UKWAPUAJI MALI ZA CCM

 

Waziri Mkuu yumo

*Anunua shule ya Chama, abanwa, airejesha chapuchapu

*Yeye, Dk. Bashiru Ali wakwepa waandishi wa JAMHURI

*Wajumbe NEC wataka achunguzwe mali anazomiliki

*Wamlinganisha Rais Magufuli na Nyerere kwa uadilifu

 

 

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

 

Kamati ya Kufuatilia Mali za Chama Cha Mapinduzi (CCM), imegundua madudu ya kutisha katika jumuiya za chama hicho zilizofuja mali chama hicho, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Kati ya yaliyobainika, Jumuiya ya Wazazi ya CCM, inatuhumiwa kuuza shule za sekondari sita, ambako moja kati ya shule hizo, ameuziwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Majaliwa ameuziwa Shule ya Sekondari Nyangao iliyopo Lindi Vijijini.

Shule hizo zimeuzwa wakati wa utawala wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo (2012-2017), huku Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Jumuiya hiyo, Dk. Charles Tizeba, akitajwa kutoa baraka zake.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa wakati wa vikao vya Halmashauri Kuu Taifa (NEC) pamoja na Kamati Kuu (CC) vikiendelea jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Dk. Bashiru Ali, alipata fursa ya kuwapitisha wajumbe katika maudhui ya taarifa ya Kamati yake. Alitumia saa 4 kuwasilisha muhtasari wa taarifa aliyoiandaa.

“Unajua Kamati iliwasilisha mambo mazito, ambayo vikao viliazimia ipelekwe kwenye Kamati ya Maadili, ili sasa wahusika washughulikiwe na chama… sijajua huko kwenye Kamati ya Maadili wataanza kushughulikiwa lini,” kimesema chanzo chetu.

Kwa nyakati tofauti wajumbe wanane wa NEC wamezungumza na JAMHURI na kuliambia habari za ‘kutisha’ kuwa kati ya mali za Chama zilizokwapuliwa, Waziri Mkuu Majaliwa aliuziwa shule hiyo.

“Kwa kweli kwenye kikao ilikuwa kama tumepigwa ganzi taarifa hiyo ilipotajwa. Tulikuwa tunaangaliana kwenye nyuso na kumwangalia Waziri Mkuu Majaliwa ikawa kama anatokwa jasho vile. Kamati ilitoa mapendekezo kuwa Waziri Mkuu achague kati ya kurudisha shule au kuachia Uwaziri Mkuu.

“Kamati ikasema Waziri Mkuu ameamua kuirudisha shule hiyo kwa CCM na kuendelea na Uwaziri Mkuu… kwa kweli tulishangaa ujasiri wa Kamati, lakini tukamfurahia mwenyekiti wetu.

“Tumemfurahia Rais Magufuli – Mwenyekiti wetu, anarejesha enzi za Mwalimu [Julius] Nyerere. Mwalimu Nyerere alikuwa hafichi maovu. Hata kama ungekuwa mtu wake wa karibu kiasi gani. Ukikosea anakwambia umekosea. Alifikia hatua akaandika kitabu cha TUJISAHIHISHE. Kitabu hiki kinasisitiza uadilifu na kukubali kukosolewa,” amesema mmoja wa wajumbe wa NEC.

“Bado nina hamu ya kutaka kujua hii shule Waziri Mkuu aliuziwa shilingi ngapi? Ukarabati aliofanya alitumia shilingi ngapi? Fedha hizo alizipata wapi yeye kama mtumishi wa umma? Je, kiasi alichonunua shule na kuikarabati kinaendana na pato lake la mshahara wa kila mwezi? Je, ni shule hii pekee aliyonunua au ana miradi mingine yenye utata? Kama ndiyo, fedha anazipata wapi? Kama hakuna maelezo ya wazi, basi tukubali Rais Magufuli kazi anayo,” amehoji mjumbe mwingine wa NEC.

 

Habari za uhakika kutoka ndani ya CCM zinasema kwamba mapendekezo ya kamati ya Dk. Bashiru, yalimtaka Waziri Mkuu, kujipima kama anaweza arudishe shule au mamlaka ya uteuzi, itengue uteuzi wake.

“Mpaka ninavyozungumza nawe hapa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amerudisha shule haraka bila kutoa nafasi kwa mamlaka ya uteuzi. Aliandika barua kwa kamati akisema amerudisha shule na irudi kuwa mali ya CCM.

“Sijui kama Waziri Mkuu hakuwa anajua kwamba ananunua mali ya CCM, ila sasa amerudisha tena akiwa ameshaifanyia marekebisho makubwa shule hiyo, napo kuna maswali. Ameongeza majengo mapya pamoja na kuongeza madarasa,” kimesema chanzo chetu.

Waandishi wa gazeti la JAMHURI wamesafiri hadi Lindi Vijijini, eneo la Nyangao ilipo shule hiyo inayodaiwa kuuzwa kwa Waziri Mkuu Majaliwa, na kukuta imefanyiwa ukarabati mkubwa, na ikapandishwa hadhi kuwa na kidato cha tano na sita.

“Hii ni shule ya Waziri Mkuu, amekuwa anakuja hapa mara kadhaa, hata wanafunzi wamewahi kwenda bungeni kumtembelea… awali ilikuwa shule ya Jumuiya ya Wazazi, ghafla tukasikia fununu kwamba imeuzwa kwa Kassim Majaliwa,” kimesema chanzo chetu shuleni hapo.

JAMHURI limewatafuta wahusika wote wanaotajwa kuhusika na ‘ufujaji’. Waliopatikana wameruka kimanga na kusema hayo ni mambo ya jumuiya hivyo wasiulizwe kama watu binafsi.

Jitihada za gazeti la JAMHURI kumpata aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Bulembo hazikuzaa matunda. Ijumaa iliyopita tulipata taarifa kwamba alikuwa njiani kwenda msibani Nzega ambako alikwenda kumsitiri mama wa Mbunge wa Jimbo la Nzega, Hussein Bashe.

Baada ya jitihada za kumpata azungumzie kashfa ya kuuza mali za chama, hasa shule za wazazi zinazomilikiwa na jumuiya hiyo kutozaa matunda, waandishi wa JAMHURI walimtafuta binti yake, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum, Halima Bulembo, naye aliahidi kumfikishia babaye ujumbe.

“Tuko njiani tunatoka Nzega mazishini, hata mimi mmenipata kwa sababu labda niko kwenye eneo lenye mtandao… baba yuko kwenye gari jingine ila nitamwambia akupigie,” Halima alimwambia mmoja wa wahariri wa JAMHURI.

Saa 24 baadaye, JAMHURI likamtafuta Bulembo bila mafanikio, na baada ya kurudi kwa bintiye, alisema hakuwa amemwambia labda mpaka Jumatatu [jana] ndiyo siku ataweza kumpata na kumfikishia ujumbe.

Kama ambavyo imekuwa vigumu kwa Bulembo kupatikana, jitihada za kumpata Waziri Mkuu Majaliwa hazikuzaa matunda, hata kwa kupitia kwa wasaidizi wake.

Jumamosi, wahariri wa JAMHURI, waliwasiliana na Katibu wa Waziri Mkuu, Raymond Gowelle, ambaye alitaka kujua sababu ya kumtafuta bosi wake, ambako baada ya kuambiwa aliahidi kumtaarifu.

“Unajua leo ni wikiendi, hata bosi leo yuko mapumziko… mimi leo niko ofisini ninafanya shughuli zangu za kawaida. Hivyo nitamwambia pindi nitakapoonana naye,” amesema Gowelle.

Baada ya kukwama kumpata kupitia kwa wasaidizi wake, JAMHURI lilimpigia simu Waziri Mkuu Majaliwa, lakini ikawa inaita bila kupokewa. Baadaye walimpelekea ujumbe wa maandishi (sms), lakini muda mfupi baada ya ujumbe huo kufika Jumamosi, simu yake ilipopigwa tena ikawa haipatikani.

JAMHURI, kama lingempata Waziri Mkuu, lingemwuliza maswali kadhaa ikiwamo, kwanini aliamua kununua mali za CCM? Alinunua shule hiyo kwa shilingi ngapi? Wakati ananunua alijua ni mali ya CCM, au mali binafsi ya Bulembo? Fedha za kununua shule hiyo amezipata wapi? Pamoja na maswali mengine mengi.

JAMHURI limemtafuta Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas na kumweleza kuwa linamtafuta Waziri Mkuu kuthibitisha kwanini amerejesha shule hiyo aliyoinunua kihalali, na Dk. Abbas akasema: “Hilo ni suala binafsi naomba mmtafute yeye mwenyewe au mmpate kupitia wasaidizi wake, kama Serikali siwezi kulisemea.”

JAMHURI limezungumza na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuhusu suala hili:

 

 

 

JAMHURI: Tumepata taarifa kuwa watuhumiwa wa uchotaji wa mali za chama, akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyerudisha shule ya chama aliyokuwa amenunua, wengi wanarudisha mali za chama kwa sasa. Ni mali kiasi gani zimerejeshwa hadi sasa na wahusika ni kina nani?

Polepole: Mbona majibu ninayo… ninaanza kama ifuatavyo, kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa, kilichoketi tarehe 28-29 Mei, pamoja na mambo mengine kilipokea taarifa ya uhakiki wa mali za chama uliofanywa na Tume ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Na kikao kimejadili taarifa ile ambayo imepewa hadhi ya kuwa taarifa ya ndani mpaka vikao vya chama vyenye dhamana ya usalama na maadili vitakapoketi na kutoa mapendekezo kwa namna ambavyo vikao vitaona inafaa, kwa sababu kilichofanyika ni ‘findings’ za Tume.

Tume [Kamati] haihukumu, haitafuti mwizi baada ya [hapo] mapendekezo ya tume yote, yanaanza kufanyiwa kazi. Mapendekezo yenye sura ya jinai au vitendo vyovyote vinavyokiuka misingi ya Chama Cha Mapinduzi, mapendekezo haya yatakwenda kwenye Kamati ya Maadili na Usalama. Vikao hivyo viko chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula.

Vikao hivyo vitaamua taarifa ipi iende kwa umma na taarifa ipi ibaki kuwa taarifa ya ndani kwa utaratibu wa chama chetu.

JAMHURI limemtafuta Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru kuzungumzia tuhuma hizi bila mafanikio. Hata baada ya kumpelekea ujumbe mahsusi kupitia simu yake ya mkononi na kwa watu wake wa karibu, hakujibu. “Dk. Bashiru si kwamba hajibu maswali yenutu, hata sisi tuliompelekea salaam pongezi hakutujibu,” amesema mmoja wa wana-CCM.

 

 

 

Desemba, mwaka jana, Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli aliitaka Jumuiya ya Wazazi ya CCM kuzirejesha serikalini shule za sekondari ambazo imeshindwa kuziendesha ziboreshwe na zitoe elimu bora kwa wanafunzi.

Alitoa agizo hilo kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Jumuiya ya Wazazi mjini Dodoma. “Uongozi utakaokuja na ninyi Jumuiya ya Wazazi kama mtaona inafaa kwa baadhi shule ambazo mmeshindwa kuziendesha na hasa katika shule hizi 54 mkaamua shule 10 au 20 kwamba zichukuliwe na Serikali tutazichukua kwa ajili ya kufidia hayo madeni,” alisema Rais Magufuli.

Alisema mpango wa Serikali kutoa elimu bure kwa shule zake umeleta changamoto kwa shule zinazomilikiwa na watu binafsi kukosa wanafunzi kwa kuwa wengi wanaenda shule za Serikali ili kukwepa gharama za masomo.

Jumuiya ya Wazazi inamiliki miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii na imewekeza katika sekta ya elimu ambako ina shule 54 za sekondari na chuo kimoja cha Ufundi cha Kaole mkoani Pwani. Kinatoa Astashahada ya Kilimo na Mifugo.

Mchakato wa kuzirejesha baadhi ya shule za jumuiya hiyo serikalini umeanza kwa Shule ya Sekondari ya Omumwani iliyoko mkoani Kagera.

“Mwaka jana [2016] tulipoenda Kagera baada ya tetemeko nilitembelea Shule ya Omumwani na nikaona huduma nzuri ilizokuwa inatoa kwa wanafunzi waliokuwa shule zao zimeanguka. Nikatoa maagizo mlikubali kupokea wanafunzi wa serikali na shule mbalimbali katika mji wa Bukoba na mkaanza kuwahudumia pale.

“Baadaye nikawaomba kwamba shule sasa tuichukue iwe ya Serikali, mlinikubalia tumeichukua, tukabaki namna ya kutafuta fedha za kulipa. Wiki iliyopita tumelipa hizo bilioni 1.7,” alisema Rais Magufuli.

Kamati ya Dk. Bashiru

Kamati iliyoundwa kufuatilia mali za CCM imebaini mambo mazito ambayo yanatajwa kuwa yatasababisha baadhi ya wanachama na viongozi kutafakari upya uhalali wa nafasi zao ndani ya chama hicho.

Mmoja wa wajumbe kwenye kamati hiyo ameliambia JAMHURI kuwa mambo waliyokutana nayo ni ya ‘kutisha na kushangaza’.

Kamati hiyo iliyoundwa na wana CCM tisa, wakiongozwa na Dk. Bashiru, iliundwa na Mwanyekiti Rais Magufuli, Desemba 20, mwaka jana mjini Dodoma.

Wajumbe hao ni Walter Msigwa, Albert Msando, Galala Wabanhu, Albert Chalamila, William Sarakikya, Komanya Kitwara, Dk. Fenella Mukangara na Mariam Mungula.

Baadhi ya mambo yaliyokwishabainika ni kuuzwa kwa viwanja vingi katika maeneo karibu yote yaliyokwishatembelewa na Kamati hiyo.

“Lakini jambo la kushangaza ni kuona hata majengo ambayo kwa asili ni mali ya CCM, sasa yana hati miliki za watu binafsi,” chanzo cha habari kililieleza JAMHURI wakati kamati hiyo ikikaribia kukamilisha kazi yake.

Ulitolewa mfano wa nyumba iliyopo wilayani Kinondoni, Dar es Salaam ambayo ingawa ni mali ya CCM, sasa ni mali ya familia ya kada aliyefariki dunia siku za karibuni.

“Kila mtu alidhani ile nyumba ni mali ya (anamtaja jina), amefariki dunia, familia inaendelea kuishi humo, sijui hili litaamuriwa vipi,” kimesema chanzo chetu.

Matukio kama hayo yametajwa kuwa mengi katika wilaya zote za Dar es Salaam na katika mikoa ambayo kamati hiyo imetembelea ikitekeleza majukumu yake.

“Arusha tumekuta jengo moja ambalo ni mali ya CCM kuanzia enzi za TANU likiwa limemilikishwa kwa familia na sasa kuna hoteli…mambo mengi yanatisha,” amesema.

Pamoja na suala la nyumba na viwanja, eneo jingine ambalo wajumbe wamebaini ufisadi mkubwa ni kwenye nyumba na maeneo yaliyopangishwa kwa wafanyabiashara. Maeneo hayo ni pamoja na viwanja vya kuegesha magari, vibanda vilivyojengwa kuzunguka viwanja vya mpira na maeneo mengine ya wazi.

Inaelezwa kwamba baadhi ya watumishi wa CCM wamehodhi maeneo hayo kwa kulipa kiasi kidogo mno cha fedha kwa CCM, ilhali wao wakiwa wameyakodisha kwa wafanyabiashara na wanalipwa fedha nyingi.

“Pale Arusha tumekuta mpangaji analipa Sh 400,000 kwa mwezi kwa chumba, lakini zinazopelekwa CCM ni Sh 30,000 tu,” kimesema chanzo chetu.

Katika uhakiki huo, eneo jingine linalotajwa ni la vitega uchumi ambavyo vililetwa kuisaidia CCM kujitegemea, lakini kwa namna isiyoeleweka chama hicho kimejikuta kikiwa hakina umiliki wowote.

Chanzo chetu kilisema baadhi ya vitega uchumi hivyo vipo kwenye nyanja ya mawasiliano ambako kampuni moja kubwa ya simu ambayo awali CCM ilikuwa ikiimiliki, sasa iko mikononi kwa watu binafsi.

“Kampuni hii ililetwa nchini kama sehemu ya kuisaidia CCM kujiimarisha kiuchumi, lakini baadaye umiliki wake haueleweki ulihama vipi CCM…hili nalo litatolewa majibu kamati itakapokuwa imemaliza kazi yake,” kilisema chanzo chetu.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa eneo jingine ambalo limeleta mshituko ni la fedha wakati wa uchaguzi, hasa Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Rais.

Kuna taarifa kuwa baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM kwa miaka mingi wametumia kipindi cha Uchaguzi Mkuu kuwa cha ‘mavuno’ ya fedha na mali kutoka vyanzo mbalimbali – ndani na nje ya nchi.

Imeelezwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa ‘marafiki wa CCM’, kimekuwa kikiishia mifukoni mwa wachache. Fedha nyingi zimekuwa zikikusanywa kutoka kwa ‘marafiki wa CCM’ bila hata maelekezo kutoka ngazi za juu za chama hicho na hivyo kuwanufaisha wachache.

 

“Walikuwa wakipita huku na kule ndani na hata nje ya nchi wakikusanya fedha kwa kigezo kuwa zinatakiwa kusaidia ushindi wa CCM. Fedha nyingi sana zimetolewa kwa njia hiyo na kuishia mifukoni mwao wakati CCM yenyewe ikiwa haina taarifa za makusanyo hayo.

“Kuna watu wamejipatia fedha nyingi sana kwa njia hiyo, na tunapendekeza ikiwezekana ziletwe kwenye chama au zirejeshwe kwa wenyewe kwa sababu mchezo huo umechafua taswira ya chama.

Rais Magufuli alikutana na kamati hiyo Desemba 28, mwaka jana Ikulu jijini Dar es Salaam na kuwataka wajumbe kufuatilia na kuhakiki mali zote za chama, kumhoji mtu yeyote ambaye atahitajika kutoa taarifa juu ya mali za chama na kubaini thamani ya mali, mahali zilipo, makusanyo ya mapato na wanaozishikilia au kutumia mali hizo.

Alitoa mwito kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zote zinazohusu mali za chama kwa kamati hiyo, na akaagiza watakaoitwa kuhojiwa waitikie mwito.

 

 

 

 

 SOMA GAZETI LOTE LA JAMHURI HAPA

 

Please follow and like us:
Pin Share