Leo ni Siku ya Kimataifa ya Watoto. Kihistoria ni siku iliyoanza kuadhimishwa tangu karne ya 18, lakini sasa inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.

Ni siku inayopewa jina la watoto, lakini ukweli ni siku ya watu wazima kutafakari iwapo wanasimamia vyema jukumu lao la kulinda haki na maslahi ya watoto.

Katika hotuba aliyotoa Ikulu mwaka 1964 ikiwa imelengwa kwa watoto, Mwalimu Julius Nyerere aliwaambia watoto kuwa jukumu lake kama rais na lile la baraza lake la mawaziri ni kusimamia mipango itakayotunza nchi na rasilimali zake kwa ajili ya watoto, vizazi vijavyo, na vile vilivyopita. Alisema hawakukabidhiwa nchi ili waitumie hovyo hovyo.

Kwenye sera za elimu za wakati huo alisisitiza jukumu la serikali la kurithisha elimu na urithi wa utamaduni kwa watoto.

Jukumu la kwanza kabisa na muhimu la serikali la kutoa elimu bora kwa watoto bado halijabadilika tangu enzi hizo za Mwalimu.

Lakini jukumu la kulinda maslahi ya watoto haliwezi kuwa la serikali peke yake. Haihitaji utafiti wa kina kubaini kuwa haki za watoto hazizingatiwi kwenye jamii nyingi.

Mlolongo wa ukiukwaji wa haki za watoto utajaza vitabu vingi, lakini nitagusia masuala machache tu.

Tanzania, pamoja na nchi nyingine za Afrika, tunazo jamii zenye mila za kukeketa. Ni mila ambazo zisipotekelezwa zinamtenga msichana na jamii anamoishi. Anaonekana ni mwanajamii ambaye hajakamilika. Hawezi kuolewa. Na katika jamii ambako anaolewa hawezi kuzikwa kwenye eneo la makaburi ya familia yake.

Wapo watoto wanaoingizwa kwenye mapambano ya vita na kulazimishwa kuua. Haya matukio yametokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Liberia, na Sierra Leone.

Watu wazima ambao tunaamini wanaongozwa na mawazo ya kijinga – na hili hutokea Tanzania – wanaacha watu wa rika lao kuwatumbukiza watoto kwenye vitendo vya mapenzi kinyume cha sheria, na kinyume cha maadili. Ikumbukwe kuwa wahalifu hawa ni wanaume zaidi, na ni nadra kuwa wanawake.

Baadhi yao wanaweza kuwa wagonjwa wa akili, lakini inafahamika wapo wengine ambao wanafanya haya matendo kwa kuelekezwa na waganga wa kienyeji wakiamini watatajirika au kupata mafanikio maishani bila kuchapa kazi.

Kwenye nchi nyingine wapo watu wazima wanaotumia watoto kwenye biashara ya ngono.

Ni baadhi ya mifano inayoanika tabia ya kibinafsi ya watu wazima. Wanafanya hivyo kwa kuamua kuwa maisha ya sasa, maisha yao, ni muhimu kuliko maisha yanayofuata – yale ya watoto na wajukuu zao.

Lakini tunapozungumzia kulinda haki na maslahi ya watoto tukumbuke kuwa vipo vitendo na uamuzi mwingi ambao hauonekani kugusa maslahi ya watoto moja kwa moja, lakini hufanyika na kuathiri maslahi yao.

Matokeo hasi ya uharibifu wa mazingira yanaweza kuonekana mara moja, lakini zipo athari ambazo zitashuhudiwa na wajukuu zetu.

Ubadhirifu na wizi wa mali ya umma unachelewesha kukamilika kwa mipango na mikakati ya serikali kuboresha maisha ya Watanzania na kutuongezea gharama ya mipango hiyo. Ni gharama tunayowabebesha walipakodi wa baadaye.

Huwezi kujali maslahi ya watoto kama hufanyi kazi kwa bidii, na hasa iwapo umejaaliwa elimu, afya, na uadilifu. Kama ni mtumishi wa umma, kuacha kazi yako ikamilishwe na atakayeshika nafasi yako ni sawa na kuwabebesha walipakodi wa baadaye uvivu unaolipwa mshahara.

Kosa ambalo baadhi ya watu wazima hufanya ni kuamini kuwa alimradi wanatimiza wajibu wa kulinda maslahi ya watoto wanaowazaa na kuwalea, hawana haja ya kujizuia kufanya vitendo vinovyoathiri maslahi mapana ya jamii.

Kwa kuwa athari zote mbaya dhidi ya watoto husababishwa na watu wazima, haya matatizo yatapungua tu kwa uamuzi sahihi wa watu wazima. Lakini hilo halitatokea kwa urahisi kwa sababu ya ugumu wa kubadilisha tulichozoea.

Suluhisho la muda mrefu ni kutoa elimu kwa watoto inayomshawishi mtoto kukua na kuwa mtu mzima akiamini kwa dhati kuwa maslahi yake, ya watoto wake, na maslahi ya wenzake na watoto asiowazaa yanafungamana na maslahi ya jamii nzima leo na kwa vizazi vijavyo. Akue akipima kila uamuzi na uwezekano wa uamuzi huo kuathiri wengine.

Siyo kazi rahisi kutekeleza wazo hilo kwa sababu kila anapotizama, kila anaposikiliza, na kila anaponusa, mtoto anaandamwa na ujumbe unaoshabikia ubinafsi na jitihada za mtu mmoja mmoja za kujihakikishia mafanikio ya haraka haraka maishani.

Hata elimu nayo inaegemea kumwandaa mhitimu kuwa na uwezo wa kujiletea ahueni ya maisha kama kipaumbele muhimu kuliko vingine.

Tunachochea shauku ya mafanikio ya mara moja, mafanikio ya leo, siyo ya mwakani, na siyo ya vizazi vijavyo. Ni mazoea ambayo kwa kiasi fulani yanaisogeza leo kuwa kipaumbele cha maisha na siyo kesho.

Mafanikio ya kufikia maendeleo kwa taifa yanahitaji pia raia mmoja mmoja kujiwekea mikakati yake ya kujiletea maendeleo. Lakini maendeleo ya uhakika yanahitaji kila mmoja kuchukua tahadhari ili uamuzi wake usiathiri maslahi ya wengine.

Siku ya leo watu wazima tufanye tathmini ya maisha yetu na uamuzi tunaofanya ili kuuboresha uweze kulinda maslahi ya watoto wa leo na ya vizazi vijavyo.