New York, Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Ri Yong-ho, ameonya kuwa hakuna namna ambayo nchi yake itaharibu zana za nyuklia wakati Marekani bado inaendelea kuiwekea vikwazo.
Ri Yong-ho aliuambia mkutano wa Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York, Marekani kwamba vikwazo hivyo vinapunguza imani kwa Marekani.
Hivi karibuni Korea Kaskazini imerejea wito wake wa kuitaka Marekani na Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo hivyo na imeungwa mkono na washirika wake wa karibu kutoka China na Urusi.
Lakini uongozi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, unasema vikwazo hivyo vitadumu hadi pale Korea Kaskazini itakapoharibu zana zake za nyuklia.

Rais Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, walifanya mkutano wa kihistoria mwezi Juni, mkutano huo ulifanyika nchini Singapore, ambapo Rais Kim aliahidi kuharibu zana za nyuklia.
Waziri wa Mambo ya Nje, Ri, anasema Marekani ilikuwa inasisitiza suala la kuharibiwa silaha kwanza, sera ambayo iliongeza idadi ya vikwazo.
“Bila ya imani kwa Marekani hatuwezi kuwa na uhakika wa usalama wetu wa kitaifa, na katika hali kama hiyo, hatuoni sababu ni kwa namna gani tutaharibu silaha zetu kwanza.
“Imani kuwa vikwazo vinaweza kuchangia sisi kusalimu amri ni ndoto,” alisema.

Kipi kimefanyika tangu mkutano wa Singapore?

Makubaliano yaliyoafikiwa huko ni kwamba Korea Kaskazini ingeharibu zana zake za nyuklia, lakini hayakuwa na mwongozo au muda au njia ya kuthibitisha mchakato huo.
Mwezi Agosti Rais Trump aliilaumu China ambaye ni mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini kwa suala hilo kutokana na tofauti zake za kibiashara na Marekani.

Hata hivyo mapema mwezi huu Kiongozi wa Korea Kusini, Moon Jae-in, alifanya ziara ya siku tatu nchini Korea Kaskazini – ikiwa ndiyo ya kwanza kufanywa na rais wa Korea Kusini mjini Pyongyang kwa miongo kadhaa.
Rais Moon anasema aliweza kuthibitisha kujitolea kwa Kim Jong-un katika kuharibu zana za nyuklia, pia alikuwa na nia ya kukutana tena na Rais Trump hivi karibuni.
Kim pia aliahidi kuharibu eneo kuu la kufanyia majaribio ya makombora.