Serikali imeanza mchakato wa kumchukulia hatua nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Nandy baada ya kusambaa mtandaoni kwa video inayomuonesha akiwa na msanii mwenzake Bilnass katika faragha.

Video hiyo iliyoanza kusambaa juzi katika mitandao ya kijamii, inawaonesha Nandy na Rapa Bilnass, wakiwa kitandani katika hali ya utupu.

Mashabki na wadau wa muziki wamejitokeza kulaani kitendo hicho, wakisema kimevuka mipaka na kudai kuwa serikali inapaswa kuingilia kati.

“Video ile inamshusha hadhi Nandy ambaye nyota yake imeanza kung’aa, ni jambo la kushangaza kwa nini waweke video ile ya faragha mitandaoni wakati zile picha za mwanzo zilizowaonesha wakiwa pamoja zilitosha kuthibitisha kuwa wao ni wapenzi,” alisema mtangazaji wa redio moja.

Katika mitandao ya kijamii, watu wengi waliamua kuwatolea uvivu kwa kueleza kitendo hicho kimewakasirisha na kwamba kinakiuka maadili.

Hata hivyo, Nandy kupitia akaunti yake ya Instagram aliomba radhi kutokana na tukio hilo na kuwaomba Watanzania kumuombea kwa sababu hayuko sawa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey mngereza alipoulizwa kuhusiana na tukio hili alieleza kwamba, wameitisha kikao maalumu ili kuangalia hatua za kuwachukulia wasanii hao.

“Nipo kwenye kikao cha kujadili suala hilo, nipigie baada ya saa tatu utapata kila kitu kuhusu jambo hilo,” alisema Mngereza.