MWANZA

NA MWANDISHI WETU

 

Mkuu wa Shule ya Sekondari Igokelo, Hamisa Hassan, akifafanua jambo
kuhusu tatizo la mimba kwa wanafunzi shuleni hapo.

Wanafunzi 12 wa Sekondari ya Igokelo, Wilaya ya Misungwi mkoani
Mwanza, wamegundulika kuwa na ujauzito mwaka huu, hivyo kulazimika
kuwa kando na masomo yao.

Mimba hizo zimewalenga zaidi wanaosoma kidato cha kwanza, cha pili,
tatu na nne walio na umri chini ya miaka 18.

Mbali na na hayo, imegundulika pia baadhi ya wanafunzi wengine wa kike
shuleni hapo, wamekatishwa masomo yao kwa kuozwa na wazazi wao, ili
wajipatie mali.

Shule hiyo imetajwa na baadhi ya watu kuongoza kwa wanafunzi wake
kubeba ujauzito, wilayani Misungwi kuanzia Januari hadi sasa!

Uchunguzi wa JAMHURI unasema kuwa, kuanzia Januari hadi Juni mwaka
huu, wanafunzi watano walibainika kuwa na ujauzito, baada ya kupimwa
afya zao. Wengine saba waligundulika baadaye kati ya mwezi Julai na
Agosti,2018.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, wameliambia gazeti hili kuwa,
chanzo cha yote hayo ni baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo ya kutwa
kutembea umbali wa maili 10, kutoka nyumbani kwenda shuleni,
umasikini, tama za vijana na kutokuwa na elimu juu ya madhara ya
mahusiano ya kimapenzi ,wangali masononi.

Wameitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wazazi na walezi
kuwageuza watoto wao kuwa vitega uchumi, kuwaoza wangali masomoni ili
wapate mali, ukatili wa kijinsia pamoja na wanafunzi wenyewe kutokuwa
na uwezo wa masomo darasani.

UONGOZI WA SHULE

Mkuu wa Shule hiyo ya Sekondari Igokelo, Hamisa Hassan, amekiri kuwapo
kwa idadi hiyo ya wanafunzi wake waliopimwa na kubainika kuwa na
ujauzito. Anasema wengi wao wanasoma kidato cha kwanza.

“Tatizo ni kubwa sana. Kipindi cha mwaka 2018 changamoto kubwa ni
mimba hapa Igokelo. Watoto wengi waliopima tumewakuta wana mimba.

“Miongoni mwa watoto hao tuliowapima, watoto kama watatu wa kidato cha
tatu, kidato cha pili kama wawili na cha nne mmoja.

“Lakini, wengine wote wanakuwa ni kidato cha kwanza. Yaani mimba 12.
Mimba hizo tulikuwa tunazipima kwa awamu awamu. Kipindi cha kwanza
Januari mpaka mwezi wa sita, tulikuwa na mimba tano,” anasema Mkuu wa
Shule ya Sekondari Igokelo.

Anasema kipindi cha pili, walipeleka mtaalamu wa afya shuleni hapo kwa
ajili ya upimaji ujauzito, ambapo walibaini wanafunzi saba tayari
walikuwa wamenasa ujauzito.

Kwamba, ili kupambana na hali hiyo uongozi wake shuleni hapo
ukishirikiana na Shirika la Kivulini linalohusika na kuzuia ukatili wa
wanawake na watoto, wamekuwa ukitoa elimu kwa wanafunzi kuhusu elimu
ya madhara ya mimba za utotoni, pamoja na faida ya elimu katika maisha
yao.

“Kivulini wanasaidia sana kuzuia ukatili wa kijinsia na mimba za
utotoni. Tunawaeleza madhara ya kujiingiza wenye mahusiano ya
kimapenzi wakiwa na umri mdogo.

“Umuhimu wa kujilinda kama mabinti, kama wanafunzi. Lakini, ukiangalia
zaidi shida kubwa ipo kwa wazazi.

“Ugumu wa maisha wa familia unasababisha wazazi washindwe kuwapa
mahitaji mahususi vijana wao, kitu kinachopelekea wao vijana
kujiingiza katika mahusiano ili wapate mahitaji ya msingi,” anasema
Hassan.

“Igokelo wapo watoto wanatoka Wenzamiso kuja shuleni kilometa saba,
kuna mtoto anatoka Nyahiti, kuja Igokelo Sekondari ni kilometa sita na
pointi. Kuna mtoto anatoka Nyangaka, kutoka Nyangaka kuja Igokelo
Sekondari ni kilometa tano.”

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule, aliwataja vijana madereva wa
bodaboda (pikipiki) kuwa moja ya watu wanaowashawishi wanafunzi kwa
kuwapa lifti, waendapo shuleni asubuhi na wakati wa kurejea nyumbani.

Anasema Jografia ya shule hiyo yenye walimu 26, watoto wengi wanapita
kwenye mapori, punde waendapo shuleni na kurudi nyumbani jioni baada
ya masomo, kwani hiyo ndiyo shule pekee katika kata hiyo yenye vijiji
sita.

“Humo kwenye mapori wanakutana na vishawishi vingi, wengine wamepata
ujauzito kwa kubakwa!,” anasema Hassan, Mkuu wa Shule ya Igokelo
Sekondari.

Mwanafunzi mmoja aishie Kijiji cha Busolwa aliyekuwa akisoma skatika
huleni hiyo yenye upungufu wa walimu wanne wa hesabu, ametajwa kupata
ujauzito baada ya kubakwa porini, wakati akitoka shuleni.

Kulingana na hayo, vyombo vya dola wilayani Misungwi vinashauriwa
kuchukuwa hatua dhidi ya watu wanaowadhulumu kingono wanafunzi.

Jamii pia imeombwa kujitokeza mahakamani kwenda kutoa ushahidi kesi za
ukatili wa kijinsia, ubakaji na ulawiti wa watoto.

Aidha, JAMHURI imebaini baadhi ya wazazi na walezi hawafuatilii
mienendo ya watoto wao kielimu, kimaadili, hivyo ili kukomesha mimba
za utotoni, jamii iwe karibu zaidi na watoto wawapo nyumbani na
shuleni.

AOZWA

Mwanafunzi mmoja anayesoma kidato cha kwanza ‘B’ katika Shule hiyo ya
Igokelo, yenye upungufu wa walimu wanne wa somo la kemia (jina
linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 17, Septemba 19,2018, aliozwa na
baba yake mzazi, aitwaye Jackson Songoma.

Mzazi wa mwanafunzi huyo anayeishi Kijiji cha Mwajombo, anadaiwa
kupewa mahali ya ng’ombe watano, kisha kuruhusu mwanaye nayedaiwa kuwa
mtoro na mwenye uwezo hafifu darasani, aache masomo na kuanza
kuhudumia ndoa.

Mmoja wa washukiwa wa mkasa huo, Samuel Majige, alipohojiwa na gazeti
hili amekiri kushiriki sherehe ya kuozwa kwa binti huyo aliyezaliwa
Aprili 24,2001, maarufu kwa jina la ‘’Bukombe.’’

Vitendo hivyo vinakwenda kando na Sheria ya Mtoto nchini, Namba 21 ya
mwaka 2009, pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 1989 unaoangazia
haki za mtoto, ambapo Tanzania iliukubali mkataba huu Julai 10,1991.

Kipengele cha (ii) cha mkataba huo wa kimataifa, pamoja na mambo
mengine kinatamka mtoto anayo haki ya kupata elimu.

Halikadhalika, kipengele cha (iii) kinataka kulindwa na
wazazi/walezi/jamii au Serikali, dhidi ya madhara, huku Sheria ya
Mtoto ya mwaka 2009, sehemu ya (vii) inasema mtoto ana haki ya kupata
huduma bora za elimu, malazi matibabu kwa ajili ya ustawi wake.

Tayari watuhumiwa watano wameshakamatwa na Polisi Wilaya ya Misungwi,
kuhusu tukio hilo.

Ofisa Mtendaji Kata ya Igokelo, anayehudumu pia Tarafa ya Misungwi,
Lucas Bukundi, anathibitisha kuozwa kwa mwanafunzi huo.

Bukundi anaviomba vyombo vya dola kuchukuwa hatua dhidi ya watu
wanaokatisha masomo ya wanafunzi, kwa kuwaoa, kuwapa ujauzito na
kuwaoza.

Ofisa Elimu Wilaya ya Misungwi, Dianah Kuboja, alipotafutwa ili
azungumzie tatizo la wanafunzi kubeba ujauzito wilayani humo,
hakupatikana ofisini kwake. Simu yake ya kiganjani pia haikuwa hewani
wakati alipotafutwa.

Mkuu wa Wilaya hiyo (DC), Juma Sweda, anasema kukamatwa kwa watu hao,
wakiwamo baba mzazi wa binti na yule wa muoaji, ulitokana na taarifa
zilizoripotiwa mapema na Mtendaji Kata ya Igokelo.

“Wamo ndani,” anasema DC Sweda, huku akitoa onyo kwa wazazi na walezi
wenye tabia ya kuwaoza wanafunzi, akisema wakibainika lazima
watakamatwa na kushtakiwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Mkuu huyo wa wilaya anasema kuwa, watu wote waliohusika kumuoza mtoto
huyo watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana, alipoulizwa juu ya
tukio hilo, hakuwa tayari kulizungumzia akisema, yupo ‘bize’ na tukio
la kuzama Kivuko cha MV Nyerere huko Ukerewe mkoani hapa.

KIVULINI

Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally, anataja visababishi
vya mimba na ndoa hizo za utotoni kuwa ni, familia nyingi kutelekezwa
na wanaume, wakati huu wa mavuno.

Anasema baadhi ya watoto hukosa usaidizi wa baba zao, kutokana wanaume
hao kwenda kuponda starehe na magenge ya makahaba, maarufu kwa jina la
“Nzige, Kisemosi au Kipapatio.”

Sababu nyingine zilizotajwa na Ally ni uwapo wa minada mingi, baadhi
ya wanafunzi wa darasa la saba kukata tama ya masomo, kutokana na
wazazi wao kuwatishia kuwalaani iwapo watafanya vizuri kwenye
mitihani, kisha kushinda kwenda sekondari.

“Sasa shida ipo hivi, kuna mtindo wanafunzi wanaokabiliwa na mitihani
mbeleni, huwa wanakwenda kuweka kambi kwenye miji ya watu. Wavulana
wanne na wasichana wanne. Na wanasema kinachoendelea huko siyo kusoma.
Wanafanya mambo yao mengine.

“Na hii ni kama imehalarishwa na walimu pamoja na wazazi,” anasema
kiongozi wa Shirika
hilo la Kivulini, linaloendesha kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia
wilayani Misungwi.

Ally anasema, wazazi huwaamuru watoto wao kuchora madudu kwenye
mitihani, ili washindwe kwenda sekondari waolewe na kuipatia familia
ng’ombe, huku wakiume wakiwa wasaidizi wa kuchunga mifugo nyumbani.

Mkurugenzi huyo wa Kivulini aliwataja pia walimu kuwa baadhi yao
wanatabia za kuadhibu, kukariri na kukamia watoto kwa kuwapiga viboko,
wanafunzi wanaokabiliwa na tatizo la ukosefu wa sare za shule.

“Hivi vitu si tu vinawakatisha tamaa baadhi ya wanafunzi kuendelea na
masomo, bali vinawaathiri hata kisaiklojia. Baadhi ya walimu wamezoea
kuwa na vitisho, hasa wanapokuwa zamu ya kusimamia wanafunzi shuleni,”
anasema Ally.

Mkurugenzi Ally anasema: “Na kwa sababu walimu hawana lugha ya
kirafiki, mtoto anabakwa njiani akifika shuleni hawezi kusema anakaa.
Mwalimu akiuliza swali akishindwa tu kujibu, fimbo. Huyu mtoto
hatakaa.”

Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kata ya Idetemya, wilayani
humo (jina tunalihifadhi) anasema:

“Kempu za kujisomea wengi hawafanyi hivyo. Wanakaa kitandani eti
wanajisomea, wanashikana shikana, halafu mambo mengine yanaendelea.”

HALMASHAURI

Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Thomas Lutego,
anasema mimba na ndoa za utotoni hazikubaliki, huku akilishukuru
Shirika la Kivulini kwa kuanzisha kampeni kupinga ukatili wa kijinsia
wilayani humo.

Anasema Halmashauri ya Misungwi inaangalia namna ya kukabiliana na
changamoto ya wanafunzi wa Sekondari ya Igokelo, wanaotembea umbali
mrefu.

“Ipo bajeti ya kujenga mabweni. Lakini, ile ya kujenga sekondari zaidi
hapa Igokelo haipo kwa mwaka huu 2018/2019. Tunaamini upatikanaji wa
fedha ndiyo utakaosaidia kuleta maendeleo,” anasema Lutego.

Baadhi ya wazazi wilayani humo wameshauri Wizara ya Afya na wadau
wengine, kuanza kuelimisha wanafunzi juu ya madhara ya nzao za
utotoni, kwani mbali na kukatisha ndoto zao, pia vinasababisha vifo.

Ester Maduhu, Sayi Kija na Seleman Jacob, wanapendekeza kila kata
ijengewe sekondari mbili, ili kuondoa vikwazo vya wanafunzi wa kike
kutembea umbali mrefu.

“Ikiwezekana hata sheria ibadilishwe. Badala ya kufungwa aliyempa
mimba mwanafunzi, mwanafunzi wa kike atakayebeba ujauzito akamatwe na
afungwe miaka 30 jela.

“Tukifanya hivi hata wao wanafunzi wa kike wataogopa kujamiana,”
anasema Saida Mohamed, mkazi wa Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza.