Binadamu anaposhirikiana na binadamu wenzake katika kufanya kazi huwa hana budi kutimiza mambo matatu; wajibu, uwezo na kujituma. Anapotimiza haya hupata maendeleo yake na ya wenzake.
Hii ni moja ya taratibu za binadamu katika kufanya kazi. Watanzania hatuko nje ya utaratibu huu. Lakini baadhi yetu hatufuati mambo haya kwa sababu tunadhani au tunaamini kazi ni balaa, kazi ni utumwa, ilhali kazi ni baraka. Binadamu wema wanaishi kwa kufanya kazi iliyo halali.
Natambua maandiko ya dini zetu na simulizi za wahenga wetu zinaeleza kwamba kufanya kazi ni lazima, asiyefanya kazi asile. Kazi si balaa, kazi ni baraka kwa sababu uhai ni baraka na uhai ni kazi. “Mauti ni mwisho wa kazi. Kutamani kutofanya kazi ni kutamani mauti; yakija utajuta,” nukuu.
Nimenukuu maelezo haya ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuweka msisitizo katika mazungumzo yangu kuhusu Mtanzania anavyotakiwa kutambua kuheshimu na kuthamini kazi.
Kwenda kazini, kushinda kazini, kupapasa kazi au kufanya kazi kwa kipimo chako cha kuonekana unafanya kazi si kufanya kazi, bali ni kuchezea kazi. Kufanya kazi ni kutimiza mambo yafuatayo ambayo yatakupa heshima, sifa bora na kukuweka katika utu. Kwani kazi ni kipimo cha utu.
Kufanya kazi ina maana ya kuwajibika. Kuwajibika ni jambo linalomlazimu mtu kulitimiza. Mtu hana hiari nalo katika kulifanya. Kwake ni sharti, faradhi na jukumu. Asipokuwa na haya ndani ya nafsi yake bado hajafanya kazi.
Pili, uwezo. Hali ya kuweza kufanya kazi kwa kutumia maarifa, ubunifu na ujuzi katika madaraka yako kutimiza jambo ulitendalo. Elimu na utaalamu wako uvitumie kupata mafanikio. Wananchi wanahitaji mno maendeleo kupitia utendaji mzuri wa kazi yao. Maendeleo hayapatikani kwa kutofanya kazi.
Tatu, kujituma. Unapofanya kazi ujitolee kwa hiari bila kuamrishwa. Bidii ya kazi itoke ndani ya nafsi yako, akili na misuli ya mwili wako. Moyo wako ni kisuto cha wewe kutofanya kazi. Usiwe na moyo wa kupenda uvivu, uzembe na kulalama kwamba hali ya maisha ni ngumu na ‘vyuma vimekaza’, huo si utu ni ugoigoi.
Hapo ulipo jiulize na jipime. Unapofanya kazi yoyote mambo haya unayapa nafasi kutawala akili na viungo vyako vya mwili? Uvivu, uzembe na uzuzu ni maadui wakubwa dhidi ya kazi. Kiongozi na unayeongozwa yapimeni maneno haya na kuyatafutia tiba ‘ngunguri’ si ‘ngangari’.
Unapofanya kazi kwa maana halisi ya kazi, unakuwa mtu mpya kila siku katika akili, nguvu na afya njema. Unaleta maendeleo yako na ya wenzako. Usipofanya hivi unakuwa kama mzigo. Binadamu (Mtanzania) hastahili kuwa kama furushi la nguo linalonuka uvundo.
Tangu tupate uhuru wa nchi yetu sasa imetimu miaka 57, serikali zote za awamu tano zimezungumzia na zimehimiza kufanya kazi. Uhuru ni Kazi, Ruhusa Kufanya Kazi, Uwazi na Ukweli, Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya na Hapa Kazi Tu. Kipi kinakusibu Mtanzania kufanya kazi kwa tija?
Katika awamu zote hizi inatubidi kujitathmini tumefanya kazi au tumechekea kazi? Endapo tumefanya kazi, vipi sasa tunalalama? Nani ametuchekecha katika mustakabali wa kufanya kazi? Au nani ametuzuia kuwajibika, kuwa na uwezo na kujituma, hata tumsubiri waziri mkuu aje kutuwajibisha, kutupa uwezo na kujitumisha?
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutuambia Watanzania tujifunze kusoma wakati ni huu na tusikalie uchumi. Kazi ni kipimo cha utu.