“Nina uwezo mkubwa mno wa kuyafanya maisha yawe ya uchungu au ya furaha. Nina uwezo wa kuwa chombo cha maumivu makali au chombo cha kuvutia, naweza kunyanyasa au kutia hamasa, kuumiza au kuponya. Kama tukiwatendea watu kadiri walivyo, tunawafanya wanakuwa wabaya zaidi. Kama tukiwatendea watu kama wanavyopaswa wawe tunawasaidia kuwa namna wanavyoweza kuwa.”
Wolfgang Von Goethe.
Kila mmoja wetu ameitwa kuwa mponyaji wa majeraha ya wengine licha ya kwamba yeye mwenyewe anayo majeraha yake. Binadamu wote tunayo majeraha ya kihisia, kiakili, kiroho, kimwili, kiuchumi na kifamilia. Inawezekana una majeraha ya kusalitiwa na mwenzi wako wa maisha.
Inawezekana una majeraha ya kufiwa na mwenzi wako wa maisha. Inawezekana una majeraha ya kuishiwa mtaji wa kibiashara. Inawezekana una majeraha ya kiuchumi. Majeraha ni mengi. Nafasi hainiruhusu kuyataja yote. Itoshe kusema kuwa makala hii ina nia ya kuyaponya majeraha yako ya kihisia, kiuchumi, kifamilia, kiafya na kiroho. Kila mwisho wa kitu au hali fulani huleta mwanzo mpya. Ninakualika usafiri pamoja nami katika makala hii inayolenga kukutia moyo, kukufundisha, kukufariji na kukuimarisha.
Unapoamua kufanya mambo makubwa katika maisha yako, ni lazima uwe tayari kukabiliana na watu ambao wamejipanga kuyashambulia malengo yako (vision attackers). Hawa ni watu ambao wameamua, wamedhamiria na wako tayari kukukwamisha na kukushambulia kwa namna yoyote ile. Na lengo lao ni moja tu, ‘usifanikiwe’.
Kuna aina mbili za watu wa aina hii. Kwanza, ni wakimya [silent attackers]. Hawa wanakushambulia kimya kimya. Hawataki ufahamu kwamba wao ni maadui zako. Hawa wanakuonyesha uso uliojaa tabasamu, lakini moyoni wanakusimanga.
Aina ya pili ni watu walio wazi. Hawa wanajipambanua wazi kwamba ni maadui zako. Wanakushambua wazi wazi. Kanuni ya mafanikio inasema: “Ni lazima ukutane na watu wa aina hii.” Watu wa aina hii hawakwepeki. Ni muhimu sana kumwomba Mungu kila wakati ili akufunulie nia ya ndani ya mioyo ya watu wanaokuzunguka.
Dunia imejaa watu wasiowatakia wenzao mema. Wapo watu ambao wakiona unafanikiwa wanaumia. Wapo watu ambao wanatamani kukuona ukihangaika usiku na mchana. Wapo watu ambao wakiona mnaelewana vizuri na mke au mume wako wanaumia.
Furaha yao ni kwamba, watamani kuona hamuelewani ndani ya ndoa yenu. Wapo watu ambao wakiona mnaelewana na wafanyakazi wenzako wanaumia. Wapo watu ambao wanapenda wakuone ukiendelea kuishi kwenye nyumba za kupanga. Hawapendi kuona ukipata pesa wala kupata mafanikio ya aina yoyote. Naomba kukufundisha jambo la busara hapa. Watu wa aina hii wapo. Tunaishi nao.
Wengine ni ndugu zetu wa damu. Wengine ni majirani zetu. Wengine ni wafanyakazi wenzetu. Wengine ni marafiki zetu. Wengine tunasali nao kanisa moja. Nisikilize hapa, usiwachukie watu wa aina hii. Ukiwachukia utakuwa unawapa upenyo wa kukudhoofisha katika utafutaji, upendo, hisia na kiuchumi.
Wapende watu hawa. Waombee kwa Mungu watu hawa. Siku zote wema una ushinda ubaya. Acha wa kuonyeshe ubaya, lakini kwa upande wako waonyeshe wema. Usitumie nguvu nyingi kuwachukia. Tumia nguvu nyingi kuwasogeza mbele ya kiti cha rehema cha Mungu. Watapigana nawe kwa namna nyingi lakini watashindwa. Wewe ni mshindi.
Watu wengi tumejeruhiwa katika maisha yetu. Tunayo majeraha mengi. Naomba kukunong’oneza jambo hili: ‘Mwenyezi Mungu anakupenda sana’. Ni kweli, kuna watu katika maisha yao wamejeruhiwa kiroho, kimwili, kiakili, kiuchumi, kiuhusiano na kiuongozi. Wamejeruhiwa. Wamejeruhiwa. Pole kwa kujeruhiwa. Usihuzunike. Usiogope. Usisononeke. Kama umejeruhiwa na mke au mume wako, kumbuka ‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na mtoto wako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na rafiki yako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha.’ Kama umejeruhiwa na jirani yako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha.’ Kama umejeruhiwa na serikali yako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha.’ Kama umejeruhiwa na kiongozi wako wa kiroho, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha.’ Kama umejeruhiwa na mwajiri wako, kumbuka, ‘Mungu hajakuacha.’ Narudia kusisitiza kwa msisitizo uliojaa ukweli na hekima kwamba: ‘Mungu hajakukataa. Mungu hajakuacha. Mungu anakupenda sana.’