Wiki iliyopita niliandika makala kuhusu fikra zinavyoweza kukukomboa kiuchumi. Katika makala yale nilieleza kuwa ili kufanikiwa kibiashara na kiajira tunahitaji hamasa kuliko hata kubadilisha siasa zinazotawala na Katiba mpya. Nilisema mtu namba moja wa kuukomboa uchumi wako ni wewe mwenyewe.
Asilimia kubwa ya wasomaji wamekubaliana nami kuwa nimeunda hoja vizuri na hili linathibitisha kuwa wengi wanakubaliana na haja ya kuwapo na mjadala huu ambao utaziamsha na kutafakarisha bongo zetu.
Hata hivyo, kama ilivyo kawaida nimeendelea kukutana na kundi la wasomaji wanaoamini kuwa pasipo siasa mtu hawezi kufanya chochote cha maana. Mimi nimekuwa nikiamini kuwa Serikali haiwezi kufanikiwa pasipo watu, lakini watu wanaweza kufanikiwa kiuchumi pasipo hata kuwapo Serikali. Imani yangu inapingana na watu wengi ambao matumaini yao kiuchumi yamo mikononi mwa siasa na wanasiasa.
Kimsingi, nakubaliana kuwa siasa safi ina mchango katika ukombozi wa kiuchumi. Lakini napinga kwa nguvu zote utamaduni wa Watanzania wengi kuendekeza uvivu na kutowajibika kibinafsi kwa kuzipa mzingo siasa kwa kila jambo. Nimelazimika kupanua mjadala wa wiki iliyopita kufuatia baruapepe aliyoniandikia msomaji aliyejitambulisha kwa jina la Mwabungu P. L.
Msomaji huyo ameandika hivi (nanukuu):“Rejea Jamhuri. J’ne Julai. 16, 2013 na A. Sanga “Fikra na uchumi……..” Hakika uko sahihi. Hata hivyo kupata Taifa unalotaka kuchora ni muhimu mfumo wa utawala ujali misingi ya kidemokrasia sio kibomokrasia. Uendeshaji wa utawala kwa kutegemea juhudi binafsi za watawaliwa hatima yake ni unyama, kwamba aliye na nguvu ndiye mla nyama”. Kinachotakiwa ni uongozi unaoweza kusimamia nguvu hizi za kishetani na kuleta uwanja sawa kwa wote.”
Msomaji aliendelea kuandika; “Si vizuri kuwalaumu waTz kuwa tumezembea kifikra ndiyo maana tuna maisha magumu; kwani haya ni matokeo ya uongozi mbovu. Kumbuka maendeleo tunayoshabikia sasa ni matokeo ya mlolongo wa historia ambayo huonesha matokeo hasi au chanya endapo uelekeo fulani utazingatiwa ama kupuuzwa. Rejea ‘growth of nations, renaissance, reformation, age of discovery, age of absolutism etc” mwisho wa kumnukuu.
Kwa dhati kabisa ninapenda kumpongeza msomaji huyu kwa namna alivyotoa maoni yake kwa kujenga hoja nzuri na kwa umakini mkubwa. Nimeamua kunukuu ujumbe wake kwa sababu ni moja ya maoni adimu sana na yanayoonesha dhahiri kuwa msomaji huyu ni mtu mwenye tafakari ya kina na mfuatiliaji mzuri wa mambo.
Ninachokubaliana na wasomaji wengi waliochangia (ambao sijanukuu michango yao kutokana na uhaba wa nafasi) ni kuwa wanasiasa wamechangia kwa sehemu kubwa uwepo wa hali mbaya za kiuchumi miongoni mwa Watanzania. Wameifikisha jamii ya Waafrika hapa ilipo kutokana na kukosa maono endelevu, utashi wa kisiasa, migongano ya kimaslahi, ulafi wa madaraka na uzembe katika kusimamia rasilimali za nchi kwa maslahi ya umma.
Vyama vya siasa vimepewa kipaumbele badala ya maslahi ya kitaifa. Kwa ajili ya matumbo yao, wanasiasa wamekuwa tayari kuitoa kafara kwa kuinyonga demokrasia na kumwaga damu za watu. Kushindwa kuongoza kwa wanasiasa kwa dhamana za kimadaraka walizopewa kumeleta shida na migogoro mikubwa katika jamii.
Nisichokubaliana nacho ni mtazamo wa baadhi ya wasomaji (ambao upo miongoni mwa wanajamii wengi) kuona kuwa umaskini wa wanajamii kwa asilimia 100 ni matokeo ya kushindwa kwa wanasiasa. Ninakataa kusema kuwa wanajamii hawahusiki japo kwa asilimia kidogo kuhusu umaskini wao.
Yapo mambo ambayo ni kweli mwananchi hawezi kufurukuta kuyafanya kama waliopewa dhamana ya uongozi wa kisiasa watakuwa wanafanya ‘madudu’. Lakini pia kuna rundo la mambo ambayo mwananchi wa kawaida anatakiwa kufanya mwenyewe kwa ajili ya ustawi wake mwenyewe.
Kuna kitu kwenye taaluma ya uchumi kinaitwa kanuni na nadharia za uchumi (theories and laws of economic). Ili kanuni hizi ziweze kufanya kazi na kueleweka huwa kunalazimika kuwekewa kitu kinachoitwa fikra ombwe (assumptions). Katika mjadala huu ninalazimika kukopa taaluma hiyo ya kiuchumi ili tutengeneze ‘assumptions’ zitakazotusaidia.
Hebu sasa tutwae ‘assumptions’ kuwa chama kinachoungwa mkono na wananchi wengi kimeingia madarakani (mbali na chama kilichopo madarakani kwa sasa) na kimeanza kutekeleza sera na ilani zake (ambazo zinadhaniwa ni nuru na tumaini la kweli kwa maendeleo ya mwananchi maskini katika taifa).
Kwa picha hiyo ya chama chenye ukombozi kamili kuwapo madarakani kuna maswali ya msingi tunapaswa kujiuliza. Je, Serikali itafanya kila kitu kwa ajili ya kuyakomboa maisha ya mtu mmoja mmoja? Inafahamika kuwa wajibu wa Serikali bora ni kuandaa mazingira mazuri ya mwananchi kujikwamua kiuchumi. Je, hayo mazingira yakishaandaliwa ni nini wajibu wa mwananchi husika?
Ikiwa tunakubaliana kuwa mwananchi wa kawaida anao wajibu wa kufanya hata kama Serikali bora itakuwapo madarakani, kuna maswali mawili yanazaliwa tena hapo.
Mosi ni, je, ni mambo gani ambayo mwananchi hawezi kufanya bila Serikali kumsaidia? Pili ni, je, ni mambo gani ambayo mwananchi anaweza kuyafanya kwa ustawi wake bila hata mkono wa Serikali? Sasa swali la mwisho ambalo ndiyo msingi wa mjadala huu ni, je, ni nini kinawazuia watu wengi kufanya mambo ambayo hayahitaji mkono wa Serikali kwa ajili ya ustawi wao?
Hebu tuangalie mfano ufuatao halafu tuone nafasi ya ‘wanasiasa walioshindwa’ na wajibu wa mwananchi maskini katika mazingira ya ‘siasa zilizoshindwa’. Chukulia walimu wawili wa Shule ya Msingi Songambele (jina la shule limetumika kama mfano tu) ambao wote walianza kazi mwaka mmoja, wanaishi katika mazingira yanayofanana, wote wanafamilia (mke na watoto wawili kila mmoja) na wote wanalipwa mshahara wa daraja moja, ambao ni Sh 246,000.
Kwa upande wa wanasiasa tunaweza kusema kuwa ni uzembe na uonevu mkubwa kumlipa mwalimu mshahara mdogo kiasi hicho katikati ya nchi iliyojaa utajiri na rasilimali kedekede. Pia ni suala linalokatisha tamaa kusikia wanasiasa wakisema kuwa Serikali haina pesa ya kuongeza mishahara wakati wameshindwa kudhibiti uvujaji na wizi wa mapato ya Serikali tangu Serikali Kuu hadi katika Serikali za Mitaa.
Wanaochukizwa na hali kama hizi (hata mimi ninachukizwa ingawa naweza kutofautiana na wengine kuhusu suluhisho lake), kimsingi wana mapendekezo mengi kuhusu mkwamo huu kutegemea na vipindi vilivyopo.
Wakati wa uchaguzi mbiu hupigwa na wito hutolewa kwa wananchi kuikataa Serikali iliyopo madarakani kwa kukiondosha chama kinachotawala. Cha kujiuliza ni hiki: Je, ni kweli chama kilichopo madarakani ni chimbuko la mkwamo wa uchumi wako wewe binafsi kwa asilimia 100?
Pendekezo la pili (ambalo vuguvugu lake linazidi kushika kasi katika nchi nyingi za Afrika ikiwamo Tanzania) ni kuandikwa kwa Katiba mpya. Mimi ni mmoja wa Watanzania tunaolilia kuandikwa kwa Katiba mpya haraka iwezekanavyo. Lakini bado ninajiuliza swali hili: Je, Katiba mpya ndiyo suluhisho pekee la umaskini wetu? Pengine inaweza kuwa suluhu, hebu tuendelee kujadiliana.
Tumeshapeleka malalamiko mbele ya Serikali (ambayo baadhi ya wasomaji wameongea kwa hasira wakidai kuwa imeshindwa) kuhusu mishahara ya hawa walimu wawili wa Shule ya Msingi Songambele. Sasa tuwaangalie hawa walimu wawili namna wanavyokatumia hako kamshahara kadogo wanakokapata.
Mwalimu wa kwanza aliamua kutenga kiasi kadhaa kila mwezi na baadaye akanunua seti ya video kisha akajenga banda pale kijijini na kuanzisha biashara ya kuonesha video akitumia jenereta. Mwalimu wa pili yeye kila anapopata mshahara breki ya kwanza ni katika vilabu vya pombe kulewa na kutanua. Arudipo nyumbani huwa mweupe kabisa na kujikuta anabaki na miayo akiungoja kwa hamu mwisho wa mwezi ili mshahara uingie aendeleze ‘mzunguko wa kimaskini’.
Maendeleo na ukuaji wa biashara ya mwalimu wa kwanza vikamwezesha kupanua biashara hiyo hadi vijiji vya jirani na baadaye akajenga nyumba na kumudu kusomesha watoto wake. Huyu wa pili mambo yakawa yanamwendea vibaya miaka nenda rudi huku madeni yakimwandama (aliyokopa kwenye taasisi za kinyonyaji zilizowaingilia wafanyakazi wengi, hasa walimu), na kujikuta mwisho wa mwezi anapokea mshahara wa Sh 45,000 kutokana na makato ya mikopo!
Katika nukta hii ndipo nasisitiza kuwa tunatakiwa kujisaili. Inakuwaje wafanyakazi waliopo katika mazingira na vipato sawa watofautiane kimaendeleo? Wakati wanajamii wengine wakijikita katika ‘kupambana’ na ugumu wa maisha, kwa nini kuna wanajamii wengine (ambao ni kundi kubwa) wanaachwa nyuma na badala yale wanaishia kulalamika, kulaani na kunung’unika bila kuangalia ni kwa namna gani wamechangia uwepo wa hali mbaya wanazolalamikia?
Kwa mfano, Watanzania wengi tumekuwa wezi, ama niseme tusiothamini suala la muda. Wafanyakazi wameajiriwa ili wafanye kazi saa nane kwa siku lakini ukifuatilia utagundua kuwa wengi wanafanya kazi chini ya saa matano kwa siku. Makazini ni kawaida kuona watu wakipiga soga, wakijivuta kushughulikia majukumu yao bila kusahau utoro katika maeneo ya kazi.
Hivi karibuni kumezuka mtindo wa wafanyakazi wengi kuwa ‘bize’ na mitandao ya intaneti badala ya kufanya majukumu yao. Katika hizo intaneti ni bora hata wangelikuwa wanafanya mambo ya maana, lakini wengi wao utakuta wanazitumia kuangalia picha za ngono, wakijitahidi sana wanatumia ‘facebook’ japo wachache huzuga kuwa wanatazama akaunti za barua pepe zao.
Wanajamii kama hawa wanaopokea mishahara inayotokana na kodi za wavuja jasho, lakini bado wanaendeleza wizi wa rasilimali muhimu ya muda na kukwamisha uzalishaji, je, nao tuwatetee kuwa hawana makosa? Je, hawa unaweza kusema wamekosa utashi wa kisiasa na siasa safi?
Isisahaulike kuwa vitendo kama hivi vinafanyika kuanzia serikalini hadi kwenye kampuni na taasisi binafsi. Si huko tu, watu wanafanya wizi na uvivu hata katika kazi zao binafsi. Mtu anakwenda shambani kulima lakini analima kivivu na baadaye anawahi kijiweni ama katika maeneo ya pombe. Je, matatizo kama haya yanastahili kushikishwa ‘ugoni’ kwa wanasiasa?
Kimsingi, nimelazimika kuuleta uchambuzi huu katika wiki hii tofauti na mpangilio niliokuwa nimeukusudia kwa sababu ya mambo makuu mawili.
Kwanza, nimelazimika kusisitiza haja yangu ya kujadili wajibu wa wanajamii (kama mtu mmoja mmoja) katika mkwamo huu, kwa sababu kung’ang’ana na wanasiasa itakuwa ni kuzunguka mduara ambao kila siku tunaucheza, yaani kuwaandika na kuwalaumu wanasiasa.
Pili, ni kusisitiza haja ya kujadili bila kupendelea wala kujisahau kuhusu wajibu wa mwananchi kwa maendeleo yake mwenyewe.
Ninadhani kuwa kama hatutaanza kujenga utamaduni wa kutafakari wajibu wetu kwa maendeleo yetu tutarithisha imani za uzembe, uvivu na utegemezi kwa kizazi hiki na kijacho. Tukifanya hivyo tutakuwa na kizazi kitakachokuwa kinasubiri ‘mjomba CCM, mjomba CUF ama mjomba Chadema’ kwa ajili ya kufanyiwa kila kitu.
Kitu cha kufahamu ni kuwa katika mkwamo wa kiuchumi anayehusika kukukomboa ni wewe mwenyewe na uamuzi wako.
+255 719 127 901