NA MUNIR SHEMWETA, LINDI
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amefanya ziara katika mikoa ya Lindi na Ruvuma kukagua mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi, kuhamasishaji ulipaji kodi hiyo na kusikiliza kero za migogoro ya ardhi.
Wengine kwenye ziara hiyo walikuwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kusini, Gasper Luanda, Kaimu Kamishna wa Ardhi Vijijini Kokwika Ishenkumba; na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Denis Masami.
Naibu Waziri alibaini kuwapo kwa uzembe kwa baadhi ya watendaji wa Serikali hasa katika idara za ardhi za halmashauri wasivyotekeleza majukumu ipasavyo.
Hali hiyo imeikosesha Serikali mapato na kuibua chuki miongoni mwa wananchi.
Baadhi ya halmashauri ziko nyuma kwenye matumizi ya mifumo ya ukusanyaji kodi kwa njia ya kieletroniki na nyingine zikiwa zimeshindwa kuingiza wamiliki wa ardhi kwenye mfumo.
Baadhi ya halmashauri alizozitembelea awali na kuzipa maelekezo ya matumizi ya mfumo wa kieletroniki zimeendelea kurudia makosa ya awali.
Mabula alianzia ziara yake mkoani Lindi katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ambako huko alikagua mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi na kuangalia uhifadhi wa majalada ya ardhi. Kwa kawaida jalada hutakiwa kuwa na maelekezo kutoka afisa mmoja kwenda kwa mwingine sambamba na nyaraka muhimu za mwombaji au mmiliki.
Katika halmshauri hiyo Mabuka alibaini kutowasilishwa kwaSh milioni 208 kwenye mfuko wa wizara ikiwa ni makusanyo ya kodi ya ardhi tangu mwaka 2015. Kiasi hicho cha fedha ni cha miezi ya Mei, Juni, Julai na Desemba mwaka 2015.
Aligundua baadhi ya wamiliki wa ardhi kutoingizwa katika mfumo wa kieletroniki wa kulipa kodi ya pango la ardhi; jambo linalotoa mwanya wa kutolipa kodi ya ardhi na wakati hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Akazitaka halmashauri zote nchini kuanzia Julai mosi, mwaka huu kuyatambua na kuyabaini maeneo yote ya mijini ambayo hayana hati ili wamiliki wake walipe kodi ya ardhi kama wanavyolipa wenye hati.
Kwa mujibu wa Mabula, kazi kubwa inayotakiwa kufanywa na halmashauri ni kukagua viwanja vyote na mashamba na kuwa na orodha kamili ya wote wenye maeneo yasiyo na hati ili waingizwe kwenye mfumo wa kulipa kodi ya ardhi.
“Bahati nzuri katika bajeti ya wizara ya 2018/2019 suala hilo limeingizwa hivyo ni lazima wamiliki wa viwanja katika maeneo ya mijini walipe kodi, na katika hili hakuna atakayefaidika na huduma ya ardhi bure,’’ amesema Mabula.
Amesema wapo watu wenye uwezo na maeneo makubwa, lakini Serikali haipati kitu, hivyo ni wajibu wa halmshauri kuhakikisha Serikali inapata mapato kupitia ardhi.
Changamoto kubwa iliyoonekana katika ziara hiyo ya Naibu Waziri ni upungufu wa watumishi na vitendea kazi kwa baadhi ya halmashauri kama ilivyoolezwa na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Lindi, Shaibu Ndemaga.
DC huyo anasema wilaya yake ina upungufu wa wapimaji ardhi, wathamini na vifaa vya kisasa. Pia ufahamu mdogo wa wananchi kuhusu sera ya ardhi nao amesema ni changamoto inayosumbua Halmashauri ya Lindi.
Mabula alizitembelea pia wilaya za Liwale na Nachingwea mkoani Lindi ambako alikutana na tatizo la baadhi ya wamiliki wa ardhi kutoingizwa kwenye mfumo wa kulipia kodi ardhi kwa njia ya kieletroniki.