Ukitaka kufahamu habari za mjini – mji wowote – muulize dereva wa teksi. Kwa kawaida ana taarifa nyingi na muhimu,

na si ajabu kuwa hivyo. Anabeba abiria kila wakati na abiria kama ilivyo tabia ya binadamu yeyote, wana mdomo na hushindwa kukaa kimya kwa muda mrefu. Lazima watakuwa na kitu wanakiwaza na mawazo yanapozidi huyamwaga.

Bila kuulizwa abiria watasema wanatoka wapi, wanakwenda wapi, wameudhiwa na nani, hawapendi nini, wanafanya nini, na watafanya nini. Wakati wote huo wakimjaza dereva data za taarifa ambazo zinahitaji kompyuta kadhaa kuzihifadhi.

Hii sifa haijashika mizizi kwa madereva wa teksi wa siku hizi, wale tunaowatafuta kwa kutumia simu za viganjani, wale vijana wanaoendesha magari ya Uber, Twende, Bolt na huduma nyingine za aina hiyo.

Nazungumzia wale wakongwe ambao bado tunawasimamisha kwa kupiga miluzi. Ukijua cha kuwauliza utajifunza mengi.

Mmoja wao aliniona eneo la mapokezi la Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere miezi kadhaa iliyopita nikihangaika kutafuta zile teksi za teknohama, akanishawishi nichukue yake na kuahidi kunitoza nauli ile ile nafuu niliyokuwa naisaka. Nikakubali.

Tukielekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam mazungumzo yetu yaligusia masuala mbalimbali. Aliniambia: “Tajiri aliyebaki Tanzania ni mmoja tu, Rais John Magufuli.”

Nilipomuomba afafanue akasema ni yeye peke yake ndiye anayetoa pesa kwa ajili ya masuala mbalimbali: reli ya standard gauge yeye, kununua ndege mpya za Shirika la Ndege la Tanzania yeye, na hata kuwapa zawadi ya viwanja Taifa Stars kwa kufuzu fainali za AFCON nchini Misri, ni yeye pia.

Nilitua Dar siku chache baada ya Taifa Stars kuifunga Uganda Cranes 3-0 na kufanikiwa baada ya miaka 39 kuingia kwenye fainali za michuano ya timu za taifa za Bara la Afrika.

Nilitaka kuendeleza mada ya utajiri wa Rais Magufuli nikikumbushwa makosa ya uandishi wa habari wa zama hizi ambao hauko makini sana kufafanua vema kati ya uamuzi wa serikali wa kuwekeza au kutumia pesa katika eneo fulani, na kutofautisha na uamuzi wa Rais Magufuli kutoa mchango wake binafsi kwa ajili ya suala fulani.

Uamuzi huo wa aina mbili unaunganishwa kuwa kitu kimoja, ingawa hakuna athari yoyote ya wazi, unajenga taswira isiyo sahihi juu ya taasisi ya urais na kiongozi anayeongoza taasisi hiyo kwa wakati huo. Haitakuwa ajabu kuwepo watoto wanaoamini kuwa njia moja ya kuwa tajiri ni kuwa rais. Lakini si tatizo la uongozi wa juu tu. Ni tatizo ambalo lipo katika kila ngazi ya uongozi.

Hata hivyo nilivutiwa zaidi na mazungumzo aliyoendeleza juu ya Taifa Stars na mechi ile waliyocheza na timu ya taifa ya Uganda.

Aliniambia kuwa wafuatiliaji wengi walishangaa sana Taifa Stars kuifunga Uganda. Aliniuliza: “Wewe yale magoli tuliyofunga uliyaona?”

Nilimwambia kuwa sikuitazama mechi. Akasema tukubaliane kuwa muamuzi alituhurumia goli la pili alipotoa adhabu ya penalti. Lakini goli la kwanza na la tatu si magoli ambayo mlinda mlango mwenye uzoefu anaweza kufungwa.

Kwenye chati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni Uganda inashika nafasi ya 80, wakati Tanzania inashika nafasi ya 131.

Taifa Stars ilipoifunga Uganda Cranes, Machi 24, 2019 Uganda ilikuwa tayari imefuzu kushiriki mechi za fainali za AFCON zilizoanza Cairo Juni 21, Uganda ikiongoza Kundi ‘A’ kwa alama 13. Kwa ufupi, Uganda haikuhitaji hata kucheza ile mechi.

Baada ya Rais Magufuli, mazungumzo yakahamia kwa Rais Yoweri Museveni. Taarifa ambazo dereva wangu alinipa ni kuwa kabla ya mechi ya Uganda Cranes dhidi ya Taifa Stars, maagizo yalikuwa yametolewa na Rais Museveni kwa timu yake ya taifa kuiachia Tanzania ishinde.

Nami nikaelewa kuwa ni kwa mantiki hiyo tu ndiyo unaweza ukakubali kuwa timu iliyoongoza kwenye kundi lake inaweza kupoteza ile mechi ya Dar es Salaam kwa magoli mengi kiasi kile bila majibu.

Tangu kuondolewa Idi Amin madarakani kwa msaada wa Tanzania, historia ya uhusiano kati ya Tanzania na Uganda ni nzuri kwa kiasi kikubwa. Ofisa mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, inayopakana na Uganda, alinisimulia kuwa kuna wakati walikamata ng’ombe kutoka Uganda ambao mchungaji alisema ni mali ya Rais Museveni. Haikuchukua muda walipata simu kutoka Ikulu, Dar es Salaam wakielekezwa kuwarudisha wale ng’ombe mara moja.

Katika mazingira ya aina hii hatuwezi kushangaa sana Rais Museveni kuagiza kuiachia Taifa Stars kushinda mchuano ule wa mwezi Machi.

Tutakachoshangaa ni iwapo Rais Museveni atarudia maelekezo hayohayo iwapo Uganda na Tanzania watakutana kwenye michuano inayoendelea Cairo. Alipowaaga Cranes aliwaambia wapeleke Kombe la AFCON nchini Uganda.

Kwa Tanzania na kwa Taifa Stars, ujumbe ni mmoja tu: Cairo ni mapambano mtindo mmoja na wale tunaowaamini ni rafiki zetu si marafiki tena. Na sisi pia tuiombee Taifa Stars mafanikio na kuleta kombe nyumbani.