Natuma salamu nyingi sana kwako lakini najua inawezekana umekaa katika kiti na umeshika tama ukitafakari mambo yanavyokwenda, unaona mahali ambapo mambo yamekwama na kuna mteule wako yupo yupo, kama nakuona unampa muda wa kujitafakari ajue unataka nini lakini anashindwa, unamtumia meseji juu ya mambo yanavyokwenda lakini amekaa kimya au kuitisha kikao cha kujadili jambo ambalo wewe umeliona na ungedhani anapaswa kulitatua mara moja.

Pole, najua kuwa nawaza usichowaza, ni kweli, ninajua kwamba una mambo mengi sana katika kichwa chako, najua kwamba una ‘makwazo’ mengine ambayo hujaweka bayana lakini kwa sababu mimi ni mhenga naweza kusoma moyo wa mtu na kujua anagugumia na jambo lake moyoni na kushikwa maumivu.

Naweza nikasema najua unachowaza kidogo kwa mbali, unawaza sana wakati ukiomba kura miaka minne iliyopita na matarajio yako hayakuwa haya kama ambavyo yanaendelea, hukuwa na kina Magufuli wenzako ambao ungeshirikiana nao kupambana na zile ahadi ulizotoa  miaka minne iliyopita. Najua unawaza wale ambao wamekuangusha katika safu yako ya ushambuliaji ya maendeleo, inawezekana walikuwa ni kina Magufuli  mnaofanana sura na si tabia.

Una kipindi kingine na una mtihani mwingine wa kuwapata kina Magufuli wa tabia, si kufanana sura, ni kipindi ambacho unaweza kuichora vizuri ramani ya vita ya uchumi iwapo utawapata wanaoweza kukusaidia katika mapambano, tunajua ugumu wa mapambano ambayo yapo na kwa hakika wapo wengine ambao umewakabidhi silaha ya vita ya maendeleo, tunasikia tu mambo yakienda salama huko waliko, lakini wengine ni mpaka uache lindo lako uende kupigana katika lindo lao.

Dhamira yako inaweza ikawa inakutuma vingine na kuna watu wako hawaelewi unataka nini katika mipango ambayo mmejiwekea, katika hili nadhani wengi hawakukuelewa uliposema siasa zimekwisha na sasa tufanye kazi. Kwa ushauri wangu awamu ijayo jaribu kuachana na wanasiasa watakuchosha kabla hujachoka, wachungulie sana watendaji wako mioyoni na si nje kwa maana ya nguvu, elimu na uwajibikaji wa utumishi.

Kuna ombwe kubwa sana la utumishi katika ngazi ya uteuzi wako na kuwatumikia wananchi, na hawa ndio wanaotakiwa kuipeleka dhamira yako kwa wananchi waliokuchagua na ambao hawakukuchagua, wengi wamekuwa na ndimi nyingi na utendaji ni mdogo, wengi wamekuwa wanasiasa na utendaji wanawaachia walio chini yao, najua huu mtihani ni mgumu kumjua nani ni nani mpaka uwe naye.

Katika awamu yako hii umeona namna ambavyo umekumbana na baadhi ya wateule waliokushinda japokuwa wakati ukiwateua uliamini watakusaidia, nakupongeza kwa sababu hukufikiria kama kuna gharama ya uadui na chuki, hukufikiria kuna kupoteza marafiki au kura, uliamua kupambana kuwatafuta wengine na kuwatoa wale ambao hawakufikia vigezo vyako.

Naamini wenye nia ya dhati wapo, lakini wamefichwa na vivuli vya waovu, pindua meza angalia chini yupo nani, na akusaidie wapi, waovu wengi watakuzingira ili usiwaone kina Magufuli wengine ambao ukiunganisha timu, basi malengo yanatimia, sitaki kusema kwamba sasa hivi unajua mambo mengi sana kupitia wasaidizi wako, lakini niseme kwamba una taarifa nyingi tofauti na miaka minne iliyopita.

Kuna watu wanapigwa vita sana kiasi cha kukushawishi uachane nao na wala usiwateue au usiwatumie, hao ndio miti yenye matunda, wapo waliopigwa mpaka wakaanguka, huwezi kuwaona tena, hayo ni matokeo ya michezo ya siasa na utumishi, hiyo ni michezo ya baadhi ya wakubwa kutotaka kuwaona wa chini wakifanya kazi kama ambavyo wewe ungependa iwe.

Endelea kujipanga lakini upigaji bado upo sana, lazima ujue kila mahali palioza, unajitahidi kusafisha kutoa uvundo lakini bado harufu za rushwa, wizi, ubinafsi, unyanyasaji vinatamalaki kwa mbali, umeanza kusafisha dari, endelea kushuka ukifika uvunguni utashangaa, lakini uvunguni hauwezi kufika wewe mwenyewe, ni lazima uwe na kina Magufuli wengi kila mahali.

Mheshimiwa Rais, watu wamekosa amani kwa mambo mengi, wapo waliokosa kwa kupotoshwa na kusingiziwa, kiufupi wamenyanyaswa kwa kupindisha kauli zako, miti mingi imepopolewa, imeumizwa, imeteswa, na bado wanaendelea kuteseka, huko mbele tutafutie wenye nia njema.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.