Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, hongera kwa kazi nzuri; siwezi kukupa pole kwani kazi ni kipimo cha utu na wewe unakitekeleza ipasavyo.

Mheshimiwa Rais, nakuandikia barua hii kwa masikitiko makubwa baada ya wewe kuwa msikivu na kutaka Watanzania wenzako wapate Katiba mpya, lakini hata hivyo, Mheshimiwa Rais, kuna baadhi ya Watanzania wanayumbisha mpango huu mzuri unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.

Mheshimiwa Rais, kabla ya wewe kuruhusu suala la mchakato wa Katiba mpya, wananchi walipiga kelele wakitaka Katiba mpya lakini wewe ukawa msikivu na kuruhusu mchakato wa Katiba mpya.

Mheshimiwa Rais, nakuandikia barua hii na kukushauri usilivuje Bunge Maalum la Katiba kwa sababu wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wanaotoka nje, wamekata tamaa na hawana hoja wakiwa ndani ya bunge hilo.

Kwa sababu kama wana hoja kwanini wasikae bungeni ili waendelee kushindana kwa nguvu ya hoja. Lakini cha ajabu wao wanatoka, hivyo kuwasaliti wenzao waliowatuma kuwawakilisha bungeni.

Mheshimiwa Rais, ninakuomba ukatae kuona na kusikia baadhi ya watu kuwadhihaki waasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume kwani hawawatendei haki waasisi hao wa Taifa letu.

Kama wana hoja warejee bungeni na kushiriki majadiliano ili mwisho wa siku pande zote zifikie maridhiano yenye tija kwa Watanzania.

Kasumba ya baadhi ya watu kuwadhalilisha waasisi wa Taifa letu isiruhusiwe kabisa, kwani ni hatari kwa mustakabali wa Tanzania. Kama saini zilizopo kwenye Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Tanzania) ndizo zilizowekwa na waasisi wa Muungano huo, wapinzani wanataka za aina gani tena?

Wapinzani waling’ang’ania suala la kutooneshwa hati, hati zimeonekana sasa wanaleta vikwazo vingine!

Mheshimiwa Rais, ninakuomba usiendelee kuwavumilia watu wanaodhalilisha waasisi wa Taifa letu kwani ni dhahiri hawautakii mema umma wa Watanzania. Ninakutakia kila la kheri katika ujenzi wa Taifa letu la Tanzania.

Mgingi Mhochi (Anko),

S.L.P. 1384,

Musoma, Mara.

0759 278 509 au 0787 245 429