Nakumbuka mchakamchaka na mapigo ya bendi ya shule enzi za elimu ya msingi. Mwalimu wa michezo, mwalimu wa zamu na wengine waliokuwa wakipenda ukakamavu walikuwa mstari wa mbele kwenye shughuli hizo kabla ya kuingia darasani.
Kwa upande mwingine, siku ilikuwa na kawaida ya kufungwa kwa michezo, siku moja moja likitumika gozi la ng’ombe, yaani mpira wa soka ulionunuliwa dukani, na ni wateule wachache wasiozidi 30 walioucheza. Akina dada hawakuwa na bahati sana, kwa sababu michezo yao iliishia kuwa ya kienyeji kama kuruka vijumba na kamba, na kuwashangilia wavulana.
Mchakamchaka na kucheza gwaride pamoja na soka ya ushindani kati ya shule moja na nyingine, vilijenga hamasa miongoni mwa wanafunzi, na ilileta ‘jeuri’ ya kweli kwa shule iliyoshinda mechi. Tulikuwa tukiulizwa kwenye gwaride na mchakamchaka; vijana mpo? Tukajibu, tupo, tupo kabisa, jeuri ya chama, yeeba!
Msingi huo wa michezo shuleni na kabla ya hapo mitaani ndiyo uliopo kwa mataifa mengi, lakini wenzetu wametilia maanani zaidi, kwa sababu ni wepesi wa kung’amua kwenye pesa na faida kiuchumi. Angalia leo jinsi nusu fainali ya michuano ya Euro 2012 inavyovuta hisia za watu si wa Ulaya tu, bali hata mabara mengine.
Magazeti ya kila siku na kwa namna ya pekee yale ya michezo yamejaza habari za Euro 2012 na vituko vya wachezaji, waamuzi na mashabiki, kwa sababu ni kitu kikubwa. Acha ujumla huo, taifa moja moja – chukulia Uingereza kwa mfano – wanaona fahari na jeuri kweli wanaposhinda mechi dhidi ya wengine.
Jeuri na furaha inaongezeka wanapotokea kupangwa au kuangukia kucheza na taifa lenye jina kubwa na kulifunga. Michuano hii imeamsha uzalendo wa aina yake hapa England, maana Jamhuri ya Ireland iliondoka kwa aibu ya mabao mengi ya kufungwa, Scotland na Wales hazikufuzu kushiriki, England – kaka yao mkubwa ikabaki kama mzazi.
Siku kabla ya mechi, siku ya mechi na baada ya mechi za England, ungeona magari yamepambwa kwa bendera yao – kitambaa cheupe chenye msalaba mwekundu. Si bendera ya Uingereza nzima maana hapo wanaona wanayeyusha ule ukuu wao – ni England si Uingereza.
Utawapenda wanapojadili uimara wa kikosi chao, hata kama kinashinda kwa bahati, kwa kuzuia mabao yaliyokwishaingia kwenye wavu, kwa kulaumiana kwenye uteuzi wa timu. Yote hayo ni kabla na baada ya matukio, lakini kwenye mechi wanakuwa wamoja dhidi ya ‘adui’, na adui si mwingine bali timu wanayomenyana nayo.
Walifurahi na kujisikia sana walipotoka sare na Ufaransa, wakasema Wafaransa walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kutwaa kombe na hawajawahi kufungwa kwa muda mrefu. Walicheka, wakanywa pombe na kuvuta sana sigara.
Walipokuja kuwafunga Waswidishi na wenyeji wenza Ukraine, London ililipuka. Magazeti, televisheni na kila kituo cha redio neno likawa England inavyofanya vizuri; jinsi kocha wao Roy Hodgson alivyo mzuri kwenye kazi, akipewa nafasi ya juu sana, ngazi chache kutoka kwa waziri mkuu.
Wachezaji wao, mmoja mmoja huko Ukraine na Poland wakawa wanaitisha mikutano ya waandishi wa habari, wakiwa na bendera ya nchi yao na kueleza jinsi watakavyocheza vizuri. Kwamba wapo kwa ajili ya kushinda na kulitangaza jina la Uingereza. Ni bahati mbaya nimeandika makala haya kabla ya mchezo wa robo fainali kutokana na sababu za kiufundi, lakini habari ndiyo hiyo.
Uingereza inatumia soka kujikuza sana kiuchumi; ligi kuu ya England ndiyo inayopendwa na kufuatiliwa kuliko zote kote duniani. Ya Hispani ni ya pili. England imewekeza vilivyo kwenye soka kuanzia vituo vya kufundisha wanamichezo tarajiwa tangu wakiwa watoto hadi miundombinu yenyewe.
Viwanja ni vingi, klabu na timu ni nyingi na hata mabilionea wa kigeni wanaleta pesa zao na kumwaga kwenye soka hapa England, baada ya nchi yenyewe kutandika jamvi la kuwafaa. Serikali inavuna kwenye kodi si kawaida. Kiutalii inapata mapato makubwa maana kila mwaka mamilioni ya watu wanaingia kwa ajili ya ligi na michezo mingine.
Wachezaji wanauzwa kwa bei kubwa ajabu utafikiri ni kiwanda au mashine fulani hivi, lakini pia heshima ya nchi, jeuri yake mbele ya nyingine inakuwa juu, yaani ni kama wako kwenye paa la dunia.
Biashara zinazoendeshwa kwa ajili ya soka tu zinaiingizia nchi mabilioni ya paundi, ajira zinatengenezwa za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, halafu unakuta watu wana kipato kikubwa. Lakini ukiangalia kazi wanayofanya ni ya kawaida, isiyo ya nguvu na wanaburudika kweli kweli.
Huko ndiko kutumia vipaji, rasilimali na maliasili kwa maendeleo ya taifa, kutumia michezo kama ngazi za kulifanya taifa kung’aa mbele ya mengine. Michezo imedhihirisha uzalendo wa Waingereza – England kwa namna ya pekee hapa nilipo, na wanachuma pesa taratibu bila wasiwasi, wakati sisi huko tunakimbizana na mambo magumu kupita kiasi, na bado hatutoki.
Hebu tutafakari na kuangalia fursa kama hizi ambazo zinatuinua kiuchumi, lakini pia zinakuza uzalendo, sifa ya nchi na jeuri ya chama, yeeba. Alamsiki.