Kabla ya michuano ya Kombe la Dunia kuanza
nchini Urusi mwaka 2018, kulikuwa na matumaini
makubwa kuwa Afrika ingeendeleza kasi ya ukuaji
katika soka kama ilivyofanya nchini Brazil mwaka
2014 wakati wawakilishi wake wawili – Nigeria na
Algeria walipofikia hatua ya mtoano kwa mara ya
kwanza.
Badala yake bara zima litakuwa linajiuliza ni wapi
chombo kimekwenda mrama, kwani timu za Afrika
zimeshinda mechi tatu na kufungwa 10 katika vipute
vyao 15 kwa jumla. Dakika 20 za mwisho zimekuwa
mwiba mzito kwa timu za kutoka Afrika katika
mashindano haya.

Tunisia

Tunisia ilikuwa Kundi G kabla ya kuifunga Panama
katika hatua ya lala salama, ambapo wawili hao
walikwisha kufahamu kuwa wanaelekea nyumbani.
Ingawa Nigeria iliifunga Iceland, pia imeondoka
Urusi kwa kumaliza katika nafasi ya tatu kwa Kundi

D.
Tunisia haikufuzu kutoka kundi gumu lenye
Uingereza na Ubelgiji.
Tunisia maarufu, Carthage Eagles, walilazwa na
Uingereza dakika za mwisho, sawa na mataifa
mengine ya Afrika yalivyoathirika kutokana na
mabao ya kuchelewa na mipira ya juu.
Ingawa kutokuwepo kwa nyota wao Youssef
Msakni, imetajwa kuwaumiza, mchango wake pia
haungeweza kuwazuia walipobomolewa na Ubelgiji
5-2.
Mbali ya yote hayo, Tunisia wameacha historia ya
kufunga magoli matano katika mechi tatu.

Misri

Misri ilitarajiwa kuweka rekodi yake katika Kombe la
Dunia kwa kuwa na kikosi kizuri chenye mmoja wa
wachezaji bora duniani.
Kwa mtazamo wowote ule, Mohamed Salah,
alitawala kampeni ya kufuzu kwa Misri – kati ya
mabao 10 ya Misri, Mo Salah alifunga saba na
kuchangia mengine mawili yaliyowasaidia kushiriki
Urusi.
Kwa bahati mbaya aliumia. Aliyechukua nafasi ya
Salah – Marwan Mohsen – mwenye goli moja mechi
23 za kimataifa – hakufanya lolote.
Hata iwapo Salah angekuwa na hali nzuri, ufanisi
wa Misri unazidi kutiliwa shaka baada ya kurejea
kwenye Kombe la Dunia ikiwa ni miaka 28 –

walifanya makosa mengi kwenye ulinzi.
Mabeki Ali Gabr na Ahmed Hegazi hawakuelewana
vema licha ya kunolewa na Hector Cuper – Kocha
mwenye uzoefu na idara ya ulinzi.
Misri haijatimiza matarajio ya wengi, kwani kulikuwa
na matarajio chungu nzima kwa mabingwa hao
mara saba wa Kombe la Mataifa barani Afrika.

Morocco

Morocco ilionekana kuzimwa mwanzoni
walipofungua kombe kwa kujifunga wenyewe dakika
za mwisho dhidi ya Iran na kulazwa 1-0.
Safu butu ya ufungaji iliwachuuza Morocco, kwani
hawakuweza kuzitumia nafasi zao mbele ya nyavu
za wapinzani.
Mechi yao ya mwisho, Simba hao wa Atlas,
walikaribia kuilisha Hispania kichapo chake cha
kwanza katika mechi 23, lakini mabingwa hao wa
2010 waliwalazimisha sare ya 2-2 dakika za
mwisho, kama ilivyo ada dhidi ya timu za Afrika
katika kombe hili wakayeyuka.
Morocco iliipa somo Hispania licha ya kuwa na
mastaa wanaokipiga Real Madrid na Barcelona, na
baadhi yao kuichezea Manchester City, Manchester
United, Bayern Munich na Atletico Madrid.
“Ni timu bora sana iliyopoteza mechi mbili 1-0, na
ilistahili zaidi,

” alisema Kocha wa Hispania,

Fernando Hierro.

Nigeria

Kufungwa dakika za mwisho na Argentina
kumeiumiza Nigeria na kuifanya ishutumiwe kutoka
nyumbani, wengi wakistaajabu kwa nini ngome yao
haikupigwa jeki dakika za mwisho, lakini kampeni ya
Super Eagles Urusi ni ya matumaini bora siku za
usoni. Ilikuwa na wachezaji 18 wenye umri mdogo
walioshiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Penalti ya Victor Moses iliiwezesha Nigeria kuipiku
Argentina kwenye kundi kabla ya bao la dakika za
lala salama

Senegal

Senegal, iliyoshiriki Kombe la Dunia tangu ilipofika
robo fainali 2002, imepata alama nne katika Kundi H
baada ya kuifunga Poland na kutoka sare na Japan.
“Limekuwa pigo kubwa kwa bara hili kwa kurudi
hatua moja nyuma, kwani kuondoka kwa Senegal
kumeifanya Afrika kupata matokeo mabaya zaidi
katika miaka 36 iliyopita,

” amesema Drogba.
Senegal imekuwa timu ya kwanza kuondolewa
katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa kutumia
sheria za ‘nidhamu’

, baada ya kulazwa na

Colombia, ila ikalingana kila kitu; pointi, magori ya
kufunga na kufungwa na Japan.

VAR iliifunga Afrika?

Mengi yanasemwa kuwa mtambo wa teknolojia –
Virtual Assistant Referee (VAR), umewaumiza
wengi, ila Afrika imezidi, ingawa Misri na Mohamed
Salah walipata penalti dhidi ya Saudi Arabia
kutokana na uamuzi wa VAR.
Hata hivyo, si Waafrika wote wameondoka Urusi.
Inaelezwa kuwa marefa kutoka Afrika
wataliwakilisha bara hili kwa kusimamia mechi
zinazoendelea za hatua zilizosalia.