Serikali imeeleza kuwa inalinda thamani ya Shilingi kwa kudhibiti mfumuko wa bei ya huduma na bidhaa, kuhamasisha usafirishaji na uuzaji wa bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi kupitia program ya “Export Credit Guarantee Scheme” na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za Kigeni.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Devotha Mathew Minja aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kulinda thamani ya Shilingi kwa kuwa wapo wamiliki wa majengo ambao wanapangisha majengo kwa kutumia fedha za kigeni kama vile Dola ya Kimarekani badala ya fedha ya Kitanzania hivyo kusababisha kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa matumizi ya fedha za kigeni sambamba na Shilingi ya Tanzania hapa nchini yanasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 (The Foreign Exchange Act, 1992), Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwaka 2006 na Tamko la Serikali la mwaka 2007 kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kulipia bidhaa na huduma katika soko la ndani.
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa mwezi Desemba 2017, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), alitoa tamko kwa umma kuwa kuanzia Januari Mosi, 2018 bei zote hapa nchini zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania zikijumuisha kodi ya nyumba za kuishi na ofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei ya vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.
“Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni, ambapo zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, visa kwa wageni na gharama za viwanja vya ndege na hoteli, hata hivyo wageni hao wanapaswa kutambuliwa kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa Kampuni”. Alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha aliongeza kuwa viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka bei hizo katika sarafu vinatakiwa kuwekwa wazi na visizidi vile vya soko, vilevile ni benki na maduka ya fedha za kigeni pekee ndiyo yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.
Katika maswali ya nyongeza ya Mbunge huyo alitaka kujua sababu zinazofanya baadhi ya Taasisi kuendelea kupata na kutoa huduma kwa Dola, pia alihoji Serikali itapitia lini upya Sheria zake ili kuwa na sheria itakayozuia matumizi ya fedha za Kigeni kama ilivyo kwa nchi ya Afrika Kusini.
Dkt. Kijaji alisema kwa kuwa wajibu wa marekebisho na kupitisha Sheria ni wa Bunge hivyo basi, iwapo sheria iliyopo ina upungufu ni vema kukafanyika maboresho kupitia Bunge.“Ikumbukwe kuwa katika misingi ya Uchumi mambo yanayosababisha kushuka au kudorora kwa thamani ya fedha yeyote duniani ni pamoja na Nakisi ya Urari wa Biashara ambapo kwa Serikali ya Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa katika kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini” alisema Dkt. Kijaji.
Alibainisha kuwa Mfumuko wa bei na tofauti ya Msimu huchangia kushuka kwa thamani ya fedha ambapo Tanzania inaendelea kudhibiti mfumuko huo na Serikali tayari imefunga zaidi ya maduka 92 ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo yameshindwa kufuata sheria na taratibu za nchi ili kudhibiti maduka hayo kuwa kichaka cha kusafirisha fedha za Tanzania isivyo halali mambo ambayo yanaonesha juhudi za Serikali kuimarisha kwa kiwango kikubwa thamani ya shilingi.