Wizara ya Fedha imeombwa ipeleke boti wilayani Rorya, Mara ili kukabiliana na maharamia katika Ziwa Victoria. Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Chacha, amesema matukio ya uvuvi haramu na biashara ya magendo vinashamiri Ziwa Victoria upande wa Rorya kutokana na kukosekana kwa boti ya doria. Amesema maharamia wakiwamo wanaotoka nchi jirani, hupora nyavu, samaki, mafuta na hata boti za wavuvi wa Tanzania na kukimbilia nchi jirani. Amesema endapo boti itapatikana, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kituo cha Shirati itashirikiana na Jeshi la Polisi ili kukabiliana na biashara ya magendo, maharamia na watu
wanaoendesha vitendo vya uvuvi haramu. “Kuna wimbi kubwa la wahalifu – wavuvi haramu na maharamia wanaoingia nchini katika maeneo yetu ya wilaya hii katika Ziwa Victoria na kuendesha vitendo vya unyang›anyi na wakati mwingine kuwapiga Watanzania viboko. “Kuna biashara ya magendo kutoka nchi jirani –wanaingiza mabati, sukari, nguo na bidhaa nyingine na hivyo kuikosesha Serikali mapato,” amesema Chacha. Meneja wa Forodha TRA mkoani Mara, Laurent Kagwebe, amesema; “Idara yetu ya Forodha kituo kikubwa mkoani hapa cha mpakani Sirari wilayani Tarime tuna gari moja la doria – linafanya kazi usiku na mchana kuzunguka kukamata watu wanaoingiza bidhaa nchini bila kufuata taratibu kwa kupitia njia za panya zilizoko wilaya za Tarime na
Rorya. “Katika mipaka ya nchi kavu pekee kuna njia za panya 48 ambazo zinapitika kwa magari, baadhi zipo katika vijiji vya Sirari, Kubiterere, Kogaja, Shirati, Ikoma, Gosebe, Kibeyo, Borega, Nyansincha, Itiryo na Kegonga. «Hata sisi wenyewe tunaomba kupatiwa msaada wa magari mengine na pikipiki na hiyo boti ili tuweze kukabiliana na wimbi hili la biashara
ya magendo kwani hili gari moja kuzunguka njia zaidi ya 48 katika wilaya mbili tunapata wakati mgumu kuwakamata. “Wafanya magendo wamekuwa wakiliona gari letu kwenye vijiji na kupigiana simu, vijana wa pikipiki huvusha mizigo kuingiza nchini na kutoa bidhaa nyingine kwenda nje ya nchi hali inayotuwia vigumu kuwadhibiti kutokana na upungufu wa vitendea kazi kama magari na pikipiki. Tunaomba msaada huo ili tuweze kwenda na kasi ya kudhibiti wafanya magendo na kasi ya kukusanya mapato kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu,” amesema. Ametoa mwito kwa wafanyabiashara kulipa ushuru na kodi bila shuruti ili kuepuka usumbufu usio wa lazima. Ameonya kuwa wanaofanya biashara za magendo wakikamatwa mali zao, vikiwamo vyombo vya usafiri vitataifishwa.