Mpendwa msomaji wa makala ya Katiba Mpya Tanzania Mpya, nilipoanza kuzungumzia uhuru wa kutoa maoni na suala la Muungano, nilianza kwa kufuatilia historia ya nchi yetu angalau kwa wale wasioijua historia ya Muungano ili wapate kuijua vizuri na kuona ni wapi tulitoka, tulipo na tunakoelekea, lakini pia si tu tunaelekea wapi bali tunaelekea wapi kwa namna gani.

Historia inaonesha wazi kwamba ushiriki wa Watanzania katika kuziunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar ulikuwa hafifu. Uamuzi mwingi kuhusu Muungano ulifanywa na chama tawala kilichokuwa chama pekee wakati katiba ya mwaka 1977 inatengenezwa.

Kutokana na ushiriki mdogo, Watanzania wengi wamekosa uhusiano wa moja kwa moja na Muungano wao. Hauonekani kuwa wa Wazanzibar wenyewe wala wa  Watanganyika. Jambo hili la Muungano limekuwa likiwashughulisha mno wenzetu wa Zanzibar hadi kufikia hatua ya kuchoma makanisa na kufanya fujo zisizo na uhusiano wowote na Muungano. Ukijiuliza  uhusiano uliopo kati ya makanisa na Muungano unakosa maana halisi.

Tujiulize, kweli kuna sababu za msingi za kuvunja Muungano wetu? Dunia tunayoishi inapokea mabadiliko makubwa yanayochangiwa na mambo mbalimbali hasa  utandawazi. Kuungana limekuwa jambo la kila nchi kuweka mahusiano ya ushirikiano katika mambo mbalimbali yanayohusu taifa. Tunayo mifano hai kama Marekani na Uingereza tunakoshuhudia Muungano uliotengenezwa kwa sheria nzuri zinazoeleza kila jambo kuhusu Muungano wao.

Niutumie mfano rahisi wa ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioanza na nchi tatu, baadaye zikaongezeka mbili na kufikia nchi tano sasa zilizoungana katika mambo mbalimbali yakiwamo masuala ya soko la pamoja, ulinzi, ajira; baadaye yatakuja mambo kadha wa kadha kama sarafu moja, ardhi na masuala ya siasa moja. Sasa niseme moja kwa moja kwamba kama juhudi ni kuunganisha nchi hizi za Afrika Mashariki, kuna sababu gani ya kuvunja Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar?

Kufanya hivyo ni sawa na kusema kuna wajenzi wanaojenga ngome kubwa ya Muungano wa Afrika Mashariki, lakini pia kuna wabomoaji wanaobomoa kuta zilizokwishajengwa. Kinachotokea ni kurudisha nyuma dhana nzima ya Muungano.
 Pia tulitazame kwa upande mwingine suala la Muungano kufanywa kuwa jambo la watu Fulani, kama nilivyotangulia kusema mwanzoni kwamba Muungano ni zao la chama tawala. Hata kama sikuwapo kipindi cha Muungano, historia imetueleza wazi jambo hilo lilivyotokea hadi  hapa tulipo.

Suala la Muungano limefanywa kuwa jambo la watu fulani kwa sababu kuna kitu kinachoitwa mwafaka. Sipendi kuzungumzia mno mwafaka huu kwani sina uhakika sana na yaliyomo kama ni matakwa ya Wanamuungano au ndiyo yale yale yaliyofanyika mwaka 1977 wakati wa kuandika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Niseme wazi kwamba mwafaka si Katiba. Nasema si Katiba kwa sababu kumekuwa na fikira kwamba matatizo ya Muungano yamemalizwa na mwafaka uliofanywa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kwa kushirikiana na wahisani wa mwafaka.

Bila kupindisha maneno, niseme kwamba CCM, CUF na wahisani wa mwafaka si watu pekee wanaoweza kutoa hatima ya Muungano wetu, bali kuna kundi kubwa la Watanzania kama watapewa fursa ya kutoa maoni kwa kujadili jinsi wanavyopenda Muungano wa nchi zao uwe, litakuwa jambo jema. Hawa watapata fursa ya kujadili kero zote zinazohusu Muungano.

Lakini si kujadiliwa tu, bali tutapata kujua fikra halisi za Watanzania kuhusu Muungano zikoje, ili angalau kupata picha halisi ya Muungano tunaoutaka. Kiuhalisia na jinsi historia inavyotueleza, hapajawahi kuwapo maoni ya Watanzania kuhusu Muungano wao.

Muungano umetawaliwa na dhana za kisiasa zilizopita kiasi na kusahau misingi ya kisheria ambayo ndiyo inayoweka taratibu zote kuhusu Muungano uweje kwa maslahi ya Watanzania wote. Hivyo ni rai yangu kwa Watanzania wote na Tume ya kukusanya maoni kwamba ni jambo la msingi Watanzania kupata fursa ya kusema juu ya Muungano, katika kueleza namna ya kuwa na Muungano wenye tija na ulio na nia ya dhati ya kujenga Taifa imara linalojali maoni ya wananchi wake.

Pia napenda kuwaomba Watanzania wenzangu kuwa Muungano si dhambi, bali ni jambo la kheri kabisa lililojengwa katika msingi wa upendo na ushirikiano. Ninaamini kuungana ni rahisi kuliko kutengana. Kuna sherehe katika kuungana na msiba katika kutengana. Kutengana kutatugharimu kuliko kuungana. Badala yake tuboreshe palipo na udhaifu.

Tukutane wiki ijayo katika makala ya Katiba Mpya Tanzania Mpya wakati nitakapozungumzia suala la ardhi kama sehemu muhimu kwa Taifa na Katiba ya sasa, inavyoweza kutoa haki sawa katika umiliki wa ardhi na uwekezaji.