Sehemu ya kwanza, mwandishi wa makala hii alieleza namna wakoloni walivyoleta elimu kwa ajili ya kuwapumbaza Waafrika na kuwafanya wapuuze asili yao. Alieleza namna mkurugenzi wa kwanza wa elimu aliyeitwa Stanley River-Smith alivyokuja mwaka 1920 na kusimamamia utekelezaji wa sera hiyi kwa Waafrika nchini Tanganyika. Endelea…

Kuanzia pale Waafrika wasomi walipachikwa kasumba za ubora na uzuri wa mambo ya Wazungu tu, yale ya mila na utamaduni wetu yakaitwa ya kishenzi.

Hapa mnaona huyu River Smith anasema elimu ya juu imtoe mtoto kutoka mazingira yake ya kijijini (uproot them) na kumpandikiza (transplant them) maisha ya mijini ambako ataajiriwa na kuwa wakala au kibaraka (agents) wa ukoloni na utawala wake.

Matokeo yake ndiyo hayo baadhi ya wasomi wa vyuo vikuu kukosoa kila lifanywalo na viongozi wanachi na kusema mbona Ulaya/Marekani haya hayafanyiki? Demokrasia gani hii. Mbona hakuna mwongozo (katiba) wa nchi? Tunajitawalaje bila ya mwongozo (katiba).

Ukiwauliza iko wapi katiba ya Uingereza? (Hapo wanakuona wewe hukusoma!) Uingereza mpaka leo hii hawana KATIBA iliyoandikwa, bali wana mapokeo tu waliyorithi. Wanachorithi kutoka kwa mababu wa mababu zao – kihistoria kinaitwa “Retold History”. Lakini sisi bado tunawahusudu Waingereza hawa.

Niliposoma baadhi ya magazeti yamekiri kuwa wasomi wanamwona Rais Magufuli “Ni Fahari ya Tanzania” mkisema sasa Watanzania tumeanza kuona thamani ya UTAIFA NA UZALENDO. Bila ya kupenda taifa lako wewe ni kibaraka tu maana huna kwenu unakoweza kujivunia. Taifa bila lugha na utamaduni wake asili inakuwa kama ndege aliyenyolewa manyoya hapo nyama ya ndege haioneshi aina yake kama kunguru au njiwa!

Basi, suala hili la lugha ya Kiswahili tulione ni la muhimu sana. Ni kitambulisho cha Utanzania wetu. Wageni waje vyuo vikuu vyetu na wajifunze lugha yetu ya Kiswahili kwanza ndipo wafuate masomo yao. Je hili litawezekanaje iwapo lugha ya kufundishia vyuoni ni hiyo ya kigeni, KIINGEREZA? No way!

Kiswahili cha siku hizi ni kile cha mitaani tu. Waingereza wanaita “colloquial language”. Kule Uingereza lugha kama hizo zipo. Lakini wasomi wanatumia lugha fasaha wanaita “Queen’s English” ambayo sisi tulipokuwa shuleni miaka ile ya ukoloni, walimu wetu Waingereza, walituambia tunafunzwa “King’s English” kwa kutumia vitabu vile vilivyojulikana kama Oxford Reader Books – (book I- book VI)

Basi, kwa upande wa lugha ya Kiswahili tulifundishwa nahau safi ya Kiswahili kutoka katika kitabu kilichoitwa Sarufi ya Kiswahili By Broomfield. Hapa nitoe mifano michache ya Kiswahili kibovu cha siku hizi. Kwenye redio utasikia mwendo wa “masaa mawili”. Mimi nijuavyo “SAA” niclass au daraja la 4 ambalo kuna maneno yenye umoja na wingi namna ile ile.

Mathalani, maneno “SAA”umoja ni “saa”, na wingi wake ni “saa” vilevile. Saa moja, saa mbili, saa kumi. Hakuna kitu kama masaa.

Neno jingine ni nyumba. Umoja na wingi wake ni nyumba vilevile. Hivyo tuna saa 1 tunasema saa hii. Wingi wake tunasema saa hizi. Wingi unaonekana katika ile ajeto yake tu (kiarifa. Samaki mmoja au samaki wengi. Maneno ya daraja la kwanza kama mtu ambapo wingi wake unawekewa herufi wa na kuwa watu.

Neno mti wingi wake ni miti, daraja la pili neno mnyama wingi wake ni wanyama. Neno kama chura wingi wake tunaweka herufi “v”inakuwa vyura au kioo wingi wake ni vioo na kadhalika.

Maneno ya daraja la tano ni yale yanayo onesha ukubwa, mathalani – jumba hili – majumba haya. Jiwe hili, mawe haya, jengo hili, majengo haya.

Jamani sina nia ya kufundisha Kiswahili sanifu, bali ninaonesha umuhimu aliotuonesha rais wetu wa kutumia lugha yetu ya taifa, lakini tuitumie kwa ufasaha tusikivunje vunje kama vile majirani zetu wanavyoongea.

Kule utawasikia wakisema hii “mitu” ya Tanzania inaongea Swahili ya Pwani. Sasa Kiswahili sanifu mtu na wingi wake ni “watu” wala siyo ”mitu”.

Nchi za Bara la Afrika zimepitisha Kiswahili katika vikao vyao kule Addis Ababa, Ethiopia.

Ni wazi kuna utofauti wa matamko katika kila lugha. Kiswahili kikitamkwa na mtu wa mwambao – Mzaramo au Mwarabu ni tofauti na kile kinachotamkwa na Mngoni wa Songea au Mhaya wa Kagera. Hii iko hata katika Kiingereza.

Lafudhi ya lugha inatokana na makabila yetu. Mathalani, kule Kagera wana shida kutamka “f” wao wanatamka “fw”. Kwa mfano wanasema “mfwano” au wahehe hawana  “sh” wao wana “s”; mathalani “kushoto” wao wanasema “kusoto”. Mkurya hana “sh” yeye ana “ch” mfano kushoto yeye anatamka ”kuchoto”.

Hayo ni baadhi ya matamshi kulingana na lafudhi ya makabila. Wasukuma na Wanyamwezi wao wanapenda kukazia matamshi yao kwa kutia herufi ya namna hii – nilisemaga badala ya kusema nilishasema.

Pamoja na wasomi kadhaa kumchambua Rais wetu Dk. Magufuli kwa miaka yake mitatu ya utawala katika ujumla wao karibu wote wamekubaliana na alichokisema pale Mlimani katika ukumbi wa Nkrumah kwenye mdahalo ule. Ninaweza kusema kwa uhakika kuwa siku ile ya Novemba Mosi, Rais Magufuli alibadilisha hali ya hewa ya wasomi wa Mlimani na aliwateka na wakakubali.

Enzi za utawala wa Warumi alitokea Caesar Gaius Julius (100 – 44 BC tazama Encyclopedia Britannica uk. 1575) kushinda vita (civil war) na inasemekana alivuka mstari (crossed the rubicon) na kuteka Italia. Basi, inasemekana kwa furaha ya ushindi ule (mwaka 44BC) ndipo akajigamba kwa maneno haya “VENI, VIDI, VICI” – ikiwa na maana ya nilifika, mliona na, nilishinda!

Mimi kwa mantiki ya Mrumi yule Caesar Julius ninapenda kumalizia hongera zangu hizi kwa kumsemea Rais Dk. John Joseph Pombe Magufuli kule kufika tu pale Nkrumah, ninasema “VENI, VIDI, VICI” yaani alifika aliona na aliteka ule umma wa pale chuoni.

Heko Rais Magufuli kwa uzalendo wako.

MUNGU IBARIKI TANZANIA