Na Editha Majura, Dodoma
Ushawishi wa wabunge wa kutaka Bunge na Serikali, kumchukulia hatua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutokana na hatua yake ya kuita na kusikiliza hadharani vilio vya baadhi ya wanawake waliotelekezwa na kutopewa matunzo ya watoto, umegonga mwamba.
Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga, Jumatano jioni ya wiki iliyopita baada ya Bunge kukaa kama Kamati, muda mfupi kabla Bunge kuidhinisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, iliyowasilishwa bungeni na Waziri Prof. Palamagamba Kabudi, aliitaka serikali kutoa kauli thabiti dhidi ya Makonda, kuhusu zoezi hilo vinginevyo angetoa shilingi kwenye mshahara wa waziri.
Hata baada ya Prof. Kabudi kueleza kuwa si sahihi mahojiano hayo kufanyika hadharani, kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ilikuwa kampeni yenye lengo la kuhimiza wanawake kupeleka kwenye mamlaka husika malalamiko yao dhidi ya wenzi wao waliowatelekezea watoto, kwasababu waliotekeleza kazi husika ni wataalamu wa ustawi wa jamii.
Kutokana na Mlinga kutoridhishwa na maelezo ya Prof. Kabudi, Bunge likalazimika kujadili hoja yake iliyotaka serikali itoe kauli thabiti itakayokomesha Makonda, kufanya mambo kama alivyofanya kwenye zoezi hilo.
Kupitia mjadala huo, hoja nyingine zilijadiliwa, hivyo Makala hii imebeba hoj kadhaa ambazo zimejadiliwa bungeni. Jambo la kushukuru ni kwamba matangazo ya vipindi vya bunge, ukiondoa kile cha maswali na majibu si mubashara vinginevyo hakuna mwanamke angemfata mbunge kumuomba usaidizi endapo angepatwa na tatizo la kutelekezwa yeye na watoto.
Imedhihirika kuwa idadi kubwa ya wabunge wamekerwa na Makonda, kwa hatua zake dhidi ya wanaume wanaodatuhumiwa kutelekeza familia au watoto wao, imefikia hatua ya baadhi yao kutumia kauli za kuudhi dhidi ya watu wengine, na hakuna hata mbunge mmoja aliyeonesha nia ya kuzuia hali hiyo.
Ikumbukwe, wakati mjadala huo ukifanyika bungeni, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Faustine Ndungulile, walishaona kasoro katika zoezi hilo na kwa kwanyakati tofauti wakakosoa na kutoa ushauri wao ambao tayari ulishazingatiwa kwani kwa wakati huo shughuli hizo zilikuwa zikiendelea kwa faragha.
Kupitia mjadala huo, baadhi ya wabunge wamesema bayana bunge limchukulie hatua Makonda kwamba amedhalilisha muhimili huo, wakirejea taarifa zilizotokana na zoezi na kutangazwa kwenye vyombo vya habari kwamba kuna wabunge 47 wanatuhumiwa kutekeleza watoto wao.
Lakini taarifa hiyo haikutaja wabunge pekee, imetaja hata viongozi wa dini na hata viongozi wa kada nyingine. Hoja hapa ni je, wabunge wanapotumia ukumbi wa bunge kumshambulia Makonda na kutaka awajibishwe kwa kutaja idadi yao katika sakata hilo, watu wasiokuwa na majukwaa kamba bunge wanastahili kutendewa hayo?
Ingeeleweka ikiwa wabunge wangechukulia tukio hilo kama chachu ya kurekebishana. Hata kama hatua za kurekebishana zingefanywa kwa faragha, ingetosha kuleta taswira kwamba wapo tayari kuwekana sawa badala ya kushambulia na kudai wamedhalilishwa na wanaowakosoa.
Kiongozi ni kioo cha jamii, hivyo kiongozi anayezaa kisha kutelekeza mtoto au familia anawafunza nini anaowaongoza? Hivi aliyedhalilisha muhimili katika suala hili ni Makonda au wanaotuhumiwa (ikiwa tuhuma dhidi yao zitathibitika).
“Umefanyika udhalilishaji wa mihimili mingine ya dola, kwa mfano wametajwa wabunge 47 wakati mtu alifanya hayo mambo kwa nafsi yake katika zoezi hilo wametajwa watuhumiwa kwa ubunge wao, ni zoezi lililosababisha mtafaruku nchini na hata humu bungeni kuna watu hawakukaa sawa tangu zoezi lilipoanza, nataka commitment ya serikali kuhusu lini hali hii itakoma? natoa hoja ili bunge lijadili suala hili,” amesema Mlinga.
Wote walioshiriki mjadala huo wamekiri kuwa zoezi lililoratibiwa na Makonda, lilikiuka faragha ya watoto inayohitajika kwa mujibu wa sheria na ukiacha mawaziri ni mbunge mmoja tu aliyeeleza bayana kuunga mkono zoezi hilo, huku akisema hata kama ni kuchukiwa acha achukiwe.
Mbunge wa Buyungu (Chadema), Mwalimu Bilago, amesema huwa anajiuliza Makonda anapata wapi ujasiri, kufanya mambo ambayo tangu kuumbwa kwa nchi hii hayakuwahi kufanyika, anaonya kuwa nchi inapelekwa pabaya.
“Bunge limedhalilishwa, anataja wabunge kama ana watu wake anawatafuta aendelee kuwatafuta kimyakimya, sasa baada ya Dar es Salaam mnakwenda kutafuta watoto hao wapi? Hii biashara ni hatari sana inasababisha watu kuishi kwa hofu imefikia familia zinakaribia kuvunjika tunapigiwa simu tunashinikizwa “na wewe umo na wewe umo,” amesema Bilago.
Mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Mariam Msabaha, ametaka Makonda pamoja na wanawake walioitika wito wake katika zoezi hilo, wachukuliwe hatua za kisheria, akiamini kuwa wamekiuka sheria na Katiba ya Nchi kwa kudhalilisha watoto na wakina mama.
Mbunge wa Wete (CUF), Mbarouk Salim Ally, “Mheshimiwa Makonda lazima afahamu kuwa anachofanya ni kosa, naitaka serikali ikataze jambo hili na achukuliwe hatua za kisheria, watu wasidhalilishwe na asilete fitna kati ya akina baba na watoto kwa sababu mtoto anapozaliwa, kama anaishi vizuri na mama yake ataoneshwa tu baba yake au atamtafuta mwenyewe na kumfahamu lakini siyo kwa mazingira yale ya udhalilishaji,”
Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mwanne Mchemba amesema, “Binafsi natetea hoja hii kwasababu mpaka leo wanaume 602 wamekubali. Sheria ya mwaka 1971 inaruhusu mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa kupewa shilingi 100, wanawake wengi wamekwenda pale kwa uchungu, wanazalishwa na kuachwa mimi kama mwanamke nasema hata kama nitachukiwa nichukiwe lakini namuunga mkono Mhe. Makonda kwa alilofanya.”
Naye Waziri Mwalimu ameeleza kuwa zoezi hilo ni halali kama ilivyoelezwa awali Prof. Kabudi kwani Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 inatoa mamlaka kwa kamishna wa ustawi wa jamii, kusimamia masuala yote ya malezi ya mtoto.