*Lakodi kina mama ili wawapekue watuhumiwa

 

Kituo cha Polisi Mbuguni, Arumeru Mashariki mkoani Arusha, kinalazimika kukodi wanawake wanaoishi jirani na kituo hicho ili kuwafanyia upekuzi watuhumiwa wanawake kabla ya kuwaweka mahabusu.

 

Kukodiwa kwa kina mama majirani kunatokana na kituo hicho kukosa askari polisi wanawake.

 

Hayo yamesema na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Rebecca Mngodo (Chadema).

 

Silima amesema kukosekana kwa wanawake katika kituo hicho kumetokana na mazingira ya kazi na kutokuwapo nyumba.

 

Amenukuu Kanuni za Kudumu (PGO) Namba 353 ambayo inasema askari wa kike wasipelekwe mahali au katika kituo cha kazi kisizokuwa na nyumba za uhakika za kuwawezesha kuishi.

 

Akijibu swali la msingi, Silima alikiri kuwa Kituo cha Polisi Mbuguni hakina askari polisi wa kike.

 

“Hii inatokana na upungufu wa askari wa jinsia hiyo na mazingira yanayozingatiwa wakati wa kuwapangia kazi. Pamoja na ukosefu huo, kazi zinazohitaji mazingatio ya kijinsia hufanywa kwa kutumia wanawake wengine katika eneo hilo kwa mujibu wa sheria na zinaendelea vizuri.

 

“Serikali inao mpango wa kukarabati kituo hicho na vyumba vya mahabusu ili view katika hadhi inayostahili na kuona uwezekano wa kujenga nyumba za askari na hatimaye kupeleka askari wa kike,” amesema.

 

Ametoa wito kwa wabunge kuwahamasisha wananchi na wadau wengine ili kujenga miundombinu katika vituo mbalimbali vya polisi nchini kote.

 

(TOLEO MAALUMU LA IJUMAA, JULAI 6, 2012)