na ripoti ya CAG iliyothibitisha kuwa hapo bandarini wanajilipa posho hadi mara tatu na wakati mwingine wanalipana posho za safari bila kusafiri.
Wafanyakazi hao wenye uchungu mkubwa, wameieleza JAMHURI kuwa uvumilivu wao unakaribia ukomo, kwani kuishi maisha sawa na kuwa gerezani kutawafanya waanze mgomo baridi.
“Hata wafungwa si huwa wanagoma kula bwana! Tunaelekea huko. Kila tunachoahidiwa hakitekelezwi, Kipande amepandikiza vibaraka kila mahala ukisema lolote tu papasi wake wanamfikishia. Hii ni hatari. Uongozi wa majungu ni sawa na kushindwa kazi,” alisema mfanyakazi mwingine.
Wadai Kipande hajafanya lolote
Tambo na mbwembwe za kuongezeka kwa mapato, kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi anazotoa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Madeni Kipande, imebainika kuwa anafaidi matunda ya uwekezaji mkubwa aliofanya Ephraim Mgawe, Mkurugenzi Mkuu, aliyefukuzwa kazi.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu, mwaka 1996 iliiweka Bandari katika orodha ya mashirika ya kubinafsishwa, na hivyo Bandari zote nchini zilikaa miaka 10 bila kufanya uwekezaji wowote hadi mwaka 2006 ilipoondolewa.
Hali hiyo iliifanya Bandari kuwa na hali mbaya sawa na lilivyokuwa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), ambalo nalo baada ya kuwekwa katika orodha ya mashirika ya kubinafsishwa lilikaa miaka 10 bila kuwekeza kitu chochote, hali iliyozaa bomu lililofumka mwaka 2006, nchi ilipopata mgawo wa kutisha wa umeme.
“Kwa Bandari hali iligeuka na kuwa mbaya. Katika muda wa miaka 10 hakukuwapo uwekezaji wala ukarabati wowote. Kiwango cha mzigo kilikuwa kinaongezeka, lakini winchi za kupakua na kupakia mizigo zikawa zinazeeka na kuharibika.
“Bandari ilikuwa na winchi tatu tu, ambazo nazo reli zake zilikuwa zimefumka kwa kiwango ambacho ukizitumia kupakua au kupakia kontena, zinatoka kwenye reli na kuangusha makontena. Mgawe alipoingia akaanza kukarabati winchi hizo.
“Mgawe hakuishia hapo tu, bali aliwaagiza TICTS kununua winchi kubwa, ambayo nayo ilinunuliwa na kuletwa hapa nchini. Winchi hiyo nayo ilikuwa na tatizo, kwani ililetwa na meli kubwa, ikabidi irejeshwe China, ifunguliwe na kupakiwa katika meli ndogo ndogo. Yote haya yamefanyika, na mwaka 2012 yalipokamilishwa, Mgawe akafukuzwa,” kilisema chanzo chetu.
Baada ya uongozi wa Mgawe kubaini kuwa madereva wengi ndiyo waliokuwa wezi pale bandarini, kutokana na posho ndogo ya Sh 5,000 na Sh 10,000 kwa siku za mwisho wa wiki, ulianzisha utaratibu wa madereva kulipwa kwa gari wanaloliondoa bandarini, hali iliyowaongezea pato hadi Sh 40,000 kwa siku na hivyo wakaachana na wizi wa vifaa bandarini.
“Suala la mapato kuongezeka, kina Mgawe waliongeza viwango mara mbili baada ya kufunga mashine za kupakua mafuta kwenye kina kirefu cha Bahari ya Hindi. Viwango vipya vya mizigo vilipitishwa Julai, vikaanza kutumika Novemba [2012], lakini akina Mgawe wakawa wamefukuzwa Agosti [2012]. Ungeondoa ile nyongeza iliyofanywa na akina Mgawe, Bandari ingekuwa inafanya vibaya mno,” kilisema chanzo hicho.
Upande wa mafuta machafu, akina Mgawe walifunga vizuizi (valve) kwenye mabomba ya kupakulia mafuta mwezi Julai, wao wakafukuzwa Agosti, hivyo hata hayo yanayoitwa mafuta machafu hayapo tena pale bandarini.
Hadi mwaka 2009 Bandari walikuwa wanatumia mfumo wa zamani wa kompyuta ujulikanao kama COBAL kwa ajili ya mishahara tu. Mambo mengine yote yalikuwa yanafanywa kwa mkono. Uongozi wa Bandari uliamua kumchukua mtaalamu wa masuala ya kompyuta, Marcelina Mhando, kutoka TICTS. Hata hivyo, baada ya Mhando kuomba kazi, barua yake ya maombi ilifanyiwa mbinu ikaondolewa kwenye orodha ya walioomba kazi na kuchanwa.
“Hii mizigo wanayojigamba kuwa inaongezeka ni masalia ya kilichojengwa nyuma. Kitafika mahali kitapungua. Bandari inakufa unless wanaleta mtu mwingine ambaye ana uchungu na utaalamu wa Bandari, na itamchukua si chini ya miaka mitatu. Port Master Plan wameidharau wanabuni ya kwao. Ilikuwa ya miaka 25 hadi mwaka 2025, kila bandari iwe imejiendeleza katika infrastructure, IT na vifaa, hawa hilo hawalijali.
“Ilipangwa kujenga gati mbili za kontena, limedharauliwa. Suala la Bagamoyo ilikuwa ni baada ya kukamilisha Bandari ya Dar es Salaam, sasa wameelekeza nguvu huko. Kule kuna kujenga reli, kujenga bandari yenyewe, si kitu cha leo.
“Uongozi uliopita uliweka kamera eneo la magari, lakini wakati hilo eneo wanalifanyia paving, wakakata nyaya zote. Kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam haina kamera hata moja,” kilisema chanzo chetu.
Mkurugenzi wa ICT wa Bandari, Phares Magessa, ameithibitishia JAMHURI kuwa kweli CCTV hazifanyi kazi. Chanzo kingine kimeifahamisha JAMHURI kuwa hata Benki ya Dunia iliyokuwa imejitolea kutoa mradi wa CCTV camera na mifumo ya mawasiliano katika Bandari ya Dar es Salaam, mwezi huu imeamua kujiondoa na kusitisha zabuni hiyo kabisa.
“Benki ya Dunia wanataka ushindani, lakini kilichobainika ni kwamba hapa kwetu uongozi una watu wao wanaotaka ndiyo wapewe kandarasi. Benki ya Dunia imelikataa hili na sasa imefuta mradi huu,” kilisema chanzo chetu kilichopo ndani ya uongozi wa TPA.
Bodi ya Wakurugenzi iliyoundwa baada ya kuvunjwa kwa ile ya uongozi wa Mgawe, ilipendekeza TPA kuwekeza katika ICT kama sehemu ya kuokoa uchumi wa nchi hii, lakini kwa shinikizo la Kipande Bodi hii ilivunjwa, Kipande akamshinikiza Dk. Mwakyembe kuweka wapambe wake ambao ni pamoja na Njowoka ambaye aliajiriwa kama mhudumu wa ofisi.
CAG amesema kitendo cha Njowoka kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kinaleta mgongano wa maslahi, kwani Njowoka anapokuwa kwenye Bodi anakuwa bosi wa watendaji wote wa TPA akiwamo Mkurugenzi Mkuu, lakini akitoka tu kwenye kikao anarejea katika ngazi ya utumishi ndani ya Bandari ambapo haripoti hata kwa Afisa Mwandamizi.
Alipendekeza hili liangaliwe kuepusha mgongano wa maslahi na hasa baada ya kubaini kuwa Njowoka hana elimu au uzoefu wowote katika nafasi za juu wakati kazi ya ujumbe wa Bodi ni kushauri kwa kutumia utaalamu alionao mjumbe husika.
“Katika kupitia vyeti vyake, nilibaini kuwa mjumbe huyu ana kiwango cha elimu ya msingi na hajawahi kushika nafasi ya juu katika uongozi katika shirika la umma au kampuni binafsi yoyote.
“Ninavyoona, hii ni kinyume na kanuni na taratibu za utawala bora katika kuliongoza shirika kwa kuzingatia kuwa Bodi inalo jukumu kubwa la kusimamia na kulielekeza shirika katika utendaji wa shughuli zake. Hii inaweza kusababisha mgongano wa kimaslahi na utendaji usioridhisha wa Bodi ya Wakurugenzi,” inasema taarifa ya CAG, Ludovick Utoah.