Aliyekuwa mgombea urais nchini Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean-
Pierre Bemba, ameubeza uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Desemba 23,
mwaka huu kwa kuufananisha na maigizo
yaliyopangwa kutimiza matakwa ya
wachache.
Akizungumza na wanahabari mara baada
ya jina lake kuwa miongoni mwa wagombea
sita walioenguliwa na Mahakama Kuu nchini
humo, amesema wananchi wa Congo
hawatakuwa tayari kuchaguliwa kiongozi na
kikundi cha watu wachache.
Katika mahojiano yake na Televisheni ya
France 24, amesema taifa hilo linatarajiwa
kushuhudia uchaguzi uliojaa maigizo
yaliyopangwa na watawala wachache
wenye nia ya kumweka kiongozi
wanayemtaka, atakayelinda masilahi ya
watu wachache.
Ingawa yeye na wenzake walikata rufaa
kupinga kuenguliwa kwao, lakini rufaa yao
ilikataliwa na Mahakama ya Katiba nchini
humo.
Bemba anatuhumiwa kwa kufikishwa kwake
katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu
wa Kivita (ICC).
Amesema uchaguzi huo wa kilaghai
hauwezi kuungwa mkono na wananchi
waliochoshwa na uongozi usiojali masilahi
mapana ya wananchi maskini wanaoishi
chini ya dola moja, licha ya nchi yao kuwa
na utajiri wa kila aina ya madini kila pembe
nchini humo.
Bemba alitangaza nia ya kugombea
urais baada ya kurejea nyumbani akitokea
nchini Ubelgiji na kupokewa na maelfu ya
wafuasi wake waliojitokeza kumpokea
uwanja wa ndege baada ya Mahakama ya
ICC ya mjini The Hague, Uholanzi kumfutia
mashtaka ya uhalifu wa kivita.
Bemba aliwahi kuwa kiongozi wa kundi la
waasi la Congolese Liberation Movement
(MLC), ambalo lilikuwa na wapiganaji 1,500
wakiungwa mkono na nchi jirani ya Uganda,
kisha kuanzisha mapambano dhidi ya
utawala wa Rais wa sasa nchini humo,
Joseph Kabila.
Aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais katika
serikali ya mpito kuanzia mwaka 2003 hadi
2006. Alizaliwa Novemba 4, 1962 katika
eneo la Bogada, Mkoa wa Equatuer ulioko
kaskazini – magharibi mwa nchi hiyo.
Baba yake alikuwa mfanyabiashara tajiri
mwenye ukaribu na dikteta Mobutu Sese
Seko, aliyetawala kuanzia mwaka 1965 hadi
alipopinduliwa mwaka 1997.
Mwaka 2007 alikimbilia nchini Ubelgiji,
baadaye alikamatwa kwa hati ya Mahakama
ya ICC kwa uhalifu wa kivita uliofanywa na
jeshi lake binafsi katika Jamhuri ya Afrika ya
Kati kuanzia mwaka 2002 – 2003.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa
mitandao.
Mwisho