“Hii pongezi ya Rais ni kwa sababu alipokea taarifa ya utendaji ya jiji la Arusha na tangu alipoingia nilimweleza mambo ambayo tumefanya kwa mfano amepongeza jitihada kubwa ya ujenzi wa madarasa, tunapandisha vituo vya afya mara moja na dispensary kwa ujumla tano, hospitali ya wilaya, barabara za lami, barabara za vumbi na juzi tumetangaza tenda ya kilometa 10 za lami katika jiji la Arusha ambapo barabara ya Njiro, Kwa Mlombo, Sombetini zinaenda kujengwa lami pamoja na barabara ya Ngarenalo kwangu mimi ni heshima na hii heshima nimeipokea kwa niamba ya wananchi wa Jiji la Arusha.”

Hayo ni maneno ya Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro (CHADEMA) akizungumza muda mfupi baada ya kupongezwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli kuwwa ni mmoja wa watu wanaopenda maendeleo na wanaojituma kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi wake.

Rais Dkt Magufuli aliyasema hayo Aprili 7 mwaka huu alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jiji la Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwenye maonesho ya shughuli mbalimbali za Polisi.

Alisema kuwa anampongeza Meya wa Arusha kwa sababu yeye kama kiongozi wa nchi anapenda watu wanaoleta maendeleo na kwa vile Meya Lazaro ni mmoja wao, licha ya kuwa yupo chama kingine lakini hana budi kumpongeza kwa jitihada kubwa ambazo amekuwa akizionesha kuhakikisha kwamba watu wa Arusha wanapata maendeleo.

Akizungumzia kitendo hicho, meya huyo alisema kuwa, kupongezwa kwake na Rais pia ni funzo kwa viongozi wengine ambao wamekuwa wakihama kutoka CHADEMA na kwenda CCM kwa kigezo cha kuunga mkono serikali na kudai kuwa ukitaka kufanya hivyo unachotakiwa kutekeleza tu yale uliyoahidi kwa wananchi wako na si kwa kigezo cha kuhama chama.

Wale ambao walikuwa wanabeza na hawatambui sasa wametambua kuwa Meya wao anapongezwa na Rais Magufuli mbele ya halaiki ya watu, mbele ya polisi, mbele ya Mkuu wa Majeshi hivyo Rais anaona kazi tunayofanya, na niwaambie wananchi hakuna sababu ya kiongozi wa kuchaguliwa kuhama, ukitaka kutekeleza wajibu wako na kuunga mkono serikali unatakiwa ufanye kazi ambayo umeahidi wananchi wako. Mimi leo napongezwa nikiwa ndani ya CHADEMA, nikiwa Meya wa CHADEMA na diwani wa CHADEMA kwangu mimi ni heshima” alisisitiza.