Miongoni mwa habari tulizozipa kipaumbele kwenye toleo hili ni ile inayohusu uamuzi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza kutupilia mbali kesi dhidi ya waandishi wa habari wawili waliobambikiwa kesi.
Waandishi hao walishitakiwa kwa kile kinachodaiwa kwamba walijifanya ni maofisa wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Nchi za Ukanda wa Joto (TPRI).
Hakimu Bahati Chitepo amesema mamlaka zinazohusika, yaani TPRI na Jeshi la Polisi zilipaswa kuwapongeza wanahabari hao kwa kusaidia kufichua maovu na siyo kuwafungulia kesi ya jinai.
Amesema baada ya kupitia maelezo yaliyotolewa na upande wa mashitaka amebaini kuwa waliopaswa kukamatwa na kushitakiwa ni wamiliki wa duka la pembejeo za kilimo na mifugo ambao walibainika kuuza viuatilifu ambavyo havijasajiliwa hapa nchini, na akashangaa kuona badala yake wakakamatwa waandishi wa habari waliosaidia kufichua hujuma hizo.
Tunaipongeza Mahakama ya Mkoa wa Mwanza kwa uamuzi wa busara wa kuitupa kesi hiyo. Tunaamini kesi za aina hii zipo nyingi katika mahakama mbalimbali nchini. Kama waandishi wa habari ambao wana mahali pa kusemea wanaweza kubambikiwa kesi kwa kiwango hiki, basi ni wazi kwamba hali ni mbaya mno kwa wananchi maskini wasiokuwa na sauti.
Tukio hili la Mwanza ni mfano halisi wa namna waandishi wa habari wanavyokabiliwa na hatari wawapo kazini.
Hakimu Chitepo amehoji jambo la maana ambalo nasi hatuna budi kuungana naye kuhakikisha linapatiwa majawabu. Nalo ni lile la kuwakamata wanahabari waliofuatilia taarifa ya kuwapo viuatilifu hatari na kuwaacha hao walioshiriki kuviingiza na kuviuza.
Kwa uamuzi huu wa Mahakama, jamii sasa ingependa kujua nini hatma ya hao walioshiriki kuingiza bidhaa hizo haramu na hao watetezi wao, yaani TPRI na polisi. Inavyoonekana ni kwamba matukio haya yapo mengi, na vyombo vya dola vimekuwa walinzi wa uhalifu huu.
Watanzania wangependa kujua maofisa wa TPRI walioshiriki njama za kuwabambikia kesi wanahabari na kuwaacha watuhumiwa halisi wanachukuliwa hatua gani.
Tunachukua fursa hii kuwaasa wanahabari wote kusimama imara katika kufichua maovu yanayoliangamiza taifa letu. Kamwe wasiogope.
Wala asiwepo wa kudhani kuwa kwa kuwabambikia wanahabari kesi za aina hii atawakatisha tamaa kufanya kazi zao kwa weledi.
Mwisho, TPRI ijitokeze sasa kueleza hatua ilizochukua au inazokusudia kuchukua dhidi ya watumishi wake wanaoshirikiana na wafanyabiashara kwenye uhalifu huu.
Tunaipongeza Mahakama ya Mkoa wa Mwanza kwa kutenda haki. Mwito wetu ni kuona Mhimili wa Mahakama unatumia busara hii ili kuwaokoa mamia ya watu wanaobambikiwa kesi.