*Kesi ya Singa, Rugemalira, wabunge
zamtia kitanzini
*Mfumo mpya kupokea, kukalia taarifa
wamponza
*Rais Magufuli apasua jipu, yeye ajipiga
‘kufuli’
Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
Kushindwa kupambana na rushwa kubwa,
kutotengeneza mazingira rafiki kwa watoa
taarifa za rushwa na kupuuza taarifa za
rushwa, ni miongoni mwa sababu kadhaa
ambazo zimemfanya Rais John Magufuli
kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa nchini (Takukuru), Kamishna
Valentino Mlowola, uchunguzi wa Gazeti la
JAMHURI umebaini.
Baada ya kutoka mapumzikoni, Rais
Magufuli alianza ziara ndefu katika mikoa ya
Kanda ya Ziwa; Mwanza, Mara na Simiyu,
siku ya Alhamisi, kama ilivyokawaida ‘Amka
na BBC’ tangazo maarufu la Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa,
likatawala katika mitandao ya kijamii.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dk. John Magufuli
amemteua Kamishna wa Polisi, Diwani
Athumani, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi wa Kuzuia na Kupambana na
Rushwa… Kamishna Diwani Athumani
anachukua nafasi ya Kamishna wa Polisi,
Valentino Mlowola, ambaye ameteuliwa
kuwa balozi,
” mwisho wa kunukuu tangazo
la Msigwa.
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la
JAMHURI unaonyesha kwamba tangu
Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola
ameshika hatamu za uongozi kwenye ofisi
yenye Makao Makuu Upanga, jijini Dar es
Salaam, alianza kutengeneza mazingira
magumu kwa watoa taarifa za rushwa
(whistle blowers).
Chanzo chetu kutoka katika Ofisi ya
Takukuru ambacho hakikutaka kutajwa jina
lake gazetini kimesema tangu afande
Mlowola awe mkurugenzi mkuu, alibadili
utaratibu hata wa namna ya kupata taarifa
kutoka kwa watoa taarifa za siri.
“Unajua rushwa ni jambo ambalo linafanyika
kwa siri sana… hivyo unahitaji kuwa na
‘whistle blowers’ ili kufanikisha vita hii.
Tumekuwa tukifanya hivyo miaka yote enzi
za mzee [Meja Jenerali Anatory] Kamazima,
Dk. [Edward] Hoseah na hata kabla ya
hapo, ila baada ya bosi mpya [Mlowola] kuja
akaanza kutengeneza mazingira magumu
ya kupata taarifa za siri.
“Huwezi kumwambia mtoa taarifa za siri
aache kila kitu chake mapokezi wakati siku
hizi mfumo wa teknolojia umekua sana.
Siku hizi simu ni chombo muhimu cha
kukusanyia ushahidi. Alipoingia Mlowola
ukifika getini wanakwambia uache simu
yako, kisha uende mikono mitupu.
Tukajiuliza, kuna nini? Wanataka kuficha
nini? Kuna mambo hayakwepeki katika
kukamilisha kupata ushahidi wa shauri
linalohusiana na rushwa…,
” kimesema
chanzo chetu.
Wakati Gazeti la JAMHURI likipata dondoo
zilizosababishwa kutenguliwa kwa uteuzi wa
Valentino Mlowola, Rais John Magufuli
ametaja moja ya sababu zilizomfanya
kumuondoa kuwa ni pamoja na kushindwa
kushughulikia mgogoro wa ardhi uliojitokeza
Musoma, Mara.
“Ukweli utabaki kuwa ukweli, ni lazima
tubadilike hata ndani ya chama,
” amesema
Rais Magufuli na kuongeza:
“Mimi huwa sijali kutumbua, natumbua tu…
Nimeenda pale Musoma, mtu amenunua
Musoma Hotel hashughuliki, kila kandarasi
hamalizi, waziri mkuu akapita hapa Mara
akatoa maagizo kwa PCCB (Takukuru)
shughulikia hili…”
Amesema Mkuu wa Takukuru wa Mkoa wa
Mara baada ya kupokea maagizo ya waziri
mkuu alishughulikia suala hilo ilipofika Aprili
mwaka huu na alipeleka mapendekezo
Makao Makuu ya Takukuru lakini chombo
hicho kikashindwa kutoa uamuzi.
“Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara
akalimaliza mwezi wa nne, akalipeleka
makao makuu na ameweka
recommendations (mapendekezo) zake
zote, makao makuu tangu mwezi wa
nne, leo mwezi wa tisa hawajalishughulikia.
“Nikaona Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru
lazima akae pembeni afanye kazi nyingine
na nikafanya hivyo. Nikaangaliaa na mambo
mengine yakajitokeza, nikaona kazi hii ya
kushughulikia rushwa haiwezi,
” alisema na
kushangiliwa.
Vyanzo vyetu vinasema sababu nyingine ni
kushindwa kushughulikia ushahidi wa
mashauri ya rushwa kubwa, ambapo hapa
zimetajwa kesi kadhaa ambazo zipo
mahakamani, ikiwemo ile ya IPTL. Tuhuma
nyingine ni kesi za ukiukwaji wa sheria na
kanuni za maadili ambazo hazijafikishwa
mahakamani, chini ya Mlowola Takukuru
imekuwa kimya.
Tuhuma nyingine kwa mujibu wa vyanzo
vyetu ni kushindwa kuwafikisha
mahakamani waliohujumu mita za mafuta
katika Bandari ya Dar es Salaam, jambo
ambalo inasemekana ushahidi wake
ulikuwa dhahiri, lakini pia Rais Magufuli
alitamani kuona watuhumiwa wakifikishwa
kwenye vyombo vya sheria.
Taarifa za ndani ambazo Gazeti la
JAMHURI limezipata zinaonyesha kwamba
yamekuwepo malalamiko kadhaa kutoka
kwenye taasisi nyeti, likiwemo Bunge dhidi
ya utendaji wa Mlowola, ambako wabunge
watatu walipandishwa kizimbani kwa
tuhuma za rushwa.
Wabunge hao ni Waziri wa sasa wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola; Mbunge
wa Mvomero, Sadick Murad na Mbunge wa
Lupa, Victor Mwambalaswa, wakituhumiwa
kupokea hongo ya Sh milioni 30.
Wabunge hao walituhumiwa kuomba
rushwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Gairo, Mbwana Magotta. Wote
walikuwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa
(LAAC) wakati huo.
Wabunge hao wa CCM walifikishwa mbele
ya Hakimu Mkazi, Thomas Simba Machi 31,
mwaka 2016 na kusomewa mashtaka na
Wakili wa Takukuru, Maghela Ndimbo.
Kwa pamoja walidaiwa kwa nafasi zao za
ujumbe wa LAAC kuwa waliomba rushwa
ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Gairo, mkoani Morogoro, Mbwana Magotta
ili waweze kutoa mapendekezo mazuri ya
Taarifa ya Hesabu za halmashauri hiyo za
mwaka 2015/2016.
Walidaiwa kutenda kosa hilo Machi 15,
2016, kinyume cha Kifungu cha 15 (2) cha
Sheria ya Takukuru, wakiwa katika Hoteli ya
Golden Tulip, iliyoko eneo la Masaki,
wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Agosti 3, 2016 Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP), Biswalo Mganga, aliwasilisha
mahakamani hati ya nia ya kutoendelea na
kesi, hivyo Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu ikaifuta kesi hiyo.
Gazeti la JAMHURI limemtafuta Kamishna
Valentino Mlowola kupata ufafanuzi kuhusu
tuhuma zinazomkabili ambaye amesema
kwa sasa yeye ni balozi si mfanyakazi wa
Takukuru.
Alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais Magufuli
kwamba alishindwa kuchukua hatua dhidi
ya ubadhirifu wa mradi wa maji Mkoa wa
Mara, amesema anayeweza kuzungumzia
hilo ni Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru si
yeye.
“Unajua ndugu yangu haya unayoyasema
kama ungenitafuta juzi ningeweza kukujibu,
lakini sasa siwezi kusema lolote huko
nilishatoka. Mimi ni mwananchi wa kawaida,
ni balozi sasa, hivyo naomba uheshimu
privacy (faragha) yangu,
” amesema Balozi
Mlowola.
Vyanzo vyetu ndani ya Takukuru vinasema
dalili za kutumbuliwa kwa Mlowola zilianza
kuonekana tangu Agosti mwaka jana,
baada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya
kushtukiza Makao Makuu ya Takukuru na
kueleza kutoridhishwa na kasi ya
kupeleleza na kufikisha mahakamani
mashauri makubwa ya rushwa.
Rais Magufuli alinukuliwa akisema: “Kuna
mambo mengi ya hovyo yanafanyika.
Tumehakiki pembejeo za ruzuku na kubaini
madai ya Sh bilioni 48 ni hewa, tumebaini
wafanyakazi hewa zaidi ya 19,500,
tumebaini kaya maskini hewa 56,000
zilizopaswa kupata fedha Tasaf.
“Tumebaini wanafunzi hewa 5,850
waliotakiwa kupata mkopo, kuna vichwa vya
treni 11 vimeletwa bila kuwepo mkataba na
mengine mengi. Haya yote yanafanyika kwa
rushwa, nataka kuwaona mnachukua hatua
stahiki.”
Rais alifanya ziara hiyo wiki moja baada ya
kumteua Brigedia Jenerali John Mbungo
kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa
Takukuru.
Takukuru imewafikisha mahakamani vigogo
kadhaa kwa tuhuma za rushwa akiwamo
mfanyabiashara, James Rugemalila, na
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kufua
umeme ya IPTL/PAP, Harbinder Seith
Singh, kwa rushwa na uhujumu uchumi.
Kesi nyingine kubwa ni ya aliyewahi kuwa
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Harry Kitilya, wakili
maarufu, Dk. Ringo Tenga na ya viongozi
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
ambao wanashtakiwa kwa rushwa na
uhujumu uchumi.
Baadhi ya kesi hizi zimechukua zaidi ya
miaka miwili bila kusikilizwa, huku zikipigwa
kalenda kwa kutokamilika upelelezi na kila
zinapoitwa mahakamani huelezwa kuwa
upelelezi haujakamilika.
Mwaka 2016, baada ya kuteuliwa kuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino
Mlowola, alizungumza na Gazeti
la Mwananchi, hapa chini ni mtazamo wake
kuhusu masuala ya rushwa na namna
taasisi hiyo inavyojipambanua kupambana
na rushwa.
Mlowola ambaye amewahi kuwa Kamishna
wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa
Intelijensia ya Makosa ya Jinai katika Jeshi
la Polisi alisema: “Nikiri kabla ya kufika
Takukuru nilikuwa polisi, moja ya mambo
niliyokuwa nayashughulikia ni mikakati ya
kupambana na ugaidi Tanzania.
“Nilikuwa nadhani wakati ule tatizo
linaloathiri usalama wa nchi yetu na dunia
ilikuwa ugaidi, lakini baada ya kuja
Takukuru nimegundua kuwa tatizo kubwa
kwa serikali ni rushwa.”
Anasema uuzaji wa dawa za kulevya
ukikithiri lazima kuna rushwa nyuma yake,
vivyo hivyo katika ujangili na sekta ya
ujenzi.
“Ujangili unafanyika kutokana na kushamiri
kwa rushwa, katika sekta ya ujenzi ukiona
majengo yanaanguka na barabara na
madaraja kujengwa chini ya kiwango, ujue
kuwa tatizo ni rushwa,
” anasema.
Anasema licha ya kuwa tatizo la rushwa ni
kubwa nchini, Takukuru inafanya jitihada za
dhati za kupambana nalo, jitihada alizodai
kuwa ni za kiwango cha juu kuliko
ilivyokuwa zamani.
“Siri kubwa ya mapambano dhidi ya rushwa
duniani yanategemea sana utashi wa
kisiasa. Unaweza kuwa na sheria, taasisi
nzuri, lakini ukikosa utashi wa kisiasa
mapambano yote ya rushwa hayatakuwa na
nguvu,
” anasema.
Ukubwa wa rushwa Tanzania
Anasema tatizo la rushwa nchini ni kubwa
na ndiyo sababu wagombea urais katika
Uchaguzi Mkuu uliopita sambamba na
vyama vyao, ajenda yao kubwa ilikuwa ni
kupambana na rushwa na ufisadi.
“Hii inamaanisha tatizo ni kubwa nchini
ndiyo maana ilikuwa ajenda kuu ya kisiasa.
Rais Magufuli aliahidi katika kampeni zake
kuwa atapambana na ufisadi na kuahidi
kuunda mahakama ya mafisadi. Hata
Ukawa, ajenda yao ilikuwa ni ufisadi. Kila
chama makini kilizungumzia ufisadi na
maana yake tatizo la rushwa lilikuwa kubwa.
“Taasisi mbalimbali zilifanya utafiti na
kuonyesha hali hii ya rushwa nchini.
Wanahabari nao mlizungumza na wananchi
wa kawaida, mliona jinsi wanavyolalamikia
rushwa katika huduma, mfano za hospitali,
”
anasema.
Anasema tatizo la rushwa si Tanzania
pekee, bali ni la dunia nzima, huku akitolea
mfano jinsi rushwa ilivyozua mjadala katika
mkutano wa wakuu wa nchi wa kujadili
mapambano dhidi ya rushwa (Anti-
Corruption Summit 2016) uliofanyika
London, Uingereza.
“Katika mkutano ule (Anti Corruption
Summit 2016) ambao Rais John Magufuli
alialikwa, lakini akawakilishwa na Waziri
Mkuu (Kassim Majaliwa). Yeye (Rais
Magufuli) pamoja na rais wa Nigeria
walitambuliwa katika mapambano yao dhidi
ya rushwa,
” anasema.
Anasema katika mkutano huo rushwa
ilionekana ni tatizo duniani na imeathiri hata
masuala ya usalama.
Anasema kama uchumi wa Tanzania ukitoa
tija ya kuweza kugharamia huduma za jamii
kwa ufanisi zaidi, rushwa itapungua, hasa
rushwa ndogo, kwa maelezo kuwa katika
hospitali, shule na maeneo mengine ya
kutoa huduma kila kitu cha msingi
kitakuwapo.
“Kukiwa na huduma hafifu kunakuwa na
kinyang’anyiro. Watu wenye nguvu
watataka kupata kipaumbele, lakini wakati
huohuo watumishi wa serikali vipato vyao
vidogo, hivyo watu wenye uwezo
wanawarubuni watumishi ili wawape
upendeleo,
” anasema.
Ulafi wa viongozi
Kuhusu rushwa kubwa, Mlowola anatolea
mfano mtu mwenye wadhifa wa uwaziri au
ukurugenzi ambaye analazimisha kupata
zaidi licha ya kuwa kipato chake ni kizuri.
“Kwa hali hii kampuni zinazotaka rasilimali
zitakuhonga na wewe kwa sababu ya nafasi
yako ukafanya mambo bila kujali masilahi
ya nchi yako.
“Makampuni makubwa yanahonga viongozi
wa Afrika ili wapate ulaji na sisi tunatumika
hivyo na hilo ndilo tatizo kubwa,
” anasema.
Akizungumzia madai kuwa kesi za rushwa
zinasuasua kutokana na kukosekana kwa
ushahidi, Mlowola anasema jambo hilo si
kweli, kwa maelezo kuwa Takukuru
inashinda kesi nyingi.
Hata hivyo, anakiri kuwa kuna udhaifu
katika upelelezi, pia katika upatikanaji wa
mashahidi, na tatu ni rushwa yenyewe
kuingia hadi ndani ya vyombo vya kutolea
haki.
Anasema kuna kesi za rushwa ambazo
ushahidi wake una mlolongo mrefu na
kuhusisha nchi zaidi ya moja, jambo ambalo
wakati mwingine huchukua muda mrefu na
hatimaye kesi husika kutupwa.
“Unaomba ushahidi huko Australia na
mlolongo wake ni mrefu, lazima ipite kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na
Wizara ya Mambo ya Nje ya huko, kisha
waende kwa mwanasheria mkuu wa huko
au DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka),
watathmini, hivyo inachukua muda mrefu na
kuna nchi ambazo ushahidi huo upo, zina
tabia ya kulinda makampuni yao,
” anasema.
Anasema changamoto inayoikumba taasisi
hiyo kwa sasa ni kupokea taarifa kwa
kiwango kikubwa kutokana na msisitizo wa
rais katika kupambana na rushwa na
ufisadi.
“Taarifa ni nyingi mno kiasi cha kushindwa
kuzikabili na kutoa majibu ya haraka. Ila
tunajipanga kukabiliana na hiyo hali. Ila
changamoto nyingine zinatatulika,
”
anasema Mlowola.
Mwisho