Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahamoud Mgimwa, amesema kuwa sheria za kilimo zilizopo kwa sasa nchini ni za tangu ukoloni na hazina tija yoyote kwa mkulima wa kawaida, na kwamba kinyume chake sheria hizo humuumiza mkulima kwa kunufaisha watu wa tabaka la juu.
Mgimwa ameyasema hayo Februari 15, mwaka huu jijini Dodoma wakati akifunga mkutano mkuu wa tano wa wadau wa sekta ya kilimo hapa nchini, akizitolea mfano baadhi ya sheria ambazo serikali imezikuta kutoka kwa wakoloni kuwa ni pamoja na sheria ya Bodi ya Korosho, sheria ya Bodi ya Pamba na sheria ya Bodi ya Tumbaku.
“Sheria nyingi ukiangalia ni za kikoloni, hatujazitunga sisi. Kuna sheria ya Bodi ya Korosho, sheria ya Bodi ya Tumbaku pamoja na sheria ya Bodi ya Pamba…angalia hazikuwa zinamlinda mkulima bali mkoloni, kwa hiyo, tunahitaji kuwa na sheria yetu Watanzania, sheria zinatungwa nje ya Bunge na ndani ya Bunge, kwa hiyo anzeni mchakato, mkiona kuna ukakasi tunashirikiana ili mkulima wa chini anufaike na yeye,” anasema.
Kwa mujibu wa Mgimwa, mkulima wa chini amekuwa akihangaika kulima bila usaidizi wowote lakini unapofika wakati wa mavuno serikali imekuwa ikimwingilia na kumpangia namna ya kuuza au kutouza mazao yake kutokana na mfumo mbovu na kandamizi wa sheria zilizopo za tangu ukoloni.
“Mkulima anapokwenda kulima shamba hana mgogoro na mtu yeyote, aidha anakodi shamba au alime shamba lake lakini ikifika wakati wa kuvuna… anataka kuuza serikali inakuja kumwambia hakuna kuuza nje ya nchi, sawa si sawa? Kwa hiyo hakuna sheria yoyote inayomlinda mkulima zaidi ya kumnyonya na kumkandamiza, hivyo kuna mahitaji makubwa ya marekebisho ya sheria na wadau wa kwanza wa kuangalia mapendekezo ya sheria ni ninyi wadau na wataalamu wa kilimo pekee, sisi Bunge ni kupokea mapendekezo, kujadili na kutunga sheria,” anasema.
Katika hatua nyingine, Mgimwa amemtaka mwandaaji na mratibu wa kongamano hilo la wakulima, ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kilimo Tanzania, Profesa David Nyange, kuwa na utaratibu wa kuwashirikisha wakulima wa hali ya chini.
“Wataalamu mpo wengi sana kuliko hata watu waliokusudiwa…mkutano huu ungependeza ungekuwa na wakulima wengi, wavuvi wengi, pamoja na wafugaji. Lakini liangalieni nanyi watu wanaobadilishana mawazo si tunaowalenga,” anasema.
Kwa upande wake Profesa David Nyange anasema maazimio ya mkutano huo watayachambua zaidi na kuyafikisha katika sehemu husika huku mtaalamu mwingine wa masuala ya kilimo, ambaye kwa sasa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamzora, akisema kuwa Tanzania haiwezi kuondokana na umaskini kwa wakulima bila kuongeza tija.
Mkutano huo wa siku tatu ulihudhuriwa na wataalamu na viongozi mbalimbali wa asasi za kiraia na kiserikali, miongoni mwao ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Dk. Christopher Ishengoma na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Dk. Sizya Lugeye.