*Aagiza wataalamu wafungue mpaka wa Bologonja

*Watalii kutoka Kenya wataingia kiulaini Serengeti

*Watafaidi vivutio, kisha fedha zote zitaishia Kenya

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameshakamilisha mipango ya kufungua mpaka wa Bologonja; jambo linalotajwa kuwa ni pigo kwa uchumi wa Taifa na kwa wadau wa tasnia ya utalii nchini.

Mpaka huo unaotenganisha Tanzania na Kenya, ulifungwa mwaka 1977 kwa amri ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kuzingatia maslahi mapana ya kiuchumi na kimazingira ya Taifa.

Taarifa zilizopatikana kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii zinasema tayari Nyalandu ameshawaagiza viongozi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wengine katika Wizara yake, kuhakikisha mpaka huo unafunguliwa.

Mkurugenzi  Mtendaji wa TTB, Aloyce Nzuki, ambaye Nyalandu amemwondoa kwenye nafasi hiyo, anatajwa kuwa mmoja wa watu waliopinga mpango huo kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake. Upinzani huo unatajwa kuwa miongoni mwa sababu alizotumia Nyalandu kushinikiza Nzuki aondolewe.

Endapo mpango huo utafanikiwa hiyo ina maana watalii kutoka katika Mbuga ya Maasai Mara, wataingia katika Hifadhi ya Taifa ya  Serengeti na kisha kurejea Kenya huku wakiiacha Tanzania na Watanzania wakiwa hawafaidi lolote la maana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, licha ya urafiki wake wa dhati na Nyalandu, anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi wanaopinga kufunguliwa kwa Bologonja. Hata hivyo, watu walio karibu na viongozi hao wanasema zimeandaliwa hoja maridhawa za kuwalainisha watu mbalimbali, wakiwamo wabunge ili waunge mkono kufunguliwa kwa mpaka huo.

Hata hivyo, mmoja wa maofisa katika Wizara ya Maliasili na Utalii aliyezungumza na JAMHURI, ameuita mpango huo kuwa ni uhujumu uchumi usiostahili hata kutamkwa.

“Hatujui busara ya kiongozi huyu…anataka watalii waingie Tanzania kufaidi vivutio vyetu, wajisaidie huku, kisha warudishe fedha zote Kenya…hii ni disaster ya kiuchumi (maafa) kwa wadau wa utalii,” amesema.

Mwaka 1977, mpaka huo ulifungwa kutokana na uchunguzi uliothibitisha kwamba watalii kutoka Maasai Mara walikuwa wakiingia Serengeti, na wakati huo huo malipo yote ya malazi, vyakula na huduma nyingine vikifanyika upande wa Kenya. Tanzania ikabaki na jukumu la kuwaandalia Wakenya mahali pa wao kuingia na kuchuma fedha na kisha kurejea kwao wakiwa na watalii.

Akiwa Ujerumani kwenye maonesho ya utalii Machi, mwaka huu, Nyalandu alisema atahakikisha Bologonja inafunguliwa. Habari hizo zilipokewa kwa shangwe na Wakenya ambao kwa miaka mingi wanapambana bila mafanikio.

Mwaka 2009, Serikali ya Tanzania, kwa mara nyingine, ilizuia ufunguaji mpaka wa Bologonja.

Pamoja na hoja njema za kiuchumi, hoja nyingine ilikuwa kwamba kufunguliwa kwa mpaka huo kungehatarisha mazingira na huenda kuiua Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwani watalii wengi kutoka Kenya wangeitumia njia hiyo.

TTB wakati huo ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Peter Mwenguo, ilishikilia msimamo huo na kusema kwamba kwa sababu hizo mbili — za kiuchumi na kimazingira — kamwe isingekubaliana na mapendekezo au uamuzi wa kufunguliwa kwa mpaka huo.

Wakati huo TTB ilitoa taarifa kwa wanadiplomasia wote waliopo hapa nchini na nje ya nchi na kuwathibitishia kuwa hapakuwapo mpango wa kufunguliwa kwa mpaka huo. Pamoja nao, wengine waliopewa taarifa hiyo ni wawakilishi wa kampuni za utalii, waongoza watalii na mawakala wa safari za watalii.

Mwalimu aliifunga Bologonja baada ya kusambaratika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.

Chama cha Waongoza Watalii Kenya (KATO) kimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mpaka huo unafunguliwa.

Mwaka 2009, Ezekiel Maige, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema Serikali ya Tanzania haikuwa na dhamira yoyote ya kufungua mpaka huo, na kwamba msimamo huo ulikuwa ukijulikana kwa viongozi wa Kenya.

Aliyekuwa Waziri wa Utalii wa Kenya, Najib Balala, alilalamikia kufungwa kwa Bologonja, akisema uamuzi huo haukulenga kuijenga Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Mambo mengi kwenye tasnia ya utalii yamefanywa katika Jumuiya, lakini kusitasita kwa Tanzania — hasa kwenye masuala ya mipaka — kunasumbua,” alisema Waziri huyo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi.

Maige akajibu madai hayo kwa kusema: “Umuhimu wa ikolojia ya eneo hili ambalo ni sehemu ya Urithi wa Dunia, hauwezi kutolewa kafara kwa malengo ya kufupisha safari kati ya Maasai Mara na Serengeti, na hapa ni mapitio ya wanyama wanaohama wakati wa msimu wao.”

Kwa mujibu wa Makubaliano ya Ushirikiano katika Nyaja ya Utalii ya Arusha ya Novemba 16, 1983 yaliyotiwa saini na Tanzania na Kenya, kifungu cha X(b), watalii watasafiri ndani na nje ya kila nchi kupitia mipaka au miji iliyoainishwa.

Kwa mujibu wa TTB, maeneo yaliyoainishwa kwa ajili ya watalii kuingia na kutoka ni Namanga, Sirari-Isebania, Holili-Taveta, na Horohoro-Lungalunga.

 

Watanzania wapinga

Waongoza watalii nchini Tanzania, kwa upande wao wanapinga kufunguliwa kwa mpaka wa Bologonja, wakisema kufunguliwa kwake kutaua utalii hapa nchini.

Wanasema ukifunguliwa, mamia ya magari kutoka Kenya yataingia nchini yakiwa na watalii nyakati za asubuhi na kurejea Kenya jioni.

Hifadhi ya Serengeti yenye ukubwa wa kilomita za mraba 14,763; “ndiyo makao makuu” ya msafara wa nyumbu zaidi ya milioni moja na pundamilia zaidi ya 200,000 wanaosafiri kati ya hifadhi hiyo na Maasai Mara. Kati ya miezi 12, nyumbu huwapo Serengeti kwa kipindi kirefu cha miezi 10. Ndani ya hifadhi hiyo, kuna hoteli za kitalii zisizozidi 15, loji na kambi kadhaa. Hali hiyo imefikiwa kwa makusudi ili kuepuka wingi wa watalii ambao unaweza kuchangia uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wa Kenya, kuna hoteli na kambi za watalii zaidi ya 50 na loji tisa ndani ya Maasai Mara ambayo ukubwa wake ni kilomita za mraba 1,510 pekee.

Mwaka jana, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilieleza hofu yake juu ya kuongezeka kwa vitendo vya kibinadamu ndani ya Hifadhi ya Serengeti vilivyosababishwa na wingi wa vituo vya kuingia na kutoka hifadhini humo. Chanzo cha wingi huo kilielezwa ni idadi ya watalii na vitendo vya kibinadamu kwenye Hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya.

Wakenya bado wapambana wafunguliwe Bologonja

Machi, mwaka huu wasafirisha watalii kutoka Kenya walieleza kutoridhishwa na mkutano wa mawaziri wa utalii uliofanyika Arusha kwa vile hawakujadili na kufikia mwafaka wa kufunguliwa kwa Bologonja.

Waliokutana ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Biashara na Utalii kutoka Kenya, Phyllis Kandie; Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Lazaro Nyalandu; na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Utalii, Wanyamapori na Mambo ya Kale wa Uganda, Agnes Egunyu Akiror.

Madai ya Wakenya ni kwamba kufungwa kwa mpaka huo kunawafanya wasafiri kwa magari kwa saa tano kutoka Maasai Mara kupitia Sirari (Tanzania) na hatimaye kuingia Serengeti.

Wanasema kufungwa kwa Bologonja kuna sababu za kisiasa, lakini Serikali ya Tanzania imekuwa ikisisitiza kwamba hatua hiyo ina lengo la kulinda mazingira na ajira za wananchi wake.

Wakenya hao wanasema urefu wa safari huwafanya wakati mwingine kulazimika kuendesha magari na kulala Nairobi kabla ya kuendelea na safari ya kwenda Arusha kupitia Namanga siku ya pili na kwenda Serengeti.

Wadau wa utalii katika nchi hiyo wanasema kufunguliwa kwa Bologonja kutawasaidia kupunguza gharama na muda wanaotumia kusafiri kutoka Maasai Mara, Kenya na Serengeti nchini Tanzania.

Watangulizi wote wa Nyalandu walipinga utetezi huo wa Wakenya kwa hoja zile zile za kulinda ajira za Watanzania na kulinda mazingira ya Serengeti ambayo ni moja ya maeneo ya Urithi wa Dunia.

Kaskazini mwa Serengeti kuna vivutio sita vya watalii ambavyo vinasifika duniani kote. Vivutio hivyo ni Lobo Valley, Upper Grumeti Woodlands, Mara River, Lamai Triangle, Wogakuria na Bologonja Springs.