Na Deodatus Balile
Mpendwa msomaji salaam. Wiki iliyopita sikuwa katika safu hii. Nilisafiri kwenda Kisarawe kidogo kwa ajili ya kupeleka taarifa za kilimo cha muhogo. Niliitwa na viongozi wa wananchi wa Kijiji cha Gwata, wilayani Kisarawe waliotaka kufahamu taratibu na jinsi ya kupata fursa ya kilimo cha muhogo nchini. Taratibu zinaendelea na nimewajulisha viongozi wa Gwata na kupitia safu hii nijibu swali hili ninaloulizwa kisha nirejee katika mada ya leo.
Sitanii, naomba kuwaondoa Watanzania katika mawazo ya kupata wawekezaji kutoka nje ya nchi. Kila anayepiga simu kwangu swali la kwanza ni iwapo nimepata mwekezaji kutoka China. Mimi nawambia ndugu zangu tulichopata kama Tanzania ni soko la muhogo China na si wawekezaji kutoka China. Watanzania tunalo jukumu la kuunganisha nguvu tukalima muhogo na mwisho wa siku tukauza nchini China kama wanavyofanya wakulima wa pamba, kahawa, korosho, mahindi na wengine baada ya msimu.
Hata hivyo, nikiri na kuwapongeza wananchi kwa hamu kubwa mliyoionyesha ya kuingia katika kilimo cha kibiashara ya muhogo. Hii inanipa moyo kuwa dhana ya Watanzania kuwekeza katika viwanda imeanza kupata njia. Tunachohitaji ni kuelekezwa taratibu za kufikia lengo hili. Kilimo cha muhogo na mazao mengine ni fursa ya wananchi kumiliki viwanda na kujenga utajiri halali.
Sitanii, leo kichwa cha makala hii kinasema “Bomu la watu laja Afrika.” Wiki mbili zilizopita nimepata fursa ya kuhudhuria hafla ya uzindunzi wa kitabu kiitwacho “Making Africa Work”. Tafsiri isiyo rasmi jina la kitabu hiki linamanisha “Mbinu za Afrika kujikwamua kiuchumi.” Katika uzinduzi huu alikuwapo Rais (mstaafu) wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Alitarajiwa pia kuwapo Rais (mstaafu) wa Nigeria, Olusegun Obasanjo. Hakufika ila alitumia ujumbe wa video. Kitabu hiki kimeandikwa na watu wanne amabo ni wabobezi katika utafiti. Waandishi hao ni Greg Mills, Olusegun Obasanjo, Jeffrey Herbst na Dickie Davis. Taasisi ya Brenthurst Foundation ya Johannesburg, Afrika Kusini ndiyo iko nyuma ya mpango huu wa kuikomboa Afrika kiuchumi.
Katika makala zijazo nitaelezea ujumbe uliosheheni katika kitabu hiki, ila leo natoa usuli. Taarifa za World Fact Book, zinaonyesha kuwa Tanzania kwa sasa ina watu milioni 58 na idadi itaongezeka kufikia watu milioni 62 (2020), milioni 72 (2025), milioni 83 (2030), milioni 95 (2035), milioni 109 (2040), milioni 123 (2045) na milioni 138 (2050). Afika kwa sasa inatajwa kuwa na watu bilioni 1.2 na mwaka 2050 itakuwa na watu bilioni 2.5, huku mwaka 2100 ikiwa na watu bilioni 5.7 sawa na nusu ya watu wote duniani.
Sitanii, katika uzinduzi huo alikuwapo pia Waziri wa Fedha wa zamani wa Zimbabwe, Tendai Biti na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe. Rais Mkapa katika uzinduzi huo, amezungumzia bomu la idadi ya watu, ajira, wanafunzi kushindwa kuhitimu elimu ya msingi baada ya kuingia na ajira zisizokidhi haja. “Mtu yupo kwenye ajira, ila anacholipwa ni sawa na kutoajiriwa,” alisema Mkapa na kuongeza kuwa inahitajika mikakati ya makusudi kuwa na mipango thabiti jinsi ya kuwapatia ajira na hifadhi watu hawa watakaokuja duniani miaka si mingi ijayo.
Tendai Biti ameakisi maneno ya Obasanjo aliyezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinakuwa na mambo manne. Uongozi bora, Umeme, miundombinu na chakula. Obasanjo katika ujumbe wake amesema bila maandalizi hayo, Afrika kwa idadi hii ya watu inayokuja litageuka bara la vita na uasi.
Uongozi wa kidemokrasia amesema unatoa fursa ya watu kutoa mawazo, wakasikilizwa na kupanga kwa pamoja kisha utekelezaji wa makubaliano unakuwa rahisi. Kitabu hiki kinathibitisha kuwa nchi zilizowekeza katika demokrasia shirikishi, zimepiga hatua katika maendeleo ya kweli kiuchumi. Pia, hakuna nchi inayoweza kuendelea bila umeme, barabara, reli, viwanja vya ndege na ndege, bila kusahau usalama wa chakula.
Je, sisi Tanzania tumejianda kupokea idadi hii ya watu? Afrika inayo makazi, chakula, umeme na uongozi bora wa kupanga jinsi ya kuhimili ongezeko hili la watu? Tukutane wiki ijayo.