Siri nzito za mradi wa ujenzi wa kituo kikubwa cha mabasi ya kwenda mikoani eneo la Mbezi Luis zimevuja, zikavuruga watendaji na Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam, JAMHURI linathibitisha.
Baada ya wiki iliyopita gazeti hili kuandika habari za jinsi rushwa ilivyovuruga Baraza la Madiwani, uongozi wa Jiji la Dar es Salaam na watumishi wa umma, sasa wakubwa wamechachawa na puto linakaribia kupasuka.
Tayari wiki iliyopita Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeweka kambi pale Jiji la Dar es Salaam kubaini nini kinaendelea.
“Kwa kweli JAMHURI mnastahili pongezi. Baada ya ninyi kuandika habari hii, tumefahamu mengi. TAKUKURU wamekuja hapa wamewahoji wakubwa na sasa ukiacha kiburi cha kuzaliwa tu, watendaji wakuu wana wakati mgumu.
“Kamati ya Fedha imekutana Jumanne na Alhamisi (wiki iliyopita) imembana Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana na wasaidizi wake hadi kampuni waliyotaka kuibeba (jina linahifadhiwa) imeondolewa kwenye mchakato.
“Sheria iko wazi. Mzabuni akikosea katika zabuni unamwandikia na kumweleza upungufu wake, kisha unajadiliana naye kulingana na majibu aliyotoa, ikiwa upungufu unarekebishika, mnarekebisha zabuni inaendelea na kama haurekebishiki, basi mnamwondoa na kumjulisha sababu,” amesema mtoa habari wetu.
Mwingine akaliambia JAMHURI: “Kwa kweli ukiangalia kigezo kilichokuwa kimetumika kuiondoa Kampuni ya Group Six bila kuisikiliza na kuipatia kampuni ya (jina linahifadhiwa) bila kufuata taratibu za kisheria, huhitaji kuelezwa jinsi rushwa inavyofanya kazi. Madiwani wamesimamia misingi ya kisheria, kanuni na taratibu kuondoa utaratibu wa kihuni uliokuwa umefanywa.”
JAMHURI linafahamu kuwa Jumanne wiki iliyopita, Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilikutana, lakini kikao hakikufanyika kutokana na mkurugenzi na wataalamu wake kufika kikaoni bila nyaraka za kikao kilichopita.
“Sasa tuliwauliza, Yatokanayo iko wapi? Ikawa hawana. Tukawauliza, tunafanyaje kikao bila kujua kikao kilichopita tuliyoamua utekelezaji wake umekuwaje? Tukahoji, wanaficha nini? Katika hali hiyo ilibidi tuahirishe kikao hadi Alhamisi.
“Alhamisi ilipofika wakaja na hadithi zisizoeleweka. Wakaleta mapendekezo ya kampuni ambayo haikushinda mchakato wa zabuni ya (jina linahifadhiwa). Tukawauliza maswali yanayotokana na ‘tender document’, wakajiona wajinga. Kwa pamoja, ingawa mwenyekiti wa kikao alikuwa Mwana CCM mwenzetu, tukaona hatuwezi kuuza masilahi ya nchi kutetea masilahi binafsi ya uongozi wa Jiji,” amesema mmoja wa madiwani.
Diwani mwingine ameliambia JAMHURI: “Tumewauliza hiyo kampuni wanayotaka kuibeba wana masilahi gani nayo? Tukawambia mnakumbuka Mwenyekiti wetu wa chama, Rais [John] Magufuli aliishasema hii kampuni ni ya hovyo, imeshindwa kujenga daraja na barabara, sasa ninyi kwa nini mnaibeba?
“Wakasema wameichunguza haina matatizo. Tukawauliza mmewahoji kina nani kubaini haina matatizo? Wakasema wamepiga simu na wameunda timu iliyofuatilia ubora wa utendaji wa kampuni hii. Tukawauliza, Rais Magufuli mmemhoji kujua kwa nini alisema hii kampuni ni mbovu? Wakasema hapana.
“Waliposema hapana, tukawauliza kuwa kwa hiyo ninyi Jiji hammwamini Rais Magufuli ambaye ana vyombo vingi vinavyompa taarifa za kina hadi ninyi mpuuze kauli yake kuwa hii ni kampuni ya hovyo? Wakakaa kimya. Tukaiondoa, ila nasikia wanakwenda kuitetea PPRA.”
JAMHURI linazo taarifa za uhakika kuwa uogozi wa Jiji la Dar es Salaam umejipanga kupeleka utetezi wa kampuni hiyo iliyotajwa na Rais Magufuli kuwa ni mbovu iliyoondolewa na madiwani. “[jina linahifadhiwa) amemwambia meya kuwa anaamini PPRA watawaelewa Jiji na watairejesha kampuni hii iliyoondolewa,” ameongeza mtoa habari wetu.
Tuhuma nyingine zinaeleza kuwa mmoja wa wabunge amezungumza na kampuni hiyo iliyoondolewa akawaahidi kuwa angewakutanisha na Rais Magufuli. “Huyu [jina linahifadhiwa] wamemkatia Sh milioni 100 baada ya kuwapa ahadi hiyo na wakaenda katika hoteli ya [jina linahifadhiwa] wakafanya sherehe baada ya ahadi hiyo,” amesema mtoa habari wetu.
Mtu ambaye majina yake yanatajwa kuwa ni S. M. ndiye aliyemuunganisha B. A. M. kwenye hii kazi kwa ahadi ya kuwapeleka [jina linahifadhiwa] kwa rais waweze kupewa zabuni. Amewahakikishia kuwa atawapeleka kwa rais ndiyo maana amepewa hizo pesa.
Kiongozi mwingine mwandamizi mkoani Dar es Salaam, ametajwa kupewa donge nono la Sh milioni 100 aitetee kampuni hiyo ipate zabuni ya kujenga stendi hii. “Hata hivyo, huyu bwana [jina linahifadhiwa] amekuwa ‘smart’ sana. Hata ikifika wakati wa vikao anakwepa, haingii. Hata wakienda ofisi za mkoani anaogopa viongozi wenzake wasimwone, hivyo siku hizi amewafungia vioo baada ya kupata hilo ‘fuba’,” amesema mtoa taarifa.
Mkurugenzi wa Jiji naye wanamtuhumu kuwa si bure kwa jinsi anavyoitetea kampuni isiyo na sifa. “Huyu mkurugenzi amekuwa akikutana na kupata ushauri kutoka kwa Y. M. ambaye ndugu yake ni msimamizi wa mradi wa kampuni ya [jina linahifadhiwa] anayefahamika kwa jina la ‘Mrango’ na mmiliki wa Kampuni ya Dem,” amesema mtoa taarifa.
Kulingana na nyaraka ambazo JAMHURI limezipata, awali kampuni 17 ziliomba zabuni ya kujenga Stendi ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kati ya kampuni hizo, kampuni tatu ndizo zilichaguliwa katika hatua ya awali kwa nia ya kuzishindanisha kupata mshindi wa zabuni Na. LGA/018/2017/2018/W/10. Kampuni zote hizi tatu zilizochaguliwa katika hatua ya awali ni za Kichina, ambazo ni Group Six, Hainnan na CRJE.
Ripoti ya mapitio kwa zabuni zilizowasilishwa na kampuni hizo tatu, ndiyo inayoleta kizungumkuti. “Kampuni ya (jina linahifadhiwa) imekuwa na upungufu unaotia aibu. Kwa mfano haikuonyesha mchanganuo wa gharama, Dhamana ya Benki inaonyesha CRDB iliitoa Julai 23, mwaka 2017 ikiwa ni mwaka mmoja kabla zabuni haijatangazwa… na hii kampuni inapigiwa debe la kutisha,” amesema mtoa habari wetu na kuongeza kuwa hata hivyo CRDB imelifafanua hili na kuonyesha kuwa barua ya dhamana kuonyesha kuwa ilitolewa mwaka 2017 yalikuwa makosa ya kiuchapaji.
“Mtu aliyepewa Mamlaka ya Kisheria (Power of Attorney) kusaini nyaraka za zabuni za kampuni hii hakuzisaini, badala ya kugonga mhuri wa ofisi amegonga mhuri wa moto, alipaswa kuonyesha wakandarasi wasaidizi (sub contractors), lakini hakufanya hivyo. Upungufu wa hivyo hivyo upo kwa kampuni ya pili ya (jina linahifadhiwa). Tena hii ya pili Mamlaka ya Kisheria kwa kawaida yanapotolewa na kampuni huwa yanaelezwa kuwa mamlaka hayo yametolewa kwa yeyote anayehusika, wao kwa sababu wanazozijua wakaelekeza mamlaka hayo kwa Mkurugenzi wa Jiji, kitu ambacho ni kinyume cha sheria.
“Kampuni hii nayo imefanya maajabu ya mwaka, kwani Dhamana ya Mkopo imetolewa Julai 24, 2018, lakini inaonyesha dhamana hii iligongwa mhuri Julai 23, 2018 ikiwa ni siku moja kabla ya kutolewa dhamana yenyewe, jambo ambalo haliwezekani.
“Hii kampuni nyingine inayotajwa kuwa inabebwa na afisa anayepewa maelekezo ya mdomo na mkurugenzi inaelezwa kuwa imepatia kila kitu, ila kuna wasiwasi kuwa washirika waliwavujishia baadhi ya siri za matakwa ya zabuni mapema hivyo kwa kutumia rushwa wanapata ‘advantage’ dhidi ya washindani wao. Hii si haki,” kimesema chanzo chetu.
Awali mradi huu ilikuwa ugharimu Sh bilioni 50 zilizotolewa na serikali, lakini mzabuni wa kwanza akaonyesha kuwa kazi hiyo angeifanya kwa Sh 50,698,000,000.00 bila kuonyesha kama gharama hizo zina Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ndani yake au la.
Mkandarasi wa pili kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI limeziona na ambaye kitengo cha ununuzi kilipendekeza apewe kazi ingawa alikuwa na upungufu wa kuonyesha kuwa amepata barua ya dhamana mwaka mmoja kabla ya zabuni kutangazwa, anasema anaweza kuifanya kazi hii ya ujenzi wa stendi kwa Sh 56,999,007,862.00 bila VAT. Hii ina maana ukiongeza VAT gharama inaongezeka kwa asilimia 18.
Mkandarasi wa tatu ambaye anadaiwa kuwa ana gharama kubwa, na kwamba anabebwa na Mkurugenzi wa Jiji naye alitaka alipwe Sh 64,860,367,747.21 bila VAT. Zamu hii sasa hadithi imebadilika na mkandarasi anayetajwa kubebwa na mkurugenzi ni huyo aliyeshika nafasi ya pili, lakini alikwishatajwa na Rais Magufuli kuwa hana uwezo.
Hii ina maana kuwa gharama itaongezeka kwa Sh bilioni 11,674,866,194.49, hivyo kufanya gharama halisi ya mradi kuwa Sh 76,535,233,941.70, badala ya Sh bilioni 50 zilizotolewa na serikali ambazo awali zilitajwa kuwa zinatosha. Jiji linasema kiasi kinachopungua wataongeza fedha kutokana na mapato ya ndani.
Mkurugenzi wa Jiji acharuka
Wakati hayo yakitokea, baada ya Gazeti hili la Uchunguzi la JAMHURI kuchapisha habari za rushwa inavyosumbua katika mradi wa Ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Mikoani Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana, amewatuhumu wafanyakazi wa kitengo cha Ugavi na Ununuzi kuwa wamevujisha siri za ofisi.
Wiki iliyopita, Liana amewaandikia barua watumishi wa kitengo hicho na kuwapa siku saba kujieleza kwa nini wamevujisha taarifa za mchakato wa zabuni ambao ni siri kwa Gazeti la JAMHURI.
“Mnamo Desemba 04, 2018 siku ya Jumanne Gazeti la JAMHURI liliandika habari kuhusu mchakato wa zabuni namba LGA/018/20177/2018/W/10 ya ujenzi wa Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani cha Mbezi Luis, ambapo katika habari hizo kuliandikwa mchakato mzima wa zabuni hiyo zikiwamo taarifa zisizo sahihi ambazo zilikuwa na lengo la kuichafua taasisi mbele ya watu na habari za ndani kabisa ambazo kwa mtu wa nje ya ofisi asingeweza kuzitambua bila ya kupewa taarifa na mhusika wa ndani.
“Hivyo kutokana na habari hizo inaonekana wazi kuwa watumishi wa Kitengo cha Ugavi na Manunuzi wametoa taarifa hizo nje ya ofisi bila ya kuwa na kibali cha kufanya hivyo.
“Kitendo cha kutoa taarifa za ofisi nje ya taasisi ni kinyume na kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Kanuni ya 42, Jedwali la Kwanza, Sehemu A, Kifungu cha 9. Nanukuu …. ‘Disclosure of information in contravention of the National Security Act, 1970….’ mwisho wa kunukuu.
“Kwa barua hii, nakutaka kutoa maelezo kwa nini umetoa taarifa za ofisi nje ya ofisi bila ya kupata kibali kutoka kwa Afisa Masuuli, maelezo yako niyapate ndani ya siku 07 kutoka tarehe ya kupokea barua hii. Nakala ya gazeti hilo imeambatanishwa.
“Sipora J. Liana, Mkurugenzi wa Jiji, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.”
Msomaji atahadharisha
Msomaji wa JAMHURI ambaye amepata kushika nyadhifa nzito serikalini ikiwamo uwaziri na ukuu wa mkoa, ametahadharisha kuhusu Mkurugenzi Sipora: “Huyu mkurugenzi mwanzoni sisi tulikuwa hatumfahamu kuwa ana matatizo ya asili na wafanyakazi. Akiwa Mkuranga, DC alilazimika kuandika barua ya kujiuzulu kutokana na matendo yake.
“Akiwa Tabora, madiwani walimfukuza. Akiwa Arusha aligombana na Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo hadi rais akaona bora amhamishe Mulongo. Hapa Dar es Salaam, alitoa tuhuma hewa dhidi ya wabunge wakakamatwa na TAKUKURU, kesi ikapelekwa Kisutu, uchunguzi ukabainisha kuwa hakuna kesi ya kujibu.
“Rais Magufuli anaweza kumwona ni mtendaji bora, ila ajipe muda achunguze utendaji wake. Ajiulize kwa nini kila anapokwenda miradi inakwama. Amuulize mradi wa Stendi Mkuranga uliishia wapi na kama ulikamilika. Amuulize kwa nini kila anapokwenda madiwani wanamfukuza.
“Rais asipoangalia, akamsikiliza huyu mkurugenzi bila kufanya uchambuzi, basi ajue atafukuza kazi watendaji wazuri na atakuja kubaini akiwa hana nafasi ya kurekebisha hali hii,” amesema.
Msomaji mwingine aliyekuwa kwenye Tume ya Charles Keenja, amezungumza kwa kina na JAMHURI, akasema yeye anaufurahia utendaji wa Sipora, ila anachofahamu Jiji halina uwezo wa kujenga mradi mkubwa kama huu.
“Mradi huu uhamishwe mara moja na kupelekwa Tanroads. Hizi fedha za walipakodi zinakwenda kuteketea chini ya uongozi huu wa Jiji la Dar es Salaam. Hawa waachiwe mengine lakini si ujenzi wa stendi hii kubwa na ya kisasa. Tangu Tume ya Keenja imeondoka hakuna mradi wowote waliofanya hawa watu wa Jiji hadi sasa. Hii ni hatari kwa nchi,” amesema msomaji wetu.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na JAMHURI wamesema ni aibu kuona Jiji lina mivutano ya ni mkandarasi yupi ajenge stendi wakati stendi hiyo ikihitajika kwa udi na uvumba. “Hii shida yote inatokana na usiri katika mikataba. Ingekuwa zabuni zinatangazwa, zinafunguliwa na mchakato unaanikwa kwa wananchi kutambua kipi kimo na kipi hakimo, basi wananchi wangepata huduma haraka. Usiri unatoa mianya ya rushwa, uachwe,” amesema mmoja wa wananchi.
JAMHURI limefanya mahojiano na Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana, aliyesema: “Anayenituhumu naomba apeleke malalamiko yake TAKUKURU. Huu mchakato ni siri, na bado upo katika hatua za ndani siwezi kuuzungumzia. Naona watu wenye masilahi binafsi wanahaha wanapoona wanayoyataka hayatekelezeki. Namshukuru Rais [John] Magufuli kwa kuendelea kusimama na sisi tunaotetea haki. Sitaruhusu mambo ya hovyo katika mradi huu. Katika hili sina hofu yoyote kwa maana sijachukua hata senti tano ya mtu, hivyo ninyi chapisheni tu gazetini.”