Na Deodatus Balile, Abuja, Nigeria

Wiki hii nimekuwa hapa jijini Abuja, Nigeria. Nimepata fursa ya kukutana na Rais Mohamed Buhari wa Nigeria. Nimekutana na mawaziri wa Habari, Fedha, Viwanda na Biashara. Kukutana kwetu kumekuwa kama zari. Kilichonileta hapa Nigeria ni kuhudhuria mkutano wa mwaka wa taasisi ya International Press Institute (IPI).

Kumbe Serikali ya Nigeria iliposikia kuna waandishi kutoka nchi zaidi ya 40 duniani, ikaona hii ni fursa ya kutangaza taifa lao. Ikaandaa mapokezi makubwa. Tumepewa kimulimuli kuanzia uwanja wa ndege, hadi katika makazi tulipokuwa tunafanyia mkutano, Hoteli ya Transcorp Hilton, Abuja. Jioni ya Alhamisi, Machi 21 Rais Buhari akawaalika waandishi wote kutoka mataifa ya kigeni Ikulu.

 

Jioni hiyo imekuwa ya aina yake. Tukakuta ameandaa mjadala unaohusu uchumi wa Nigeria. Alikuwa na mawaziri saba, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na yapo maneno yaliyonigusa. Waziri wake wa Fedha, Kemi Adeosun, ambaye ni mwana mama, akatupa takwimu za uchumi linazopambana nazo taifa hili.

 

Waziri Adeosum, akatwambia kuwa Nigeria inapambana kubadili vyanzo vya mapato kwa taifa hili. Amesema hadi mwaka 2015 taifa hili lilikuwa linakusanya wastani asilimia 6 kama mapato ya kodi katika uwiano wa uchumi na kodi (Tax GDP Ratio). Mbaya zaidi, nchi hii imekuwa ikitegemea chanzo kimoja cha mapato; uuzaji wa mafuta.

 

Ametwambia kuwa Nigeria inazalisha mafuta mapipa milioni 10 kwa siku, lakini kwa kulinganisha idadi ya watu wa taifa hili, kiwango hiki ni sawa na sifuri. Amesema sasa wanataka kuingia kwenye viwanda, na katika kufikia azma ya viwanda hawana njia ya mkato zaidi ya kuinua kilimo kwanza wakajitegemee kwa chakula na kuuza ziada nje.

 

Kabla ya uamuzi huu wa kuwekeza kwenye kilimo, Nigeria imekuwa inanunua chakula kwa asilimia zaidi ya 85 kutoka nje. Unajua ndani ya miaka miwili wamefikia wapi? “Kwa sasa tumezalisha tani 600,000 za chakula na kuna mwelekeo kuwa baada ya muda mfupi tutakuwa tunauza chakula nje. Viwanda vimeanza kuja vyenyewe kwa kuwa watu wana shibe,” amesema Adeosum.

Kabla sijajadili kauli ya Waziri Adeosum, naomba nigusie alichotuambia Rais Buhari. “Nchi yetu kwa muda mrefu imekuwa tegemezi katika uchumi. Mafuta yametubwetesha. Kufanya biashara Nigeria lilikuwa jambo gumu. Ukichanganya na changamoto ya usalama kutoka Boko Haram, leseni lukuki, rushwa na wakati mwingine roho mbaya za watendaji, kufanya biashara Nigeria ilikuwa kama haiwezekani.

“Lakini tumeanza, tumebadili masharti mengi. Tumeanzisha utaratibu wa wageni kupewa visa wanapofika uwanjani (visa on arrival), hakuna ofisa anayepaswa kupokea tasilimu katika malipo ya visa au malipo yoyote ya serikali, bali wageni wanalipa kwa kadi na tumetoa muda wa kuwahudumia. Mgeni akilalamikia huduma, ofisa aliyemhudumia atapaswa kutoa maelezo… uwepo wenu hapa (waandishi wa habari) ni uthibitisho kuwa Nigeria sasa kuna amani, dunia inajisikia huru kufanyia mikutano mikubwa kama hii hapa kwetu,”  amesema Rais Buhari.

Sitanii, kwanza uniwie radhi msomaji wangu maana sijawa kwenye safu hii kwa wiki tatu mfulululizo. Lakini pamoja na kutokuwapo nilikuwa nakusanya nondo. Hapa Nigeria kauli ya Waziri wao imenifanya nipitie historia ya uchumi duniani. Nchi kama Uingereza, imefikia katika mapinduzi ya viwanda baada ya kuwa imewekeza katika kilimo.

Nchi kama Marekani imepata utajiri kwa kulima miwa na mahindi ikauza wakati Vita Kuu ya Kwanza na Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Nenda India, Thailand, China, Vietnam na nyingine nyingi zimeendelea kutokana na kuwekeza katika kilimo.

Vietnam kwa mfano, mwaka 1975 ilikuwa na uchumi mdogo kuliko Tanzania. Baada ya vita yao na Wamarekani, waliwekeza kwenye kilimo. Wakapata mtaji, mwaka huu wawekezaji kutoka nje ya nchi wameingiza dola bilioni 10 kuwekeza katika viwanda.

Sitanii, nimekumbuka bajeti yetu ya mwaka 2018/2019 yenye maudhui ya “Bajeti ya Viwanda”. Nakiri imepunguza kodi hapa na pale, ila uhalisia hakuna kiwango kikubwa cha uwekezaji katika sekta mtambuka kama kilimo inayoonekana. Ndiyo, nakubali tumewekeza katika umeme na reli, ila uwekezaji huu unapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika kilimo.

 

Bajeti ya kilimo imeshuka kutoka Sh bilioni 267 hadi Sh bilioni 220 hivi. Kushuka huko kwa bajeti, kukichanganyikana na uwezo wa waziri mwenye dhamana na kilimo anayenata, anayevaa suti saa 24 badala ya kuvaa magwanda akaenda shambani, mipango hii tunaweza kuikwamisha mwishowe.

Kwamba tutajikuta tunao umeme wa kutosha, reli nzuri, ila hatutakuwa na mizigo ya kuzafirisha au malighafi za kuchakata kwenye viwanda kutumia umeme huo. Safu hii inazidi kuwa ndogo, lakini naomba kukushauri Rais John Magufuli kuwa tafadhali unda “JESHI LA KILIMO” na lisimamiwe na waziri mwenye mapenzi na kilimo – tufanye Mapinduzi ya Kilimo, kwa msingi huo tutaona matunda ya uwekezaji katika viwanda. Tukutane wiki  ijayo.