Mtu anaweza kukusababishia hasara katika namna nyingi na katika mazingira tofauti. Mathalani, mtu anaweza kukwangua gari lako, unaweza kumpa mtu kifaa kama pikipiki alete hesabu, badala yake si tu ukashindwa kupata pesa, bali pia na hicho kifaa akaharibu. Mwingine anaweza kukwambia lete mzigo ukafika sehemu husika akawa amepotea au akaukataa mzigo ilhali wewe umekwisha kuingia gharama za kuusafirisha nk. Mtu anaweza kukusababishia hasara nyingine yoyote.

Hasara yoyote ambayo mtu atakusababishia yafaa akufidie, isipokuwa kama umeamua kusamehe, au ilitoka katika mchakato ambao haukuwa halali kisheria. Katika ufafanuzi makala hii itajikita katika Sura ya 345, Sheria ya Mikataba.

1. Kukataa kukufidia

Yumkini yule aliyesababisha hasara anaweza kukataa kukulipa au kufidia kile alichosababisha. Ikiwa hili litatokea, basi yafaa umwandikie taarifa ya kumtaka kukufidia mara moja. Taarifa hii inapendeza zaidi akiandikiwa na wakili na kwa anuani yake wakili. Hata hivyo hata wewe mwenyewe waweza kuandika.

Taarifa itakuwa ikieleza kile alichotenda, hasara iliyosababishwa na hilo tendo lake, kumtaka afidie hiyo  hasara, siku au muda ambao unampa afidie hiyo hasara, na nini utafanya ikiwa atashindwa kufidia hiyo hasara ndani ya muda uliompa.

Kawaida unaweza kumpa siku 7, siku 14, siku 30, siku 45, au muda wowote kadiri unavyoona inafaa na kutosha. Na utaeleza pia kitu ambacho utafanya/hatua utakazochukua ikiwa atashindwa kukulipa. Kwa kawaida kitu cha kufanya  huwa ni kumfikisha mahakamani mhusika. Usije ukamdhuru au kufanya kitu kingine chochote ambacho hakimo katika utawala wa sheria.

Ikiwa kweli muda huo umekwisha na huyo mtu hajakufidia au kukuita katika mazungumzo, yafaa sasa kumfikisha mahakamani. Kumfikisha mahakamani ni kumlazimisha kufidia hasara aliyoisababisha. Na unapokuwa umemfikisha mahakamani, malipo yanaongezeka, kwa sababu gharama za kesi pia huingia.  Hivi ndivyo unavyoweza kumlazimisha aliyekataa.

2.  Kukubali kulipa fidia

Kukubali kupo kwa aina mbili. Kwanza, kukubali kwa maandishi kuwa nimesababisha hasara, kwa hiyo nitakulipa. Pili, kukubali tu kwa mdomo kuwa nimesababisha hasara hivyo nitakulipa. Kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba , makubaliano ya mdomo ambayo hayamo katika maandishi nayo ni mkataba halali kisheria.

Kwa hiyo iwe ameahidi kulipa hasara kwa maandishi au kwa mdomo, bado yote ni makubaliano na yanakubalika kisheria.  Lakini pia ile ahadi pekee ambayo huyu aliyesabababisha hasara ataitoa kwa yule aliyemsababishia hasara nayo  ni mkataba kamili kisheria. Ahadi tu, yaani ile kutamka tu kuwa nitakulipa au nitakufidia, tayari ule ni mkataba tosha na yafaa utekelezwe.

3.  Mambo ambayo yanatakiwa kufidiwa

Mambo haya ni kwa mujibu wa Kifungu cha 77 cha Sheria ya Mikataba. Kwanza, ni uharibifu wa aina yoyote ikiwa upo. Pili, ni gharama ambazo umetumia kuanzia unahangaika na huyo mtu mpaka kufikia mnakubaliana, pengine ulimtafuta, ulifungua kesi, ulitumia nauli, ulipiga simu na kila aina ya gharama ambayo uliingia anatakiwa kuilipa. Tatu, ni malipo mengine ambayo mtakubaliana, au yalikuwa yamekubaliwa katika ule mchakato wa mwanzo aliouharibu.

Hivi ndivyo unavyoweza kufidiwa hasara.