Napenda kusoma mawazo ya watu wengi kwenye mitandao ya kijamii. Anayetaka kujua uwezo wetu wa kufikiri, kuchambua na kuainisha mambo, huko ndiko kunakomfaa.
Kuna dosari moja nakutana nayo. Mitandao ya kijamii ina mjijadala mingi ya kuitukuza Kenya na Wakenya. Si kwenye mitandao tu, bali lolote linalotokea kwa majirani zetu hawa limekuwa likipewa uzito mkubwa kwenye viona mbali (televisheni), redio na magazeti.
Naomba wasomaji mjipe muda kufuatilia ili kubaini habari za Tanzania zinazoandikwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari vya Kenya; na kisha msome au msikilize habari za Kenya kwenye vyombo vya habari vya Tanzania. Jambo moja lililo wazi ni kuwa habari za Tanzania kwenye vyombo vya Kenya, nyingi (si zote) zinahusu ‘mabaya’ yetu. Vyombo vya Tanzania vinapoandika au kutangaza yale yanayoihusu Kenya, mengi yanakuwa chanya!
Sijaishi nchini Kenya, lakini nimekuwapo huko mara kadhaa. Nimeona na kuyaonja maisha yao. Kwa sababu hiyo, yeyote anayedhani Wakenya wanastahili sifa tunazowapa, anajidanganya.
Tunasifu uchumi wao. Tunasifu demokrasia yao. Tunasifu utendaji kazi wao. Tunasifu mafanikio yao kwenye elimu, michezo na mambo mengine mengi.
Nitakuwa mtu wa ajabu endapo sitakubaliana na baadhi yetu kwenye maeneo ambayo Wakenya wamefanikiwa. Kwenye michezo sote tunajua. Kwenye biashara tunajua namna walivyo makini kupenya hata kusikopenyeka. Wana mbinu za kila namna za kuwafanya wafanikiwe.
Juzi nilikuwa Mbezi Mwisho, Dar es Salaam katika duka la samaki. Wateja tulikuwa wengi maana samaki wanaouzwa hapo huwa katika hali nzuri. Samaki alipoandaliwa akaachwa kwenye mashine. Mwandaaji –dada mmoja- akili yote ikawa imeishia kuangalia sinema ya ki-Nigeria! Nikashauri mwenye duka, ikiwezekana aiondoe televisheni maana inasababisha akili zote za wafanyakazi ziishie kwenye runinga. Huu ndio udhaifu wetu Watanzania. Hatuna ‘customer care’. Tunapoomba kazi huwa wanyenyekevu kweli kweli, lakini tukishaipata tunageuka wakaidi na tusiojali. Kwa hili Wakenya wametuacha mbali.
Historia ya taifa letu iko tofauti kwa kiwango kikubwa na Kenya. Maendeleo yanayoonekana Kenya leo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na wakoloni na mataifa mengine ya Ulaya na Marekani. Kwao wao, Kenya ilikuwa sehemu ya Uingereza (Ulaya). Sisi Tanganyika tulikuwa kama watoto yatima tuliosubiriwa tukipata nguvu tufukuzwe ili tuyasake maisha wenyewe.
Kielimu Kenya wamekuwa mbali kwa sababu mifumo ya elimu iliwekwa na wakoloni. Wao walichokuja kukifanya ni kuongeza tu pale walipoishia wakoloni. Mifumo ya kiuchumi ilijengwa na mabwanyenye na kwa maana hiyo hadi wanapata uhuru hawakuwa na uhaba wa viwanda wala bidhaa.
Historia ya Tanzania ni tofauti kabisa. Kitu cha maana tulichoachiwa na wakoloni (tena Wajerumani) ni reli. Karibu kila kitu kinachoonekana Tanzania ni matokeo ya juhudi zetu wenyewe. Tulikuwa na viwanda vichache mno wakati tukipata uhuru. Kazi kubwa ilifanywa na Mwalimu kujenga viwanda. Tukafanikiwa mno.
Tumejitawala tukiwa hatuna chuo kikuu. Shule na vyuo vya ufundi vilivyoachwa vilikuwapo kwa lengo moja tu la kuandaa watumishi wa serikali ya kikoloni!
Muda mfupi baada ya Uhuru serikali yetu ilifanya mambo makubwa ya kujivunia. Mafanikio yote yakavizwa na hali ya uchumi ya dunia, hasa bei ya mafuta katika miaka ya 1970; na baya zaidi ni uvamizi wa nduli Iddi Amini wa Uganda. Vita ya Kagera ilikomba rasilimali zetu nyingi na kutufanya tuyumbe kweli kweli. Juhudi nyingi za kuujenga uchumi wetu zimefanywa na zinaendelea vema.
Kama taifa, tumefanya mengi mazuri ingawa tungeweza kufanya vizuri zaidi kama si kuingiwa na ufisadi na wizi wa mali za umma. Leo tunayo mambo ya kujivunia. Tuna mafanikio katika maeneo mengi, ingawa yapo mengine hayajatengemaa, hasa kwenye elimu na michezo.
Dosari hizi hatuwezi kuzitumia kama kigezo cha kujishusha hadhi mbele ya Wakenya. Watanzania pamoja na shida zetu, bado tuna hali nzuri. Hakuna Mtanzania anayeishi maisha kama ya mkazi wa Kibera, Nairobi.
Tusijidharau. Tunayo mengi mazuri ambayo majirani zetu wanayatamani, lakini sisi wenyewe tunajiona hatuna la maana. Tumebaki kila siku kuwasifu Wakenya.
Tunu zetu kama hii ya amani na umoja ni mambo tunayopaswa kujivunia. Heri kuishi maskini katika nchi yenye umoja na amani kuliko kuwa tajiri katika taifa lililojaa ubaguzi, ukabila na shida kwa wananchi. Leo Mtanzania anaweza kuwa na shida, lakini hakuna asiyekuwa na kipande cha ardhi anachokitumia kwa shughuli anayotaka. Haya Kenya hayapo. Hoja ni kuwa tutumie fursa tulizo nazo sasa.
Dhana ya kwamba Kenya wametuzidi kimaendeleo si ya kujidhalilisha. Swali hapa ni je, hayo maendeleo ni ya kina nani? Ni ya wananchi wote-maskini na matajiri au ni ya matajiri wachache? Wajibu wetu ni kuhakikisha tunatumia fursa tulizonazo kuujenga uchumi na maisha yetu wenyewe. Tumeanza vizuri. leo maduka mengi hata yale ya mpakani na Kenya yana bidhaa za Tanzania. Haya ni mafanikio makubwa.
Kushinda au kukesha tukiperuzi mitandao ya kijamii tukiwamwagia sifa Wakenya na sisi tukijidharau hakuwezi kuyabadili maisha yetu kamwe. Tutayabadili maisha kwa kutambua tunataka nini na tufanye nini ili kuyafikia matamanio hayo. Tusijiradhau. Tusijibeze wala tusijione wanyonge. Tukiamua kwa pamoja Tanzania ndiyo superpower katika ukanda huu. Uwezo na rasilimali za kuwa hivyo tunavyo.