Je, GMOs ni Sera ya Serikali?

Mheshimiwa Rais;

Kwa heshima na taadhima, niruhusu mimi mtoto wa mkulima mdogo na mwananchi wa nchi yetu tukufu nikusalimu. Hali yangu mimi na wanafamilia wenzangu, ambao ni wakulima wadogo nchini, si njema kabisa. Mheshimiwa Rais, kama ujuavyo, sisi ni takribani asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wote, na naamini kuna ndugu zako wa damu ambao ni sehemu ya jamii hii ya Watanzania.

Ukulima mdogo ndiyo uhalisia wetu. Hatuwezi kuukataa kwa sasa, japo wengi tuna matumaini ya kupiga hatua, kama Serikali itatuwekea misingi thabiti. Lakini hali yetu ni ile Waswahili wanasema ‘bora ya jana kuliko leo.’ Mikakati ya kumkwamua mkulima mdogo nitaieleza katika kitabu changu, lakini kwa leo niruhusu tu nikuulize swali la kisera.

Mheshimiwa Rais, Septemba 28, 2018 jijini Geneva, Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilipitisha Azimio la Haki za Wakulima Wadogo. Azimio hili ni ushindi kwa wakulima wadogo duniani dhidi ya makampuni hodhi katika sekta ya kilimo katika mapambano yaliyochukua miaka zaidi ya 17. Azimio hili linazungumzia haki za ARDHI, MBEGU, BAIOANUAI (Biodiversity) na SOKO LA NDANI LISINAJISIWE NA BIDHAA KUTOKA NJE.

Kimsingi, haki hizi zinaendana na Uhuru wa Chakula (Food Sovereignty) kwa nchi maskini, ambao ndiyo uhuru pekee tuliobaki nao. Kinachonishangaza Mheshimiwa Rais ni kuwa, pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wakulima wadogo nchini, Tanzania haikuwakilishwa katika Azimio hili muhimu. Nchi 34 zilikubali Azimio, nchi 11 zilikaa pembeni (abstain) na kama ilivyotarajiwa, nchi zilizoendelea zilipinga Azimio hili. Mheshimiwa Rais, tulipitwa au hatujali? Namshukuru Mungu wa wanyonge Azimio limepita.

Lakini Mheshimiwa Rais, mienendo ya Serikali inatupa shaka kubwa zaidi sisi familia ya wakulima wadogo. Naliongea hili kwa ujasiri kwa kuwa nimekulia kilimo na naishi na wakulima wadogo. Hata utafiti wangu wa uzamivu uliwalenga wakulima wadogo na unahusu Uhuru wa Chakula Tanzania.

Mheshimiwa Rais, Serikali imekuwa ikipigia chapuo teknolojia ya uhandisijini wa mazao ya GMOs nchini. Tumeliona hilo katika Programu ya ASDP II uliyoizindua hivi karibuni, ambayo inatamka wazi mwelekeo wa kilimo chetu kwa matumizi ya GMOs, siyo tu katika mimea, bali hata wanyama (ikanifanya niwaze majaliwa ya ng’ombe wa rafiki zangu Wamasai). Angalau basi tukusikie kwa maneno yako, je, wewe ni shabiki wa teknolojia hiyo na kwamba ni mdau wa mradi ya GMOs katika utafiti unaoendelea Makutupora, ambayo sasa inahalalishwa hapa nchini kupitia vyombo vya habari?

Barua yafaa iwe fupi ili isomeke kwa haraka na kueleweka kirahisi. Hivyo, Mheshimiwa Rais, nitaandika kwa uchache kuhusu sababu kwa nini Tanzania haihitaji GMOs. Lakini ninazo makala ndefu za kitaaluma zinazohusu jambo hili.

Sababu mojawapo ya kukataliwa GMOs inatokana na athari zake katika mazingira. Kwa mfano, katika utafiti uliofanywa na Mwanazuoni John Paul na kuchapishwa mwaka huu wa 2018, ikiwa na kichwa: Genetically Modified Organisms (GMOs) as Invasive Species unaonesha kuwa GMOs ni viumbe vamizi. Huharibu mazao asilia, mimea mingine, wanyama na kuleta athari katika mazingira ya viumbe hai.

Hata katika elimu ndogo ya kilimo tuliyojifunza sekondari, Mheshimiwa Rais, mahindi huzaa kwa uchavushaji. Kama mahindi ya GMOs na ya kawaida yatapandwa pamoja tutarajie nini? Kimsingi mahindi ya mbegu zisizo za GMOs yakiingiliana na ya GMOs yatapotea na kutuletea balaa kubwa la utegemezi huko mbele. Izingatiwe kuwa mbegu za GMOs hazirudiwi kupandwa zikatoa mazao.

Mheshimiwa Rais, napenda kujua kama hayo majaribio ya Makutupora yanajibu wasiwasi huu. Kwamba mbegu zao za GMOs hazitaathiri mbegu zetu, mimea mingine na mazingira kwa ujumla! Au ni utafiti unaoonesha tu kuwa GMOs zitastawi nchini? Mheshimiwa Rais unisamehe kwa kusema hili, hata bangi, ule mmea tunaoupiga vita, bado unastawi katika nchi yetu tukufu, tena vizuri mno.

Kupotea kwa mbegu zetu [kutokana na kuingiliana na mbegu za GMOs] kutatufanya tuwe watumwa wa makampuni ya mbegu. Mheshimiwa Rais, naamini umefuatilia habari kuhusu kampuni ya Monsanto, ambayo sasa imenunuliwa na kampuni ya Bayer ya Ujerumani kwa zaidi ya Sh trilioni 120 (USD 62 bn). Monsanto imekuwa ikipigwa vita hasa Amerika ya Kusini kwa namna ilivyotaka kuwafanya watu wake watumwa wa chakula. Pale ambapo tutapoteza mbegu zetu za asili, au tulizoziendeleza muda mrefu kupitia taasisi zetu za utafiti, tutakuwa tumekubali kuwa mateka.

Mheshimiwa Rais, wewe umekuwa ukipinga ubeberu kwa nguvu zako zote, na nisingependa hili la utumwa wa mbegu litokee katika utawala wako. Afrika Kusini, ambako waliruhusu GMOs tangu miaka ya 1990, sasa zaidi ya asilimia 90 ya mahindi ni GMOs na wakulima wanalazimika kulipa ziada ya ada ya teknolojia kwa Monsanto. Pamoja na kubeparisha kilimo chao, bado Afrika Kusini hawajaweza kutokomeza njaa.

Suala la utamaduni wa chakula ni muhimu pia liongelewe katika muktadha huu. Kuna ladha, harufu nzuri na uasili wa chakula. Kama ujuavyo, Mheshimiwa Rais, hizi ni sifa pekee zinazotofautisha chakula chetu. Na tunapaswa kuvitunza vyakula hivi kwa choyo kubwa – hasa kwa kuwa sisi ni kitovu cha utalii Afrika.

Tukisoma baadhi ya makabrasha na shuhuda za wageni, tunaona watalii wanakizungumzia chakula chetu katika namna ya sifa ya pekee. Mheshimiwa Rais, pengine unakumbuka kuwa, mmoja kati ya watetezi wa GMOs, Robert Paarlberg aliwahi kusema mwaka 2009 kuwa: “Chakula kilichozalishwa kiasili (organically) kina ladha na harufu ya kuvutia zaidi kuliko vyakula vya GMOs ndiyo maana nchi za Ulaya hazitaki GMOs «lakini»maskini wa Afrika hawapaswi kuwa na uchaguzi” Je, ni kweli tumefika sehemu ambayo hatupaswi kuwa na uchaguzi kwa kuwa sisi ni maskini?

Mheshimiwa Rais, katika makala yenye kichwa No Scientific Consensus on GMO Safety iliyochapisha na wanasayansi 15 kwa pamoja katika Jarida la Environmental Sciences Europe mwaka 2015, tunaelezwa kwamba japo kumekuwa na jitihada za kuuaminisha ulimwengu kuwa GMOs ni salama kwa afya, lakini kimsingi hakujawa na muafaka wa usalama wa GMOs. Na kuna baadhi ya tafiti zilizoenda mbele kueleza kuwa GMOs zina madhara kiafya. Baadhi ya madhara ya afya yanayotajwa ni pamoja na mzio na saratani. Je, utafiti unaofanyika Makutupora unalenga kuleta majibu ya wasiwasi wa madhara ya afya yatokanayo na GMOs?

Monsanto imeshtakiwa zaidi ya mara 50 huko Marekani na hivi karibuni ilipatikana na hatia, wananchi wakiilalamikia bidhaa zao kuwaleatea saratani. Kuhusu chakula cha GMO jibu la kampuni hiyo limekuwa hilo hilo kuwa hawalazimiki kisheria kuthibitisha kuwa vyakula vyao havina madhara. Wanaojiita wanasayansi wetu nchini hawatuambii ukweli, labda kwa maslahi yao binafsi. Lakini katika majadiliano tuliyofanya HakiArdhi hivi karibuni, mmoja wa wanasayansi hao, baada ya kubanwa na wakulima, alikiri kuwa uangalifu unahitajika hasa katika mimea iliyobadilishwa kuzalisha sumu ili kuua wadudu.

Mheshimiwa Rais, Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonesha kuwa Tanzania bado hatujafikia hata asilimia 30 ya matumizi ya mbegu bora, mbolea na viuatilifu. Bado tumekuwa tukizalisha zaidi ya asilimia 120 ya chakula kinachohitajika nchini. Wiki tatu zilizopita nilikuwa Mkoa wa Rukwa (Sumbawanga) na nilikutana na wazalishaji wanaolalamikia soko la mahindi na siyo changamoto za uzalishaji. Tena kuna waliovuna mahindi ya kutosha bila hata kutumia mbolea.

Lakini watu wa GMOs wanatuletea taarifa kuwa kuna uzalishaji mdogo sana na mahindi yanashambuliwa sana na wadudu. Kimsingi wanatangaza Hali ya Hatari (National Emergency) kwa jinsi wanavyotuonesha wadudu wala mahindi katika video zao.

Mheshimiwa Rais, ni kweli tumefikia huko? Kama ni kweli mbona hujatutangazia hali ya hatari ili basi GMOs tuipokee kama hatua yetu ya kupunguza kifo cha haraka? Na kama siyo kweli, kwa nini tunalazimishwa kuruka kutoka kutumia mbegu za asili kwa asilimia 80 za sasa hadi GMOs, teknolojia ya juu kabisa wakati hatujaweza kuvuna tija itokanayo na mbegu bora za OPVs na Hybrid?

Kuna agenda gani hapo? Tunakimbilia wapi? Tunapitwa na nini?

Mheshimiwa Rais, sipendi nikuchose sana. Naomba niulize swali moja la mwisho. Ubora tulio nao kama nchi ukilinganisha na nchi nyingine (Comparative Advantage) wanaouongelea wachumi au kile wasomi wa fani ya Biashara wanachokiiita eneo la ubora (niche) wetu lipo katika nini? Sidhani kama tunaweza kushindana na Marekani katika kuzalisha mahindi ya GMOs, chakula chenye unyanyapaa duniani kote. Sisi tunapaswa kuwa msingi wa chakula salama Afrika Mashariki na kwingineko duniani. Wakulima wetu wanapaswa kuwa msingi wa kuzalisha chakula hiki na kunufaika kama ilivyo sasa, ambapo soko bado si la uhakika.

Katika utafiti wangu nilitembelea vituo vya utafiti wa kilimo. Nikiri kuwa ni taasisi nyeti na zina wataalam (japo wametelekezwa) wanaoweza kutusaidia katika kuboresha mbegu zetu za asili kama wakiwezeshwa. Sote tunajua mbegu bora siyo lazima iwe ya GMOs.

Mheshimiwa Rais, tukumbuke kuwa wakati wa uongozi wa Rais Dk. Jakaya Kikwete, mradi wa GMOs wa WEMA haukuanza nchini japo ulipaswa kuanza 2008. Hii ilitokana na kifungu kinachohusiana na dhamana ya uharibifu kijulikanacho kwa Kiingereza kama ‘strict liability’ kilichopo katika kanuni zetu za usalama wa viumbe na uhai (Biosafety). Kifungu hiki kilisema mtu atakeyeingiza GMOs nchini atawajibika moja kwa moja kwa madhara yoyote yatakayotokana na GMOs kiafya, kimazingira na kiuchumi.

Hiki kifungu kiliwachelewesha watu hawa wa WEMA kuanza utafiti mpaka mwaka 2016 Serikali ilipolegeza masharti na kuweka kifungu kinachosema ‘strict liability’ haitatumika katika utafiti. Kama GMOs ni kitu chema kama WEMA wanavyodai na ni ukombozi wetu, waliogopa nini kuanza mwaka 2008 hadi wakashawishi kanuni zibadilike? Hata sasa wanadai sheria zetu zinawabana wanataka tulegeze zaidi watuletee balaa tushindwe pa kuwabana.

Walaji wa chakula kinacholimwa na wakulima wadogo hawapo salama pia. Muda si mrefu tutaanza kuona maduka makubwa (supermarkets) za vyakula vya asili (organic food) ambavyo watu wa kada ya juu tu ndio pekee watamudu kununua.  Wameshaanza na madogo madogo. Tunaendelea kutengeneza matabaka kwa maslahi ya mwekezaji.

Mheshimiwa Rais, huenda barua hii haitakupendeza. Najua pia barua hii haitawapendeza wadau na watunga sera wanaopigania GMOs izidi kutamalaki nchini. Hakika itaichukiza kampuni husika inayowekeza katika mradi wa WEMA huko Makutupora.

Wanatudhihaki kuwa sisi tunapinga sayansi. Lakini ni sayansi zipi tumezipinga hapa nchini? Kama alivyowahi kusema mwanazuoni nguli Karl Polanyi mwaka 1944, hatuwezi kuiruhusu teknolojia ya kinyonyaji na inayokusudia kunufaika na majanga ya watu itamalaki.

Mheshimiwa Rais, nakushukuru kwa kusoma hii barua. Hatimaye nimetimiza wajibu wangu. Nimesema ukweli na sina haja ya kujificha.

Mwandishi wa makala hii, Dk. Richard Mbunda, ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Anapatikana kwa simu: 0714 848685.