Katika siku za karibuni, Jeshi la Polisi Tanzania limechukua hatua mbalimbali za kujisafisha mbele ya umma. Ni baada ya kubaini kwamba wananchi wengi walikuwa hawaridhiki na utendaji wa chombo hiki cha dola.
Tumeshuhudia na kusikia baadhi ya askari polisi waliobainika kukiuka maadili ya jeshi hili wakifukuzwa kazi na kushitakiwa. Katika hili, juhudi kubwa zimeonekana chini ya uongozi wa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu.
Waliomtangulia Mangu katika uongozi wa Jeshi la Polisi si kwamba hawakutekeleza majukumu yao vizuri, lakini huyu Mangu katika kipindi hiki kifupi baada ya kukabidhiwa wadhifa huo, amedhihirisha kwa vitendo dhamira yake ya kuliimarisha jeshi hilo katika maadili na utendaji uliotukuka.
Wengi wetu tunashuhudia namna nidhamu ya askari polisi inavyozidi kuongezeka wakati wa kuhudumia raia, tofauti na siku za nyuma ambapo askari wengi walitekeleza majukumu yao kwa ubabe na vitisho dhidi ya raia.
Hata hivyo, bado IGP Mangu anayo changamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa anadhibiti ubabaishaji na udhaifu mkubwa unaoendekezwa na baadhi ya askari polisi katika utendaji kazi wao. Hawa wasipodhibitiwa mapema watalirejesha Jeshi la Polisi lawamani!
Kwa mfano, kuna taarifa kwamba askari polisi wa kitengo cha usalama barabarani (trafiki) wa mjini Singida, wiki iliyopita walizuia kwa zaidi ya nusu saa basi la abiria, Super Sami, linalofanya safari zake kati ya Mwanza na Dar es Salaam.
Trafiki hao walidai kuwa walitumia kipimo maalum na kubaini kuwa basi hilo lilikuwa linakimbia kwa kasi inayofikia kilometa 105 kwa saa kinyume cha sheria za usalama barabarani.
Walipoulizwa sababu ya kuchelewa kuadhibu wahusika na kuliruhusu basi hilo kuendelea na safari ya Dar es Salaam, walijitetea eti walikuwa wanawasiliana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) iwaambie adhabu inayostahili kwa basi linalokimbia mwendo kasi kupita kawaida!
Katika hilo, binafsi nimeshangaa kusikia kwamba polisi, hususan trafiki waliandaa kosa (la kuzidisha mwendo) bila kuainisha adhabu yake. Ni jambo lisiloingia akilini!
Ninavyoamini, na bila shaka wengi wanaamini hivyo, ni kwamba kila kosa linalokiuka matumizi sahihi ya barabara lazima liliainishiwa adhabu yake. Ni ubabaishaji kama si udhaifu mkubwa kwa trafiki kusema kwamba walizuia basi la abiria kutokana na kosa ambalo hawajui adhabu yake.
Ni wazi kuwa sababu iliyotolewa na trafiki waliozuia basi la Super Sami, kwamba walichelewa kuliruhusu kwa kuwa walilazimika kuwasiliana na SUMATRA iwaelekeze adhabu stahiki, inazungukwa na taswira ya rushwa. Hali hii haistahili kuvumiliwa katika kipindi hiki ambacho uongozi wa Jeshi la Polisi umedhamiria kufanya mageuzi makubwa ya kujisafisha.
Lakini kwa upande mwingine, inaelezwa kwamba basi la Super Sami liliendelea kuandamwa zaidi na adha ya trafiki katika vituo vilivyofuata baada ya Singida mjini. Lilizuiwa katika kila kituo cha trafiki kwa muda wa kati ya dakika kumi na nusu saa, huku mabasi mengine mengi yakipita bila kuzuiwa.
Inaelezwa kwamba usumbufu uliongezeka zaidi pale trafiki walipozuia basi hilo mjini Dodoma kwa muda usiopungua saa moja. Hali hiyo iliwalazimu abiria kushuka na kuwashambulia trafiki husika kwa maneno makali wakilalamika kucheleweshwa safari ya Dar es Salaam.
Pamoja na mengine, abiria walilalamikia kitendo cha basi la Super Sami kuzuiwa kila kituo cha trafiki, badala ya trafiki kuwaadhibu kisheria dereva na kondakta husika iwapo walibainika kukiuka sheria za usalama barabarani. Kwamba utendaji huo wa trafiki ulikuwa unawaadhibu moja kwa moja abiria zaidi ya 50 waliokuwa wanatumia basi hilo.
Ingawa hatimaye basi hilo liliruhusiwa, lakini badala ya kuwasili Dar es Salaam muda wa kawaida, yaani kati ya saa 3:30 na 4:00 usiku, lilifika saa 7:00 usiku kutokana na adha ya kuzuiwa kwa muda mrefu katika kila kituo cha trafiki mkoani Singida na Dodoma.
Lakini baadaye imetafsiriwa kwamba usumbufu huo wa trafiki dhidi ya basi la Super Sami unazungukwa na hujuma ya kutaka kuliondoa barabarani, kwa kusababisha abiria walikimbie kutokana na kero ya kucheleweshwa safarini inayotokana na kuzuiwa katika vituo vya trafiki kwa muda mrefu.
Binafsi ninaamini kwamba bado ni mapema, IGP Mangu anaendelea kujipanga kwa kufuatilia ili kubaini vitendo vya askari wachache vinavyoshusha na kuchafua heshima ya Jeshi la Polisi mbele ya umma. Bila shaka atapokea hili ninalomtonya ili alifanyie kazi kwa uzito unaostahili.
Watanzania wanapenda kuona na kusikia juhudi za kulisafisha Jeshi la Polisi zinasonga mbele na kuzaa matunda yatakayodhihirisha wazi jukumu lake la kulinda usalama wa raia na mali zao.
Bila shaka IGP Mangu anaendelea kujipanga na hatafumbia macho udhaifu wa aina hiyo na mwingine wowote unaokitia doa chombo hiki cha dola. Mungu libariki Jeshi la Polisi.