Kwa wiki kadhaa, Gazeti JAMHURI tumekuwa tukiandika taarifa tulizozifanyia uchunguzi wa kina zikiihusu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Mhusika kwenye sakata hili ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande, pamoja na viongozi wengine katika Mamlaka hiyo, Wizara ya Uchukuzi na sehemu nyingine.
Hatuna sababu ya kurejea tulichoandika kwa kuwa ni imani yetu kuwa wasomaji wameweza kuujua ukweli na uchungu mzito uliofichika ndani ya TPA, ambayo ni mali ya umma.
Tumeshupalia suala hili si kwa sababu nyingine, bali ni kwa kutambua dhima yetu kama chombo cha habari, juu ya kuwaeleza ukweli wananchi ili watambue namna fedha zao zinavyofujwa na genge la wateule wachache.
Tunayaandika haya tukitambua hatari inayotukabili, lakini kwa kuwa tumedhamiria kulisaidia Taifa letu kupitia taaluma hii, tumejikuta hatuna namna nyingine, isipokuwa kutekeleza wajibu huo ambao tunaamini ni wajibu halali kabisa.
Wakati tukiendelea kuanika ufisadi na ubabe wa kutisha ndani na nje ya TPA, Mkurugenzi Mkuu, Kipande, pamoja na wapambe wake kadhaa wanajitahidi kutaka kuonesha kuwa maovu mengi yanayofanywa, ukiwamo ufujaji wa mabilioni ya shilingi, una baraka za Rais Jakaya Kikwete! Tunamuomba Mkurugenzi Mkuu pamoja na wafuasi wake wote, waache kabisa kumhusisha Rais katika madhambi haya ambayo ni wao wenyewe walioyaunda.
Tunaweza kutofautiana na Rais Kikwete katika masuala mengine, lakini kamwe hatutakubali kuona jina la Rais aliyechaguliwa kwa ridhaa ya Watanzania, anatumiwa na kundi la watuhumiwa wa uhujumu uchumi na ufisadi kama ngao yao.
Rais Kikwete ameliongoza Taifa hili wakati ambao kuna mambo mengi mno. Anakabiliwa na changamoto za kutekeleza ahadi zake na za chama chake kwa wananchi, anakabiliwa na maandalizi ya kuwa na Katiba Mpya; anahangaika kuboresha mishahara na huduma mbalimbali za kijamii. Haya na mengine, tunaamini yanamtosha kabisa.
Kwa sababu hiyo, tunamuomba Kipande atambue kuwa uongozi wake mbovu, si mbovu kwa sababu ya mtu mwingine yeyote, bali ni yeye mwenyewe. Anastahili kukabiliana na yote mabovu aliyoyafanya kwa sababu hakutumwa na Rais Kikwete.
Tena basi, kama ambavyo amenukuliwa akisema, asithubutu kufanya makosa akidhani atakuwa na ngao ya ukaribu wake wa kieneo na Rais Kikwete. Rais Kikwete tunayemfahamu hana ubia na wanaotumia vibaya madaraka yao.
Tumeshuhudia namna alivyokataa kubariki uamuzi tata wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wa kuwang’oa wakurugenzi wawili. Kipande asivurunde akadhani Rais Kikwete atamuacha salama.
Haya tunayoyasema kwa Kipande tunayasema kwa wengine wote wanaotumia vibaya jina la Rais Kikwete na viongozi wengine kama ngao kwa dhambi zao. Tunaomba jamii kwa ujumla wake iendelee kutuunga mkono ili hatimaye tuweze kuiokoa TPA ambayo sasa imegeuzwa shamba la bibi.