MBUNGEĀ na mwanamuziki, Bobi Wine, leo anatarajiwa kurejea mahakamani mjini Gulu, kaskazini mwa Uganda anapokabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Bobi Wine na washukiwa wegine 32 wanatarajiwa kusomewa mashtaka yao kisha kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu. Mahakama ya mwanzo ya Gulu haina mamlaka ya kisheria kuendesha kesi za uhaini. Baadhi ya washitakiwa wanaendelea kupata matibabu hospitalini na huenda wakashindwa kuhudhuria mahakamani ambapo watawakilishwa na mawakili wao.
Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi ni mwakilishi wa eneo bunge la Kyadondo Mashariki na ni msanii maarufu wa muziki nchini Uganda. Alikamatwa wiki mbili zilizopita kwa tuhuma za uvamizi wa msafara wa Rais Museveni mjini Arua na kupokea kipigo kikali yeye na wenzie 32 kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama. Dereva wa Bobi Wine alipigwa risasi na kuuawa katika purukushani hizo.
Watuhumiwa hao waliwekwa chini ya ulinzi wa jeshi huku Bobi Wine awali akipandishwa katika mahakama ya kijeshi kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria. Rais Yoweri Museveni alijitokeza na kukanusha taarifa kuwa Bobi Wine ameumizwa vibaya na kuvishutumu vyombo vya habari kwa kueneza taarifa za uongo.
Baada ya kelele za upinzani kupazwa ndani na nje ya Uganda pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, kesi yake mbele ya mahakama ya kijeshi ilifutwa na kuachiwa huru kabla ya kukamatwa tena na kufunguliwa mashtaka ya uhaini katika mahakama ya kiraia. Jumatatu wiki hii, Bobi Wine na washukiwa wengine wote waliachiwa kwa dhamana.