Miaka 14 imeshatimia tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipofariki dunia katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London, Uingereza, Oktoba 14, 1999.
Kwa muda wote huu tumeshuhudia mambo mengi — mazuri na mabaya — katika Taifa letu. Uwezo wa kiakili na uadilifu wa Mwalimu ni vitu vilivyomtofautisha na viongozi wengi wa Tanzania, Afrika na dunia kwa jumla.
Mbele ya mataifa, Watanzania wamekuwa watu wa kupigiwa mfano mzuri. Wameheshimika kutokana na moyo wa kuwapenda wenzao, kuwasaidia waliohitaji ukombozi, kuwatetea wanyonge, kudumisha amani, umoja na mshikamano, na kwa jumla kujali misingi ya utu wa binadamu.
Haya mambo hayakutokea kama bahati ya mtende kuota pasipo na maji. Wapo waliyoyatengeneza. Wapo wengi walioshiriki kuijenga sifa ya Tanzania chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere.
Mambo yote mazuri yaliyoachwa na waasisi wetu walioongozwa na Mwalimu, sasa yanatoweka. Inasikitisha, na kwa kweli inashangaza, kuona leo hii kwenye mitandao ya kijamii baadhi ya watu wakifurusha matusi na kejeli kwa Mwalimu kana kwamba kiongozi huyo si lolote, wala chochote katika ustawi wa Tanzania, Afrika na dunia.
Wakati Watanzania wakishindana kumtukana, walimwengu wameendelea kumtambua na kumheshimu. Mfano mzuri ni nchini Rwanda ambako kwa kawaida Oktoba 14 ni siku ya kumkumbuka Mwalimu. Si huko pekee, bali mataifa mengi ya Asia, Ulaya na hata Marekani, wanamkumbuka na kumuenzi Mwalimu kwa makongamano na kwa kupitia hazina kubwa ya maandiko na hotuba zake.
Chini ya misingi ya waasisi walioongozwa na Mwalimu, Tanzania ilikuwa nchi yenye umoja, mshikamano, upendo na udugu wa hali ya juu. Sifa hizo nzuri zinatoweka kwa kasi. Kumekuwapo matukio mengi ya ugomvi na mauaji miongoni mwa Watanzania, kumekuwapo matukio ya kutia aibu kama yale ya usafirishaji na uuzaji dawa za kulevya, ujangili, ujambazi na maovu mengine mengi.
Watanzania tumeanza kubaguana kwa misingi ya hali, rangi, kabila, dini, kanda, na kadhalika. Tunajitahidi sana kuuvunja Muungano ambao ndiyo muungano pekee katika Afrika.
Adui rushwa sasa ni sehemu ya maisha ya kawaida ya Watanzania. Rasilimali za Taifa ambazo chini ya Mwalimu zililindwa na kuwanufaisha Watanzania wote, sasa zinaliwa na wachache. Tumeukaribisha ubepari kwa jina tamu la “uwekezaji”. Wananchi wanapokwa ardhi yao. Wakulima wanahujumiwa kwenye pembejeo. Wafugaji hawana sehemu za kuendeshea shughuli zao. Madini yanachimbwa na faida kuishia Ulaya, Marekani na Canada. Hifadhi za Taifa zimevamiwa na majangili wanaoua wanyamapori kana kwamba hawana wenyewe.
Haya yote yanafanywa huku viongozi wengi wakiendeleza unafiki wa kudai “wanamuenzi Baba wa Taifa”. Nchi imeendelea kuwa haina miiko ya uongozi. Wenye vyeo ndiyo wanaogawana zabuni. Wenye madaraka ndiyo wanaoleta wawekezaji uchwara na kuongoza upokaji ardhi ya wananchi.
Miaka 14 baada ya kifo cha Mwalimu, sisi kama Taifa tunapaswa kujitafakari. Tuwe na mjadala wa kitaifa utakaotuwezesha kurejea kwenye misingi ya uzalendo na kuishi kama ndugu wa damu moja. Tumuenzi Mwalimu kwa kuhakikisha tunakuwa na Katiba inayokidhi mahitaji ya Watanzania wote, na si makundi ya wanasiasa.
Tuhakikishe wanafunzi wanapata elimu. Tuhakikishe tunalinda mazingira. Haya yote yalisimamiwa vyema na Mwalimu. Tunapaswa kumuenzi kwa vitendo, na si kwa porojo. Kupuuza mafundisho na maonyo ya Mwalimu ni kujitafutia laana ya kitaifa.