Ujumbe wa watu watano kutoka Loliondo, Tanzania na nchini Kenya, upo nchini Uingereza kuchangisha fedha za kuendesha harakati za kupinga mpango wa serikali wa kutenga eneo la hifadhi ndani ya Pori Tengefu la Lolindo.
Hivi karibuni Gazeti la JAMHURI liliandika kuhusu safari ya Watanzania kadhaa nchini Uingereza wakilenga kupata fedha za kuendeshea harakati za kupinga mpango huo wa uhifadhi.
Watu hao watatu walipita Namanga kabla ya kwenda kupanda ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Wametambuliwa kuwa ni Samwel Naingirya, Diwani wa Ololosokwan; Yanik Ndoinyo na Shomet Naigisa. Wamekwenda kama wawakilishi wa asasi (NGO) ya TEST iliyosajiliwa nchini Kenya.
TEST inafanya kazi zake Kaskazini mwa Tanzania na sehemu chache za Kenya katika County ya Narok, lengo likiwa kujenga mshikamano kwa ajili ya kulinda ‘ardhi ya Wamasai’ bila kujali mipaka ya kimataifa.
Lengo la mkutano huo ni kutafuta fedha kutoka kwa NGOs na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na utetezi wa ardhi ya wenyeji.
Nangirya anawakilisha Oltoilo le Maa, ambao shughuli zao ziko katika Msitu wa Enguserosambu, Kata ya Orgosorok ambako wanaendesha miradi ya uhifadhi na utalii.
Mpango mkakati wa safari hiyo ni maandalizi ya kupinga mpango wa serikali wa kutenga eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 1,500 kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji, ushoroba (mapito ya wanyama) na eneo la mazalia ya nyumbu na wanyamapori wengine. Ziara hiyo itawawezesha, pamoja na wadau wengine, kukutana na kufanya mazungumzo na asasi ya Avaaz ambayo imekuwa mstari wa mbele kupinga mipango mingi ya Serikali ya Tanzania kwa eneo la Loliondo.
Ukiacha suala la uhifadhi, asasi hiyo imesimama kidete kupinga ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu (Arusha) – Makutano (Mara) inayolenga kupunguza adha kwa Watanzania wanaoishi eneo hilo na kukuza uchumi wa taifa.
Naingisa yeye anakwenda kama mwakilishi wa jamii mwenye ujuzi mbalimbali kuhusu miradi ya maendeleo na maendeleo ya jamii. Alikusudiwa kuwasilisha mada yenye kuhamasisha kuungwa mkono juhudi za kupinga wawekezaji ‘wasiowataka’ Loliondo, lakini pia kukaribisha wawekezaji kwenye usindikaji wa nyama na ngozi. Amekwenda kwa kivuli cha uwakilishi wa jamii kupitia TEST na Oltoilo le Maa.
Wakati huo huo, hali ya uhifadhi katika Pori Tengefu la Loliondo inazidi kudorora baada ya kuwapo matukio mengi ya kuingiza mifugo pamoja na ujangili.
Katika Kitongoji cha Karkamoru kilichoanzishwa jirani na kambi ya Kampuni ya mwekezaji OBC, kumeripotiwa mauaji ya twiga wanane ndani ya miezi miwili. Taarifa za vyombo vya usalama katika eneo hilo zinasema watu kadhaa wamekamatwa wakituhumiwa kuwahifadhi majangili.
Mauaji ya twiga yameongezeka siku za karibuni kutokana na mahitaji ya uboho wa wanyamapori hao unaodaiwa kutumiwa na kina mama waliojifungua ili kuwaongezea maziwa. Hakuna taarifa za kitaalamu zinazothibitisha madai hayo.
“Kumeuawa twiga wanane kwa miezi hii miwili, bahati mbaya majangili wanashirikiana na wenyewe ambao mwanzo tuliamini ni wahifadhi. Hali imebadilika.
“Watu wengi wameanza kujenga maboma yao tena karibu na mpaka wa Hifadhi ya Serengeti wakihamasishwa na NGOs kwa madai kuwa mahakama imezuia wasiondolewe hadi kesi ya msingi waliyofungua Mahakama ya Afrika Mashariki itakapokwisha. Sasa ni vurugu,” amesema mmoja wa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Inaelezwa kuwa hali imekuwa tete kutokana na baadhi ya NGOs kupita katika vijiji kuhamasisha wananchi kutoondoka eneo la uhifadhi, kwa kile wanachoambiwa kuwa eneo hilo ni mali yao.
Hivi karibuni Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangalla, amekaririwa akisema serikali iko kwenye hatua za mwisho za kutenga eneo la uhifadhi ili kulinda ushoroba, mazalia ya wanyamapori na vyanzo vya maji. Asilimia 50 ya maji yanayotumika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti vyanzo vyake ni Loliondo.
Serikali inakusudia kurekebisha sheria ili eneo litakalotengwa lilindwe kisheria; na inapendekezwa liwe chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ambayo licha ya kuwa na rasilimali za kutosha, kiikolojia ni eneo moja.
Kuna mapendekezo yasiyo rasmi kuwa endapo sheria hiyo itapitishwa, NCAA itaanza kwa kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro (vijiji 14 vya eneo husika) Sh bilioni 4.5 kila mwaka. Kiasi hicho kinatarajiwa kuongezeka kadiri mapato yatakavyokua. Fedha hizo ni sehemu ya mapato yatakayotokana na wawekezaji katika eneo hilo.
Hata hivyo, licha ya ahadi hiyo ya mapato makubwa kwa halmashauri, baadhi ya NGOs na washirika wao wanapinga mpango huo. Inaelezwa kuwa wao wanachotaka ni kuanzishwa kwa Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA), jambo ambalo linaungwa mkono na Mbunge wa Ngorongoro na Naibu Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Ufundi, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha; na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Taarifa za ndani zinaonyesha kuwa kuanzishwa kwa WMA kutakuwa na manufaa makubwa kwa wanasiasa ambao tayari wameihakikishia Kampuni ya Afrika Kusini ya AndBeyond kulitwaa eneo hilo. Tayari AndBeyond imekwisha kuanza ujenzi wa majengo ya kudumu katika eneo hilo la Kijiji cha Ololosokwan.
Tofauti na Sheria za Ardhi zinavyoagiza, Kampuni ya AndBeyond imeingia mkataba na Kijiji cha Ololosokwan wa kukodi ardhi yenye ukubwa wa ekari 25,000 kwa miaka 15. Kisheria, kijiji kinatakiwa kitoe kibali cha ukodishaji ardhi yenye ukubwa wa ekari 50 tu.
Hata hivyo eneo hilo ambalo limekodishwa kwa AndBeyond ni sehemu tu ndani ya eneo la Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,500. Serikali imekodisha eneo hilo kwa Kampuni ya OBC kwa utaratibu wa kuhuisha kibali kila baada ya miaka mitano.